86. SURAT ATT'AARIQ
(Imeteremka
Makka)
Sura hii imeanzia kwa kiapo
cha kuashiria dalili za kudra ya Mwenyezi Mungu, na inatilia mkazo kuwa kila
nafsi ina mlinzi wake na muangalizi, na inamtaka mtu ajifikirie kuumbwa kwake,
na ya kwamba yeye kaumbwa na maji yenye kutoka kwa kasi, ili ipatikane hoja
kwamba Mwenye kuumba hivi ni Mweza wa kumrejeza tena baada ya kufa kwake.Tena ikaapa
mara ya pili kwamba Qur'ani ni kauli ya kufafanua wala si maneno ya maskhara.
Na juu ya kuwa hivyo makafiri bila ya shaka wameshughulika kuikanya na
kuipangia njama. Na Mwenyezi Mungu amezirudi njama zao kwa njama kali kuliko
zao. Kisha Sura imekhitimisha kwa kutaka wapewe muhula makafiri.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Naapa kwa mbingu na Kinacho kuja usiku!
2. Na nini kitakacho kujuulisha ni nini hicho Kinacho kuja
usiku?
3. Ni Nyota yenye mwanga mkali.
4. Hapana nafsi ila inayo mwangalizi.
5. Hebu naajitazame mwanaadamu ameumbwa kwa kitu gani?
6. Ameumbwa kwa maji yatokayo kwa kuchupa,
7. Yatokayo baina ya mifupa ya mgongo na mbavu.
8. Hakika Yeye ana uweza wa kumrudisha.
9. Siku zitakapo dhihirishwa siri.
10. Basi hatakuwa na nguvu wala msaidizi.
11. Naapa kwa mbingu yenye marejeo!
12. Na kwa ardhi inayo pasuka!
13. Hakika hii ni kauli ya kupambanua.
14. Wala si mzaha.
15. Hakika
wao wanapanga mpango.
16. Na Mimi napanga mpango.
17. Basi wape muhula makafiri - wape muhula pole pole.
|