201 - 250
201. Na katika wao wapo wanao sema: Mola wetu Mlezi, tupe
duniani mema, na Akhera mema, na utulinde na adhabu ya Moto!
202. Hao ndio watakao pata sehemu yao kwa sababu ya yale
waliyo yachuma. Na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.
203. Na mtajeni Mwenyezi Mungu katika zile siku zinazo
hisabiwa. Lakini mwenye kufanya haraka katika siku mbili (akarejea) si dhambi
juu yake; na mwenye kukawia pia si dhambi juu yake, kwa mwenye kumchamngu. Na
mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba nyinyi mtakusanywa kwake.
204. Na katika watu yupo yule ambaye maneno yake kwa maisha
ya kidunia hukufurahisha; naye humshuhudisha Mwenyezi Mungu kwa yaliyomo moyoni
mwake, na hali yeye ndiye mkubwa wa ukhasimu.
205. Na anapo tawala hufanya juhudi katika nchi kwa
kufisidi humo na kuteketeza mimea na viumbe. Na Mwenyezi Mungu hapendi ufisadi.
206. Na akiambiwa: Mwogope Mwenyezi Mungu, hupandwa na mori
wa kutenda madhambi. Basi huyo inamtosha Jahannam. Paovu mno hapo kwa
mapumziko.
207. Na katika watu yupo ambaye huiuza nafsi yake kwa
kutaka radhi za Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake.
208. Enyi mlio amini! Ingieni katika Uislamu kwa ukamilifu,
wala msifuate nyayo za She'tani; hakika yeye kwenu ni adui aliye wazi.
209. Na ikiwa mkateleza baada ya kukufikieni hoja zilizo
wazi, basi jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
210. Je wanangoja mpaka Mwenyezi Mungu awajie katika vivuli
vya mawingu pamoja na Malaika, na hukumu iwe imekwisha tolewa? Na kwa Mwenyezi
Mungu ndio hurejeshwa mashauri yote.
211. Waulize Wana wa Israili: Tumewapa ishara ngapi zilizo wazi?
Na anaye zibadili neema za Mwenyezi Mungu baada ya kumfikia basi hakika
Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.
212. Walio kufuru wamepambiwa maisha ya duniani; na
wanawafanyia maskhara walio amini. Na wenye kuchamngu watakuwa juu yao Siku ya
Kiyama. Na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu.
213. Watu wote walikuwa ni umma mmoja. Mwenyezi Mungu
akapeleka Manabii wabashiri na waonyaji. Na pamoja nao akateremsha Kitabu kwa
Haki, ili kihukumu baina ya watu katika yale walio khitalifiana. Na wala
hawakukhitalifiana ila wale walio pewa Kitabu hicho baada ya kuwafikia hoja
zilizo wazi, kwa sababu ya uhasidi baina yao. Ndipo Mwenyezi Mungu kwa idhini
yake akawaongoa walio amini kwendea haki katika mambo waliyo khitalifiana. Na
Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye kwenye Njia Iliyo Nyooka.
214. Mnadhani kuwa mtaingia Peponi, bila ya kukujieni kama
yaliyo wajia wale walio pita kabla yenu? Iliwapata shida na madhara na
wakatikiswa hata Mtume na walio amini pamoja naye wakasema: Lini nusura ya
Mwenyezi Mungu itakuja? Jueni kuwa nusura ya Mwenyezi Mungu ipo karibu.
215.
Wanakuuliza watoe nini? Sema: Kheri mnayo itoa ni kwa ajili ya wazazi na jamaa
na mayatima na masikini na wasafiri. Na kheri yoyote mnayo ifanya Mwenyezi
Mungu anaijua.
216.
Mmeandikiwa kupigana vita, navyo vinachusha kwenu. Lakini huenda mkachukia kitu
nacho ni kheri kwenu. Na huenda mkapenda kitu nacho ni shari kwenu. Na Mwenyezi
Mungu anajua na nyinyi hamjui.
