101 - 150
101. Na alipo wajia Mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu, mwenye
kuthibitisha yale waliyo nayo, kundi moja miongoni mwa wale walio pewa Kitabu lilitupa
Kitabu cha Mwenyezi Mungu hicho nyuma ya migongo yao kama kwamba hawajui.
102. Na wakafuata yale waliyo zua mashet'ani kuuzulia
ufalme wa Su leiman. Na wala Suleiman hakukufuru, bali mashet'ani ndio walio
kufuru, wakiwafundisha watu uchawi, na yaliyo teremshwa kwa Malaika wawili,
Haaruta na Maaruta katika Baabil. Wala hao hawakumfundisha yeyote mpaka
wamwambie: Hakika sisi ni mtihani; basi usikufuru. Wakajifunza kwa hao wawili
yale ya kumfarikisha mtu na mkewe. Wala hawawezi kumdhuru mtu ila kwa kutaka
Mwenyezi Mungu. Na wanajifunza yatayo wadhuru wala hayawanufaishi. Na hakika
wanajua kwamba aliye khiari haya hatakuwa na fungu lolote katika Akhera. Na hakika
ni kiovu mno walicho jiuzia nafsi zao laiti wangelijua.
103. Na lau kuwa wangeamini na wakaogopa, bila ya shaka
malipo yatokayo kwa Mwenyezi Mungu yange kuwa bora. Laiti wangeli kuwa wanajua!
104. Enyi mlio amini! Msiseme: "Raa'ina", na
semeni: "Ndhurna". Na sikieni! Na makafiri watapata adhabu chungu.
105. Walio kufuru miongoni mwa watu wa Kitabu na
washirikina hawapendi mteremshiwe kheri yoyote kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Na
Mwenyezi Mungu humkusudia kumpa rehema yake ampendaye. Na Mwenyezi Mungu ni
mwenye fadhila kubwa.
106. Ishara yoyote tunayo ifuta au tunayo isahaulisha
tunailetea iliyo bora kuliko hiyo, au iliyo mfano wake. Hujui kwamba Mwenyezi
Mungu ni Muweza wa kila kitu?
107. Hujui kwamba Mwenyezi Mungu ana ufalme wa mbingu na
ardhi? Nanyi hamna mlinzi wala msaidizi isipo kuwa Mwenyezi Mungu.
108. Au mnataka kumwomba Mtume wenu kama alivyo ombwa Musa
zamani? Na anaye badilisha Imani kwa ukafiri bila ya shaka huyo ameipotea njia
iliyo sawa.
109. Wengi miongoni mwa watu wa Kitabu wanatamani lau wange
kurudisheni nyinyi muwe makafiri baada ya kuamini kwenu, kwa ajili ya uhasidi
uliomo ndani ya nafsi zao, baada ya kwisha wapambanukia Haki. Basi sameheni na
wachilieni mbali mpaka Mwenyezi Mungu atapo leta amri yake. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Muweza wa kila kitu.
110. Na shikeni Sala na toeni Zaka; na kheri mtakazo
jitangulizia nafsi zenu mtazikuta kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu
anayaona mnayo yafanya.
111. Na walisema: Hataingia Peponi ila aliyekuwa Yahudi au
Mkristo. Hayo ni matamanio yao. Sema: Leteni ushahidi wenu kama nyinyi ni
wasema kweli.
112. Sivyo
hivyo! Yeyote anaye elekeza uso wake kwa Mwenyezi Mungu naye ni mtenda mema,
basi ana malipo yake kwa Mola wake Mlezi, wala haitakuwa khofu juu yao wala
hawatahuzunika.
113. Na
Mayahudi husema: Wakristo hawana lao jambo. Na Wakristo husema: Mayahudi hawana
lao jambo. Na ilhali wote wanasoma Kitabu hicho hicho (Biblia). Na kadhaalika
walisema wale wasio jua kitu mfano wa kauli yao hii. Basi Mwenyezi Mungu
atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika yale waliyo kuwa wakikhitilafiana.
114. Na ni
nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye zuia misikiti ya Mwenyezi Mungu kutajwa
ndani yake jina lake na akajitahidi kuiharibu? Watu hao haitawafalia kuingia
humo ila nao wanaogopa. Duniani watapata hizaya na Akhera watapata adhabu
kubwa.
115. Na
mashariki na magharibi ni za Mwenyezi Mungu. Basi kokote mnako elekea, huko
Mwenyezi Mungu yupo. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye wasaa na Mjuzi.
116. Na ati wanasema: Mwenyezi Mungu ana mwana. Subhanahu!
Ametakasika na hayo. Bali vyote viliomo mbinguni na duniani ni vyake. Vyote
vinamt'ii Yeye.
117. Yeye ndiye Muumba wa mbingu na ardhi pasina ruwaza; na
anapo taka jambo basi huliambia tu: Kuwa! Nalo huwa.
