89. SURAT AL-FAJR
(Imeteremka
Makka)
Imeanza Sura hii kwa viapo
vya mambo yanayo onekana namna mbali mbali, yanayo pelekea kuangalia athari ya
kudra kwamba wanao mkanya Mwenyezi Mungu na kukanya kufufuliwa watakuja
adhibiwa, kama walivyo kwisha adhibiwa walio kadhibisha kabla yao. Na Sura
ikaingia kuthibitisha mwendo wa Mwenyezi Mungu wa kuwajaribu waja wake kwa
kheri na shari, na kwamba kupa kwake na kunyima kwake sio dalili ya kuridhika
kwake au kukasirika kwake. Tena mazungumzo yakawaelekea wanao semezwa ya kwamba
hali zao zinafichua wingi wa pupa yao na choyo chao. Kisha inakhitimisha kwa
kuashiria majuto ya wanao pindukia kiasi na kutamani kwao kwamba laiti wangeli
tanguliza mema ya kuwaokoa na hayo wanayo teseka nayo ya vitisho vya Siku ya
Kiyama, na yanayo kuwa ya kuiliwaza nafsi iliyo tua iliyo tanguliza mema wala
isikiuke mipaka, na itavyo itwa iingie pamoja na walio kirimiwa miongoni mwa
waja wa Mwenyezi Mungu katika Pepo ya Mwenyezi Mungu.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Naapa kwa alfajiri,
2. Na kwa masiku kumi,
3. Na kwa viwili viwili na kimoja kimoja,
4. Na kwa usiku unapo pita,
5. Je! Hapana katika haya kiapo kwa mwenye akili?
6. Kwani hukuona jinsi Mola wako Mlezi alivyo wafanya kina
A'di?
7. Wa
Iram, wenye majumba marefu?
8. Ambao
haukuumbwa mfano wake katika nchi?
9. Na Thamudi walio chonga majabali huko bondeni?
10. Na Firauni mwenye vigingi?
11. Ambao walifanya jeuri katika nchi?
12. Wakakithirisha
humo ufisadi?
13. Basi
Mola wako Mlezi aliwapiga mjeledi wa adhabu.
14. Hakika
Mola wako Mlezi yupo kwenye mavizio anawavizia.
15. Ama
mtu anapo jaribiwa na Mola wake Mlezi, akamkirimu na akamneemesha, husema: Mola
wangu Mlezi amenikirimu!
16. Na ama
anapo mjaribu akampunguzia riziki yake, husema: Mola wangu Mlezi amenitia
unyonge!
17. Sivyo
hivyo! Bali nyinyi hamuwakirimu mayatima,
18. Wala
hamhimizani kulisha masikini;
19. Na
mnakula urithi kwa ulaji wa pupa,
20. Na mnapenda mali pendo la kupita kiasi.
21. Sivyo
hivyo! Itakapo vunjwa ardhi vipande vipande,
22. Na akaja Mola wako Mlezi na Malaika safu safu,
23. Na ikaletwa Jahannamu siku hiyo, siku hiyo mtu atakumbuka!
Lakini kukumbuka huko kutamfaa nini?
24. Atasema: Laiti ningeli jitangulizia kwa uhai wangu!
25. Basi siku hiyo hataadhibu yeyote namna ya kuadhibu
kwake.
26. Wala hatafunga yeyote kama kufunga kwake.
27. Ewe nafsi iliyo tua!
28. Rejea kwa Mola wako Mlezi umeridhika, na umemridhisha.
29. Basi ingia miongoni mwa waja wangu,
30. Na ingia katika Pepo yangu.
|