217. Wanakuuliza
juu ya kupigana vita katika mwezi mtakatifu. Sema: Kupigana vita wakati
huo ni dhambi kubwa. Lakini kuzuilia watu wasende katika Njia ya Mwenyezi Mungu
na kumkanusha Yeye, na kuzuilia watu wasende kwenye Msikiti Mtakatifu na
kuwatoa watu wake humo, ni makubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na fitina ni
mbaya zaidi kuliko kuuwa. Wala hawatoacha kupigana nanyi mpaka wakutoeni katika
Dini yenu kama wakiweza. Na yeyote katika nyinyi akiacha Dini yake akafa naye
ni kafiri, basi hao ndio ambao a'mali zao zimeharibika duniani na Akhera. Na
hao ndio watu wa Motoni; humo watadumu.
218. Hakika wale walio amini na wale walio hama na
wakapigania Njia ya Mwenyezi Mungu, hao ndio wanao taraji rehema za Mwenyezi
Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.
219. Wanakuuliza juu ya ulevi na kamari. Sema: Katika hivyo
zipo dhambi kubwa na manufaa kwa watu. Lakini dhambi zake ni kubwa zaidi kuliko
manufaa yake. Na wanakuuliza
watoe nini? Sema: Kilicho chepesi. Namna hivi Mwenyezi Mungu
anakubainishieni Aya zake mpate kufikiri--
220.--katika mambo ya dunia na mambo ya Akhera. Na
wanakuuliza juu ya mayatima. Sema: Kuwatengenezea ndio kheri. Na mkichanganyika
nao basi ni ndugu zenu; na Mwenyezi Mungu anamjua mharibifu na mtengenezaji. Na Mwenyezi Mungu angeli penda angeli
kutieni katika udhia. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
221. Wala
msiwaoe wanawake washirikina mpaka waamini. Na mjakazi Muumini ni bora kuliko
mshirikina hata akikupendezeni. Wala msiwaoze (binti zenu) wanaume washirikina
mpaka waamini. Na mtumwa mwanamume Muumini ni bora kuliko mshirikina hata
akikupendezeni. Hao wanaitia kwenye Moto, na Mwenyezi Mungu anaitia kwenye Pepo
na maghafira kwa idhini yake. Naye huzibainisha Aya zake kwa watu ili wapate
kukumbuka.
222. Na
wanakuuliza juu ya hedhi. Waambie,
huo ni uchafu. Basi jitengeni
na wanawake wakati wa hedhi. Wala msiwaingilie mpaka wat'ahirike. Wakisha
t'ahirika basi waendeeni alivyo kuamrisheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu
huwapenda wanao tubu na huwapenda wanao jisafisha.
223. Wake zenu
ni kama konde zenu. Basi ziendeeni konde zenu mpendavyo. Lakini jitangulizieni
kheri nafsi zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kuwa hakika nyinyi
mtakutana naye. Na wape bishara njema Waumini.
224. Wala
msifanye jina la Mwenyezi Mungu katika viapo vyenu kuwa ni kisingizio cha
kuacha kufanya wema na kuchamngu na kupatanisha baina ya watu. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kusikia na Mwenye kujua.
225. Mwenyezi
Mungu hakushikeni kwa viapo vyenu vya upuuzi. Bali anakushikeni kwa yanayo
chuma nyoyo zenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mpole.
226. Kwa wanao
apa kuwa watajitenga na wake zao, wangojee miezi mine. Wakirejea basi Mwenyezi
Mungu hakika ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.
227. Na
wakiazimia kuwapa talaka basi, Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na Mjuzi.
228. Na wanawake
walio achwa wangoje peke yao mpaka t'ahara (au hedhi) tatu zipite. Wala
haiwajuzii kuficha alicho umba Mwenyezi Mungu katika matumbo yao, ikiwa
wanamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na waume wao wana haki ya
kuwarejesha katika muda huo, kama wakitaka kufanya sulhu. Nao wanawake wanayo
haki kwa Sharia kama ile haki iliyo juu yao. Na wanaume wana daraja zaidi
kuliko wao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
229.T'alaka ni mara mbili. Kisha ni kukaa kwa wema au
kuachana kwa vizuri. Wala si halali kwenu kuchukua chochote mlicho wapa wake
zenu, ila ikiwa wote wawili wakiogopa ya kwamba hawataweza kushikamana na
mipaka ya Mwenyezi Mungu. Basi mkiogopa kuwa hawataweza kushikamana na mipaka
ya Mwenyezi Mungu hapo itakuwa hapana lawama ikiwa mwanamke atajikomboa. Hii
ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu; basi msiikiuke. Na watakao ikiuka mipaka ya
Mwenyezi Mungu, hao ndio madhaalimu.
