71. SURAT NUH'
(Imeteremka
Makka)
Sura hii tukufu imefafanua
kisa cha Nuh'u a.s. pamoja na kaumu yake. Ikasimulia khabari za wito wake kwa
dhaahiri, kisha kwa siri na kwa dhaahiri. Na ikaeleza mashtaka yake kumshtakia
Mwenyezi Mungu juu ya walivyo mpuuza, na inda walio mfanyia, na ikasajili
kukakamia kwao kuyaabudu masanamu mpaka wakastahiki kupata adhabu ya Mwenyezi
Mungu. Nuh'u alipo kata tamaa nao kuukubali wito wake, aliwaapiza wahiliki na
waangamie, na akajiombea nafsi yake, na wanawe, Waumini wanaume, na Waumini
wanawake, wapate msamaha.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU
MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Hakika Sisi tulimtuma Nuh'u kwa watu wake: Uwaonye kaumu
yako kabla ya kuwafikia adhabu chungu.
2. Akasema: Enyi watu wangu! Kwa hakika mimi ni mwonyaji wa
dhaahiri kwenu,
3. Ya kwamba mumuabudu Mwenyezi Mungu, na mumche Yeye, na
mumt'ii.
4. Atakughufirieni madhambi yenu, na atakuakhirisheni mpaka
muda ulio wekwa. Hakika muda wa Mwenyezi Mungu utapo fika haucheleweshwi. Laiti
mngejua!
5. Akasema: Ee Mola wangu Mlezi! Hakika mimi nimewaita watu
wangu usiku na mchana,
6. Lakini wito wangu haukuwazidisha ila kukimbia.
7. Na hakika mimi kila nilipo waita ili upate kuwaghufiria,
walijiziba masikio yao kwa vidole vyao, na wakajigubika nguo zao, na wakakamia,
na wakatakabari vikubwa mno!
8. Tena niliwaita kwa uwazi,
9. Kisha nikawatangazia kwa kelele, tena nikasema nao kwa
siri.
10. Nikasema: Ombeni msamaha kwa Mola wenu Mlezi; hakika
Yeye ni Mwingi wa kusamehe.
11. Atakuleteeni mvua inyeshe mfululizo.
12. Na atakupeni mali na wana, na atakupeni mabustani na
atakufanyieni mito.
13. Mna nini hamweki heshima ya Mwenyezi Mungu?
14. Na hali Yeye kakuumbeni daraja baada ya daraja?
15. Kwani hamwoni jinsi Mwenyezi Mungu alivyo ziumba mbingu
saba kwa matabaka?
16. Na akaufanya mwezi ndani yake uwe nuru, na akalifanya
jua kuwa taa?
17. Na Mwenyezi Mungu amekuotesheni katika ardhi kama
mimea.
18. Kisha atakurudsheni humo na atakutoeni tena.
19. Na Mwenyezi Mungu amekukunjulieni ardhi kama busati.
20. Ili mtembee humo katika njia zilizo pana.
21. Nuh'u akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika hao wameniasi,
na wamemfuata yule ambaye mali yake na wanawe hawakumzidishia ila khasara.
22. Na wakapanga vitimbi vikubwa.
23. Na wakasema: Msiwaache miungu yenu, wala msimwache
Wadda wala Suwaa' wala Yaghutha, wala Yau'qa, wala Nasra.
24. Na hao walikwisha wapoteza wengi, wala usiwazidishie
walio dhulumu ila kupotea.
25. Basi kwa ajili ya makosa yao waligharikishwa
wakaingizwa Motoni, wala hawakuwapata wa kuwanusuru badala ya Mwenyezi Mungu.
26. Na Nuh'u akasema: Mola wangu Mlezi! Usimwache juu ya
ardhi mkaazi wake yeyote katika makafiri!
27. Hakika ukiwaacha watawapoteza waja wako, wala wao
hawatazaa ila waovu makafiri.
28. Mola wangu Mlezi! Nighufirie mimi na wazazi wangu, na
kila aliye ingia nyumbani mwangu kuwa ni mwenye kuamini, na Waumini wote
wanaume, na Waumini wanawake. Na wala usiwazidishie walio dhulumu ila kupotea.
|