77. SURAT AL-MURSALAAT
(Imeteremka
Makka)
Lilio muhimu kabisa katika
yaliyo kusanywa na Sura hii tukufu ni maneno yaliyo khusu kufufuliwa, na
Kiyama, na dalili za kuthibitisha kuwa kitatokea, na kutishwa kwa waliyo
yakataa hayo, na kurudishwa kutishwa huko kwa "Ole wao" mara kumi, na
kuwatisha kwa unyonge na adhabu itayo wapata; na kubashiriwa wachamngu kwa
starehe na neema watazo zikuta, na mwisho wake masaibu yatayo wapata makafiri
wasio iamini Qur'ani.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Naapa kwa zinazo tumwa kwa upole!
2. Na zinazo vuma kwa kasi!
3. Na zikaeneza maeneo yote!
4. Na zinazo farikisha zikatawanya!
5. Na zinazo peleka mawaidha!
6. Kwa kuudhuru au kuonya,
7. Hakika mnayo ahidiwa bila ya shaka yatakuwa!
8. Wakati nyota zitakapo futwa,
9. Na mbingu zitakapo pasuliwa,
10. Na milima itakapo peperushwa,
11. Na Mitume watakapo wekewa wakati wao,
12. Kwa siku gani hiyo wamewekewa muda huo?
13. Kwa siku ya kupambanua!
14. Na nini kitakacho kujuulisha siku ya kupambanua ni
nini?
15. Ole
wao, siku hiyo hao wanao kanusha!
16. Kwani hatukuwaangamiza walio tangulia?
17. Kisha tukawafuatilizia walio fuatia?
18. Ndio kama hivi tuwatendavyo wakosefu!
19. Ole
wao siku hiyo hao wanao kanusha!
20. Kwani
hatukukuumbeni kwa maji ya kudharauliwa?
21. Kisha
tukayaweka mahali pa utulivu madhubuti?
22. Mpaka muda maalumu?
23. Tukakadiria na Sisi ni wabora wa kukadiria.
24. Ole
wao siku hiyo hao wanao kanusha!
25. Kwani
hatukuifanya ardhi yenye kukusanya
26. Walio hai na maiti?
27. Na ndani yake tukaweka milima mirefu yenye kuthibiti,
na tunakunywesheni maji matamu?
28. Ole
wao siku hiyo hao wanao kanusha!
29.
Nendeni kwenye adhabu mliyo kuwa mkiikanusha!
30.
Nendeni kwenye kivuli chenye mapande matatu!
31.
Hakikingi moto, wala hakiwaepushi na mwako.
32. Hakika
Moto huo unatoa macheche kama majumba!
33. Kama
kwamba ni ngamia wa rangi ya manjano!
34. Ole
wao siku hiyo hao wanao kanusha!
35. Hii ni
siku ambayo hawatatamka kitu,
36. Wala
hawataruhusiwa kutoa udhuru.
37. Ole
wao siku hiyo hao walio kanusha!
38. Hii
ndiyo siku ya kupambanua. Tumekukusanyeni nyinyi na walio tangulia.
39. Ikiwa
mnayo hila, nifanyieni hila Mimi!
40. Ole
wao siku hiyo hao walio kanusha!
41. Hakika
wachamngu watakuwa katika vivuli na chemchem,
42. Na
matunda wanayo yapenda,
43. Kuleni
na kunyweni kwa furaha kwa yale mliyo kuwa mkiyatenda.
44. Hakika
ndio kama hivyo tunavyo walipa watendao mema.
45. Ole
wao siku hiyo hao wanao kanusha!
46. Kuleni
na mjifurahishe kidogo tu. Hakika nyinyi ni wakosefu!
47. Ole
wao siku hiyo hao wanao kanusha!
48. Na wakiambiwa: Inameni! Hawainami.
49. Ole
wao siku hiyo hao wanao kanusha!
50. Basi maneno gani baada ya haya watayaamini?
|