230. Na kama amempa t'alaka (ya tatu) basi si halali kwake
baada ya hayo mpaka aolewe na mume mwengine. Na akiachwa basi hapana ubaya kwao
kurejeana wakiona kuwa watashikamana na mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na hii ni
mipaka ya Mwenyezi Mungu anayo ibainisha kwa watu wanao jua.
231. Na mtakapo wapa wanawake t'alaka, nao wakafikia
kumaliza eda yao, basi warejeeni kwa wema au waachilieni kwa wema. Wala
msiwarejee kwa kuwadhuru mkafanya uadui. Na atakaye fanya hivyo, amejidhulumu
nafsi yake. Wala msizichukulie Aya za Mwenyezi Mungu kwa maskhara. Na kumbukeni
neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu, na aliyo kuteremshieni katika Kitabu na
hikima anacho kuonyeni kwacho. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba hakika
Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
232. Na mtakapo wapa wanawake t'alaka nao wakamaliza eda
yao, basi msiwazuie kuolewa na waume zao endapo baina yao wamepatana kwa wema.
Hayo anaonywa nayo yule miongoni mwenu anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya
Mwisho. Hayo ni bora zaidi kwenu na safi kabisa. Na Mwenyezi Mungu anajua,
lakini nyinyi hamjui.
233. Na wazazi wanawake wawanyonyeshe watoto wao miaka
miwili kaamili kwa anaye taka kutimiza kunyonyesha. Na juu ya baba yake chakula
cha kina mama, na nguo zao kwa mujibu wa ada. Wala halazimishwi mtu ila kwa
kadiri ya uwezo wake. Mama asitiwe taabuni kwa ajili ya mwanawe, wala baba kwa
ajili ya mwanawe. Na juu ya mrithi mfano wa hivyo. Na kama wote wawili wakitaka
kumwachisha ziwa kwa kuridhiana na kushauriana, basi si vibaya kwao. Na mkitaka
kuwapatia watoto wenu mama wa kuwanyonyesha basi hapana ubaya kwenu mkitoa
mlicho ahidi kwa mujibu wa ada. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba
Mwenyezi Mungu anayaona yote mnayo yatenda.
234. Na wale miongoni mwenu wanao kufa na wakaacha wake,
hawa wake wangoje peke yao miezi mine na siku kumi. Na wanapo timiza eda yao
basi hapana ubaya kwao kwa wanao jifanyia kwa mujibu wa ada. Na Mwenyezi Mungu
anazo khabari za yote mnayo yatenda.
235. Wala si vibaya kwenu katika kupeleka posa kwa ishara
tu kwa wanawake waliomo edani au mkadhamiria katika nyoyo zenu. Mwenyezi Mungu
anajua kwamba nyinyi mtawakumbuka. Lakini msiwaahidi kwa siri, ila mnene maneno
mema. Wala msiazimie kufunga ndoa mpaka eda ifike mwisho wake. Na jueni kwamba
Mwenyezi Mungu anajua yaliyomo katika nafsi zenu. Basi tahadharini naye. Na jueni
kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mpole.
236. Hapana ubaya kwenu mkiwapa t'alaka wanawake ambao
hamjawagusa au kuwabainishia mahari yao. Lakini wapeni cha kuwaliwaza, mwenye
wasaa kadiri awezavyo na mwenye dhiki kadiri awezavyo - maliwaza kwa mujibu wa
dasturi kuwa ni haki juu ya watendao mema.
237. Na mkiwapa t'alaka kabla ya kuwagusa, na mmekwisha
wawekea hayo mahari makhsusi, basi wapeni nusu ya mahari mlio agana, isipo kuwa
ikiwa wanawake wenyewe wamesamehe, au mume ambaye kifungo cha ndoa ki mikononi
mwake awe amesamehe. Na kusameheana ndiko kulio karibu zaidi na uchamngu. Wala msisahau fadhila baina yenu. Hakika
Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.