118. Na walisema wale wasio jua kitu: Mbona Mwenyezi Mungu
hasemi nasi au zikatufikia Ishara. Kama hivyo walisema wale walio kuwa kabla
yao mfano wa kauli yao hii. Nyoyo zao zimefanana. Hakika Sisi tumeziweka wazi
Ishara kwa watu wenye yakini.
119. Hakika Sisi tumekutuma kwa Haki uwe mbashiri, na
mwonyaji. Na wala hutaulizwa juu ya watu wa Motoni.
120. Mayahudi hawawi radhi nawe, wala Wakristo, mpaka
ufuate mila yao. Sema: Hakika uwongofu wa Mwenyezi Mungu ndio uwongofu. Na kama
ukifuata matamanio yao baada ya ujuzi ulio kwisha kujia, hutapata mlinzi wala
msaidizi kwa Mwenyezi Mungu.
121. Wale tulio wapa Kitabu, wakakisoma kama ipasavyo
kusomwa, hao ndio kweli wanakiamini. Na wanao kikataa basi hao ndio wenye
kukhasiri.
122. Enyi Wana wa Israili! Kumbukeni neema yangu niliyo
kuneemesheni, na hakika Mimi nikakufadhilisheni kuliko wengineo wote.
123. Na iogopeni siku ambayo hatamfaa mtu mwenziwe kwa
lolote, wala hakitakubaliwa kwake kikomboleo, wala maombezi hayatamfaa, wala
hawatanusuriwa.
124. Na Mola wake Mlezi alipo mjaribu Ibrahim kwa kumpa
amri fulani, naye akazitimiza, akamwambia: Hakika Mimi nitakufanya uwe mwongozi
wa watu. Akasema: Je, na katika
vizazi vyangu pia? Akasema: Ahadi yangu haitawafikia wenye kudhulumu.
125. Na
kumbukeni tulipo ifanya ile Nyumba (ya Alkaaba) iwe pahala pa kukusanyikia watu
na pahala pa amani. Na alipo kuwa akisimama Ibrahim pafanyeni pawe pa kusalia.
Na tuliagana na Ibrahim na Ismail: Itakaseni Nyumba yangu kwa ajili ya wanao
izunguka kwa kut'ufu na wanao jitenga huko kwa ibada, na wanao inama na
kusujudu.
126. Na alipo sema Ibrahim: Ee Mola wangu Mlezi! Ufanye huu
uwe mji wa amani, na uwaruzuku watu wake matunda, wale wanao muamini Mwenyezi
Mungu na Siku ya Mwisho. Akasema: Na mwenye kukufuru pia nitamstarehesha
kidogo, kisha nitamsukumiza kwenye adhabu ya Moto, napo ni pahala pabaya mno pa
kurejea.
127. Na kumbukeni Ibrahim na Ismail walipo inyanyua misingi
ya ile Nyumba wakaomba: Ewe Mola Mlezi wetu! Tutakabalie! Hakika Wewe ndiye
Msikizi Mjuzi.
128. Ewe Mola Mlezi wetu! Tujaalie tuwe ni wenye kusilimu kwako,
na pia miongoni mwa vizazi vyetu wawe umma ulio silimu kwako. Na utuonyeshe
njia za ibada yetu na utusamehe. Bila shaka Wewe ndiye Mwenye kusamehe Mwenye
kurehemu.
129. Ewe Mola Mlezi wetu! Waletee Mtume anaye tokana na
wao, awasomee Aya zako, na awafundishe Kitabu na hikima na awatakase. Hakika
Wewe ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
130. Na nani atajitenga na mila ya Ibrahim isipo kuwa
anayeitia nafsi yake katika upumbavu? Na kwa yakini Sisi tulimteuwa yeye katika
dunia; na hakika yeye katika Akhera atakuwa miongoni mwa watu wema.
131. Na Mola wake Mlezi alipo mwambia: Silimu, Nyenyekea!
Alinena: Nimesilimu, nimenyenyekea kwa Mola wa walimwengu wote.
132. Na Ibrahim akawausia wanawe, na pia Yaaqub: Enyi
wanangu! Hakika Mwenyezi Mungu amekuteulieni Dini hii; basi msife ila nanyi
mmekuwa Waislamu, wanyenyekevu.
133. Je! Mlikuwapo yalipo mfikia Yaaqub mauti, akawaambia
wanawe: Mtamuabudu nani baada yangu? Wakasema: Tutamuabudu Mungu wako na Mungu
wa baba zako, Ibrahim na Ismail na Is- hak, Mungu Mmoja tu, na sisi tunasilimu kwake.
134. Hao ni watu walio kwisha pita. Watapata waliyo
yachuma, nanyi mtapata mtakayo yachuma; wala hamtaulizwa nyinyi waliyo kuwa
wakiyafanya wao.
