83. SURAT AL-MUT'AFFIFIIN
(Imeteremka
Makka)
Imeanzia Sura hii kwa onyo
kali kwa huyo anaye jipimia mwenyewe sawa na akampimia mtu mwingine kwa
upungufu; na ikaeleza hayo kwa wayatendayo watu katika kutaka watimiziwe haki
zao katika vipimo na mizani, na ikaonya mtindo kama huo kwa kuwa ipo Siku ya
Hisabu, na ikathibitisha kuwa vitendo vyao vimedhibitiwa katika daftari la
hisabu, ambalo halimkadhibishi ila mwenye kupindukia mipaka, mwenye dhambi
aliye zuiliwa na rehema za Mola wake Mlezi, na mwisho wake ni Jahannamu.
Tena Aya zikawageukia watu wema, zikawatuza nyoyo kwa vitendo vyao, na zikataja
neema zao na alama zao, zikiashiria namna moja wapo katika neema hizo, na kwa
ajili ya hizo washindanie wanao shindana. Na Aya zikaeleza walio kuwa
wakiyafanya makafiri wakosefu kuwafanyia Waumini wanapo waona, au wanapo kuwa
Waumini wanapita mbele yao. Na Sura ikakhitimisha kwa kuwatuliza Waumini kwamba
Siku ya Kiyama itawafanyia insafu, wao watakuwa katika neema wakiwacheka
makafiri, nao wamekaa juu ya makochi wakiwaangalia, na makafiri watalipwa kwa
waliyo kuwa wakiyatenda.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Ole wao
hao wapunjao!
2. Ambao
wanapo jipimia kwa watu hudai watimiziwe.
3. Na wao
wanapo wapimia watu kwa kipimo au mizani hupunguza.
4. Kwani
hawadhani hao kwamba watafufuliwa
5. Katika Siku
iliyo kuu,
6. Siku watapo
msimamia watu Mola Mlezi wa walimwengu wote?
7. Hasha!
Hakika maandiko ya wakosefu bila ya shaka yamo katika Sijjin.
8. Unajua nini Sijjin?
9. Kitabu
kilicho andikwa.
10. Ole
wao siku hiyo kwa wanao kadhibisha!
11. Ambao
wanaikadhibisha Siku ya Malipo.
12. Wala
haikadhibishi ila kila mwenye kuruka mipaka, mwenye dhambi.
13. Anapo
somewa Aya zetu husema: Ni visa vya watu wa kale!
14. Hasha!
Bali yametia kutu juu ya nyoyo zao hao walio kuwa wakiyachuma.
15. Hasha!
Hakika hao siku hiyo bila ya shaka watazuiliwa na neema za Mola wao Mlezi.
16. Kisha
wataingia Motoni!
17. Kisha
waambiwe: Haya ndiyo mliyo kuwa mkiyakadhabisha.
18. Hasha!
Hakika maandiko ya watu wema bila ya shaka yamo katika I'liyyin.
19. Na
nini kitakacho kujuvya nini I'liyyin?
20. Kitabu
kilicho andikwa.
21.
Wanakishuhudia walio karibishwa.
22. Hakika
watu wema bila ya shaka watakuwa katika neema.
23. Wakae
juu ya viti vya enzi wakiangalia.
24.
Utatambua katika nyuso zao mng'aro wa neema,
25.
Watanyweshwa kinywaji safi kiliyo tiwa muhuri,
26. Muhuri
wake ni miski. Na katika hayo washindanie wenye kushindana.
27. Na mchanganyiko
wake ni Tasniim,
28.
Chemchem watakayo inywa walio kurubishwa.
29. Kwa
hakika wale walio kuwa wakosefu walikuwa wakiwacheka walio amini.
30. Na
wanapo pita karibu yao wakikonyezana.
31. Na
wanapo rudi kwa watu wao hurudi nao wamefurahi.
32. Na
wanapo waona husema: Hakika hawa ndio khasa walio potea.
33. Na wao
hawakutumwa wawe walinzi juu yao.
34. Basi leo walio amini ndio watawacheka makafiri,
35. Nao wako juu ya viti vya enzi wakiangalia.
36. Je! makafiri wamelipwa malipo ya yale waliyo kuwa
wakiyatenda?
|