101. AL-QAARIA'H
(Imeteremka
Makka)
Sura hii inaanza kwa kitisho
cha hiyo AL-QAARIA'H, yaani Inayo gonga, sauti inayo gonga katika masikio ya
watu, yaani ndio Kiyama. Na Sura imetaja baadhi ya hali za hiyo sauti inayo
gonga khasa kwa mintarafu ya watu na milima. Na ikashughulikia kusimulia hao
ambao mizani yao itakuwa nzito kwa kuzidi mema yao, na mizani yao itayo kuwa
duni kwa kuzidi maovu yao (na kupunguka mema yao).
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Inayo gonga!
2. Nini Inayo gonga?
3. Na nini kitacho kujuilisha nini Inayo gonga?
4. Siku ambayo watu watakuwa kama nondo walio tawanyika;
5. Na milima itakuwa kama sufi zilizo chambuliwa!
6. Basi yule ambaye mizani yake itakuwa nzito,
7. Huyo atakuwa katika maisha ya kupendeza.
8. Na yule ambaye mizani yake itakuwa khafifu,
9. Huyo maskani yake yatakuwa Moto wa Hawiya!
10. Na nini kitacho kujuilisha nini hiyo?
11. Ni Moto mkali!
|