135. Na wakasema: Kuweni Mayahudi au Wakristo ndio
mtaongoka. Sema: Bali tunashika mila ya Ibrahim mwongofu, wala hakuwa katika
washirikina.
136. Semeni nyinyi: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na yale
tuliyo teremshiwa sisi, na yaliyo teremshwa kwa Ibrahim na Ismail na Is-hak na
Yaakub na wajukuu zake, na waliyo pewa Musa na Isa, na pia waliyo pewa Manabii
wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi; hatutafautishi baina ya yeyote katika hao,
na sisi tumesilimu kwake.
137. Basi wakiamini kama mnavyo amini nyinyi, itakuwa kweli
wameongoka. Na wakikengeuka basi wao wamo katika upinzani tu. Na Mwenyezi Mungu
atakutosheni kukukingeni na shari yao, na Yeye ndiye Msikizi, Mjuzi.
138. Huko ndiko kupaka rangi kwa Mwenyezi Mungu, na nani
aliye mbora wa kupaka rangi kuliko Mwenyezi Mungu? Na sisi ni wenye kumuabudu
Yeye tu.
139. Sema: Mnahojiana nasi juu ya Mwenyezi Mungu, naye ni
Mola wetu Mlezi na Mola wenu Mlezi, na sisi tuna vitendo vyetu na nyinyi mna
vitendo vyenu? Nasi tunamsafia Yeye tu.
140. Au mnasema kuwa Ibrahim na Ismail na Is-hak na Yaakub
na wajukuu zao walikuwa Mayahudi au Wakristo? Sema: Je, nyinyi mnajua zaidi au
Mwenyezi Mungu? Na ni nani mwenye kudhulumu zaidi kuliko yule aliye ficha
ushahidi alio nao utokao kwa Mwenyezi Mungu? Na Mwenyezi Mungu si mwenye
kughafilika na hayo myafanyayo.
141. Hao ni watu walio kwisha pita. Wao watapata waliyo
yachuma, na nyinyi mt apata mliyo yachuma, wala hamtaulizwa nyinyi yale waliyo
kuwa wakifanya wao.
142. WAPUMBAVU miongoni mwa watu watasema: Nini kilicho
wageuza kutoka kibla chao walicho kuwa wakikielekea? Sema: Mashariki na
Magharibi ni ya Mwenyezi Mungu; Yeye humwongoa amtakaye kwenye njia iliyo
nyooka.
143. Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa wasitani,
ili muwe mashahidi juu ya watu, na Mtume awe ni shahidi juu yenu. Na
hatukukifanya kibla ulicho kuwa nacho ila tupate kumjua yule anaye mfuata Mtume
na yule anaye geuka akarejea nyuma. Na kwa yakini hilo lilikuwa jambo gumu
isipo kuwa kwa wale alio waongoa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu hakuwa
mwenye kuipoteza Imani yenu. Kwani Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa watu na Mwenye
kuwarehemu.
144. Kwa yakini tukiona unavyo geuza geuza uso wako
mbinguni. Basi tutakuelekeza kwenye Kibla ukipendacho. Basi elekeza uso wako
upande wa Msikiti Mtakatifu; na popote mnapokuwa zielekezeni nyuso zenu upande
huo; na hakika wale walio pewa Kitabu wanajua kwamba hiyo ni haki itokayo kwa
Mola wao Mlezi. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na yale wanayo yatenda.
145. Na hao walio pewa Kitabu, hata ukiwaletea hoja za kila
namna, hawatafuata Kibla chako; wala wewe hutafuata kibla chao, wala baadhi yao
hawatafuata kibla cha wengineo; na kama ukiyafuata matamanio yao baada ya
kukufikia ujuzi, hakika hapo utakuwa miongoni mwa wenye kudhullumu.
146. Wale tulio wapa Kitabu wanayajua haya kama wanavyo
wajua watoto wao; na kuna kikundi katika wao huificha haki na hali wanajua.
147. Haki inatoka kwa Mola wako Mlezi. Basi usiwe miongoni
mwa wanao fanya shaka.
148. Na kila mmoja anao upande anao elekea. Basi
shindanieni mema. Popote mlipo Mwenyezi Mungu atakuleteni nyote pamoja. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
149. Na popote wendako elekeza uso wako kwenye Msikiti
Mtakatifu. Na hiyo ndiyo Haki itokayo kwa Mola wako Mlezi. Na Mwenyezi Mungu si
mwenye kughafilika na mnayo yatenda.
150. Na popote wendako elekeza uso wako kwenye Msikiti
Mtakatifu. Na popote mlipo elekezeni nyuso zenu upande huo ili watu wasiwe na
hoja juu yenu, isipokuwa wale walio dhulumu miongoni mwao. Basi msiwaogope wao,
lakini niogopeni Mimi - na ili nikutimizieni neema yangu, na ili mpate
kuongoka.
|