238. Zilindeni
Sala, na khasa Sala ya katikati, na simameni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu nanyi
ni wenye kuqunuti (kunyenyekea).
239. Ikiwa
mnakhofu (Salini) na hali mnakwenda kwa miguu au mmepanda. Na mtakapo kuwa
katika amani, basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu kama alivyo kufunzeni yale mliyo
kuwa hamyajui.
240. Na wale miongoni
mwenu wanao kufa na wakawacha wake, na wausie kwa ajili ya wake zao kupata
matumizi kwa mwaka mmoja bila ya kuwatoa nyumba. Na wanawake wenyewe
wakiondoka, basi hapana ubaya kwenu kwa waliyo jifanyia wenyewe kwa mujibu wa
Sharia. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
241. Na wanawake
walio achwa wapewe cha kuwaliwaza kwa mujibu wa Sharia. Haya ni waajibu kwa
wachamngu.
242. Namna hivi
anakubainishieni Mwenyezi Mungu Aya zake ili mpate kufahamu.
243. Hukuwaona
wale walio toka majumbani kwao kwa maelfu kwa kuogopa mauti? Mwenyezi Mungu
akawaambia: Kufeni! Kisha akwahauisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila
juu ya watu, lakini wengi wa watu hawashukuru.
244. Na piganeni
katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Msikizi na
Mjuzi.
245. Ni nani
atakaye mkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema ili amzidishie mzidisho mwingi, na
Mwenyezi Mungu hukunja na hukunjua. Na Kwake Yeye mtarejea.
246. Hukuwaona
watukufu katika Wana wa Israili baada ya Musa, walipo mwambia Nabii wao:
Tuwekee mfalme ili tupigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu? Akasema: Je,
haielekei ikiwa mtaandikiwa vita kuwa msipigane? Wakasema: Itakuwaje tusipigane
katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na hali tumetolewa majumbani kwetu na watoto
wetu? Lakini walipo andikiwa kupigana waligeuka, isipo kuwa wachache miongoni
mwao. Na Mwenyezi Mungu anawajua madhaalimu.
247, Na
Nabii wao akawaambia: Mwenyezi Mungu amekuteulieni Taluti (Sauli) kuwa ni
mfalme. Wakasema: vipi atakuwa na ufalme juu yetu, na hali sisi tuna haki zaidi
kupata ufalme kuliko yeye, naye hakupewa wasaa wa mali? Akasema: Mwenyezi Mungu
amemteua yeye juu yenu na amemzidishia ukunjufu wa ilimu na kiwiliwili. Na
Mwenyezi Mungu humpa ufalme wake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na
Mjuzi.
248. Na
Nabii wao akawaambia: Alama ya ufalme wake ni kukuleteeni lile sanduku ambalo
mna ndani yake kituliza nyoyo zenu, kitokacho kwa Mola wenu Mlezi, na mna
mabaki ya waliyo yaacha kina Musa na kina Harun, wanalichukua Malaika. Bila
shaka katika hayo zimo dalili kwenu ikiwa nyinyi mnaamini.
249. Basi
Taluti alipo ondoka na majeshi alisema: Mwenyezi Mungu atakujaribuni kwa mto.
Atakaye kunywa humo si pamoja nami, na asiye kunywa atakuwa pamoja nami: ila
atakaye teka kiasi ya kitanga cha mkono wake. Lakini walikunywa humo isipo kuwa
wachache tu miongoni mwao. Alipo vuka mto yeye na wale walio amini pamoja naye,
walisema: Leo hatumwezi Jaluti (Goliati) na majeshi yake. Wakasema wale wenye
yakini ya kukutana na Mwenyezi Mungu: Makundi mangapi madogo yameshinda makundi
makubwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye
kusubiri.
250, Na
walipo toka kupambana na Jaluti na majeshi yake walisema: Mola wetu Mlezi!
Tumiminie subira, na isimamishe imara miguu yetu, na utusaidie tuwashinde watu
Makafiri--
|