88. SURAT AL-GHAASHIYAH
(Imeteremka
Makka)
Imeanza Sura hii kwa njia
ya kutia shauku kuisikiliza hadithi ya Siku ya Kiyama, na hayo mambo yatakayo
tokea humo. Inaashiria kwamba watu ni makundi mawili: miongoni mwao wapo ambao
hawatapata hishima yoyote kwa watakavyo pokewa na wataingia kwenye Moto mkali.
Na wapo watakao ifikia siku hiyo kwa furaha kwa namna ya rehema na radhi zilizo
andaliwa kwa ajili yao. Kisha Sura ikaeleza dalili zilizo wazi za uweza wa
Mwenyezi Mungu Mtukufu kufufua kutokana na wanavyo ona wenyewe kwa macho yao na
wanayo nafiika kwayo katika uhai wao. Na baada ya kuzitaja dalili hizi
ikageukia khabari za Mtume s.a.w. kwa kukumbusha kwamba waajibu wake mkubwa kwa
mintarafu yao ni wazi, ya kwamba yeye hakutawalishwa juu yao awalazimishe
kuamini, na kwamba mwenye kugeuka na akakufuru baada ya waadhi huu ni Mwenyezi
Mungu ndiye atakaye mshika kwa dhambi zake, na atamuadhibu kwa adhabu kubwa
kabisa, atapo rejea kwake baada ya kufa, kwani marejeo ya wote na kuhisabiwa
kwao wote ni kwake Yeye Mwenyezi Mungu.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Je! Imekufikia khabari ya msiba wa kufudikiza?
2. Siku hiyo nyuso zitainama,
3. Zikifanya kazi, nazo taabani.
4. Ziingie
katika Moto unao waka -
5. Zikinyweshwa
kutoka chemchem inayo chemka.
6. Hawatakuwa na
chakula isipo kuwa kichungu chenye miba.
7. Hakinenepeshi
wala hakiondoi njaa.
8. Siku hiyo
nyuso nyengine zitakuwa kunjufu.
9. Zitakuwa
radhi kwa juhudi yao,
10. Katika
Bustani ya juu.
11. Hawatasikia
humo upuuzi.
12. Humo
imo chemchem inayo miminika.
13. Humo vimo viti vilivyo nyanyuliwa,
14. Na bilauri zilizo pangwa,
15. Na matakia safu safu,
16. Na mazulia yaliyo tandikwa.
17. Je! Hawamtazami ngamia jinsi alivyo umbwa?
18. Na mbingu jinsi ilivyo inuliwa?
19. Na milima jinsi ilivyo thibitishwa?
20. Na ardhi jinsi ilivyo tandazwa?
21. Basi kumbusha! Hakika wewe ni Mkumbushaji.
22. Wewe si mwenye kuwatawalia.
23. Lakini anaye rudi nyuma na kukataa,
24. Basi Mwenyezi Mungu atamuadhibu kwa adhabu iliyo kubwa
kabisa!
25. Hakika ni kwetu Sisi ndio marejeo yao.
26. Kisha hakika ni juu yetu Sisi hisabu yao!
|