80. SURAT A'BASA
(Imeteremka
Makka)
Sura hii imeanza kwa
kumlaumu Nabii Muhammad s.a.w. kwa kumpuuza Ibnu Ummi Maktoum alipo mjia
kutafuta ilimu na uwongofu. Naye Nabii s.a.w. alikuwa kashughulika kuwalingania
Dini baadhi ya mabwana wa Kikureshi kwa kutaraji watamwitikia, ili kwa kusilimu
kwao wange silimu watu wengi. Kisha Sura inamkumbusha binaadamu kwa neema alizo
pewa na Mwenyezi Mungu tangu kuumbwa kwake mpaka kufufuliwa kwake. Na
ikakhitimisha kwa kusimulia khabari za Siku ya Kiyama, ikibainisha kwamba watu
siku hiyo ni makundi mawili, kundi la Waumini lenye furaha, na kundi la
makafiri wapotovu.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Alikunja kipaji na akageuka,
2. Kwa sababu alimjia kipofu!
3. Na nini kitakujuulisha pengine yeye atatakasika?
4. Au atawaidhika, na mawaidha yamfae?
5. Ama ajionaye hana haja,
6. Wewe
ndio unamshughulikia?
7. Na si juu yako kama hakutakasika.
8. Ama
anaye kujia kwa juhudi,
9. Naye anaogopa,
10. Ndio wewe unampuuza?
11. Sivyo
hivyo! Huku ni kukumbushana.
12. Basi
anaye penda akumbuke.
13. Yamo katika kurasa zilizo hishimiwa,
14. Zilizo inuliwa, zilizo takaswa.
15. Zimo mikononi mwa Malaika waandishi,
16.
Watukufu, wema.
17.
Ameangamia mwanaadamu! Nini kinacho mkufurisha?
18. Kwa
kitu gani amemuumba?
19. Kwa
tone la manii, akamuumba na akamkadiria.
20. Kisha
akamsahilishia njia.
21. Kisha
akamfisha, akamtia kaburini.
22. Kisha apendapo atamfufua.
23. La! Hajamaliza aliyo muamuru.
24. Hebu mtu na atazame chakula chake.
25. Hakika Sisi tumemimina maji kwa nguvu,
26. Tena tukaipasua pasua ardhi kwa nguvu,
27. Kisha tukaotesha humo nafaka,
28. Na zabibu, na mimea ya majani,
29. Na mizaituni, na mitende,
30. Na bustani zenye miti iliyo songana baraabara,
31. Na matunda, na malisho ya wanyama;
32. Kwa manufaa yenu na mifugo yenu.
33. Basi utakapo kuja ukelele,
34. Siku ambayo mtu atamkimbia nduguye,
35. Na mamaye na babaye,
36. Na
mkewe na wanawe -
37. Kila
mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na lake la kumtosha.
38. Siku
hiyo ziko nyuso zitazo nawiri,
39. Zitacheka,
zitachangamka;
40. Na nyuso
siku hiyo zitakuwa na mavumbi,
41. Giza totoro litazifunika,
42. Hao ndio makafiri watenda maovu.
|