251 - 286
251.--Kwa idhini ya Mwenyezi Mungu waliwatimua, na Daudi
akamuuwa Jaluti, na Mwenyezi Mungu akampa Daudi ufalme na hikima, na
akamfundisha aliyo yapenda. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hawapambanishi watu kwa
watu basi dunia ingeli haribika. Lakini Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya
walimwengu wote.
252. Hizi ni Aya za Mwenyezi Mungu tunakusomea kwa haki. Na
hakika wewe ni miongoni mwa Mitume.
253. MITUME hao tumewatukuza baadhi yao juu ya wengineo.
Katika wao wapo ambao Mwenyezi Mungu alisema nao, na wengine akawapandisha
vyeo. Na tukampa Isa mwana wa Mariyam hoja zilizo wazi, na tukamtia nguvu kwa
Roho Takatifu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli pigana walio kuwa
baada yao baada ya kuwajia hoja zilizo wazi. Lakini walikhitalifiana. Basi wapo
kati yao walio amini, na wengine kati yao walio kufuru. Na lau kuwa Mwenyezi
Mungu alipenda wasingeli pigana. Lakini Mwenyezi Mungu hutenda atakavyo.
254. Enyi mlio amini! Toeni katika tulivyo kupeni kabla
haijafika Siku ambayo hapatakuwapo biashara, wala urafiki, wala uombezi. Na
makafiri ndio madhaalimu.
255. Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye Aliye hai,
Msimamia mambo yote milele. Hashikwi na usingizi wala kulala. Ni vyake pekee
vyote viliomo mbinguni na duniani. Ni nani huyo awezaye kuombea mbele yake bila
ya idhini yake? Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao; wala wao hawajui
chochote katika vilio katika ujuzi wake, ila kwa atakalo mwenyewe. Enzi yake
imetanda mbinguni na duniani; na wala haemewi na kuvilinda hivyo. Na Yeye ndiye
aliye juu, na ndiye Mkuu.
256. Hapana
kulazimisha katika Dini. Kwani Uwongofu umekwisha pambanuka na upotofu. Basi
anaye mkataa Shet'ani na akamuamini Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata
kishikio madhubuti, kisicho vunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia,
Mwenye kujua.
257. Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wa walio amini. Huwatoa
gizani na kuwaingiza mwangazani. Lakini walio kufuru, walinzi wao ni
Mashet'ani. Huwatoa kwenye mwangaza na kuwaingiza gizani. Hao ndio watu wa
Motoni, na humo watadumu.
258. Hukumwona yule aliye hojiana na Ibrahim juu ya Mola
wake Mlezi kwa sababu Mwenyezi Mungu alimpa ufalme? Ibrahim alipo sema: Mola
wangu ni yule ambaye huhuisha na kufisha. Yeye akasema: Mimi pia nahuisha na
kufisha. Ibrahim akasema: Mwenyezi Mungu hulichomozesha jua mashariki, basi
wewe lichomozeshe magharibi. Akafedheheka yule aliye kufuru; na Mwenyezi Mungu
hawaongoi watu madhaalimu.
259. Au kama yule aliye pita karibu na mji ulio kwisha kuwa
magofu tu, akasema: Ataufufuaje Mwenyezi Mungu mji huu baada ya kufa kwake?
Basi Mwenyezi Mungu alimfisha yeye muda wa miaka mia. Kisha akamfufua.
Akamuuliza: Je umekaa muda gani? Akajibu: Labda nimekaa siku moja au sehemu ya
siku. Akamwambia: Bali umekaa miaka mia wewe. Hebu angalia chakula chako na
vinywaji vyako, havikuharibika. Na muangalie punda wako. Na ili tukufanye uwe
ni Ishara kwa watu iangalie hii mifupa yake jinsi tunavyo inyanyua kisha
tunaivisha nyama. Basi yalipo mbainikia alinena: Najua kwamba Mwenyezi Mungu ni
Mwenye uweza juu ya kila kitu.
260. Na alipo sema Ibrahim: Mola wangu Mlezi! Nionyeshe
vipi unavyo fufua wafu. Mwenyezi Mungu akasema: Kwani huamini? Akasema: Hasha!
Lakini ili moyo wangu utue. Akamwambia: Twaa ndege wane na uwazoeshe kwako,
kisha uweke juu ya kila kilima sehemu, kisha wete, watakujia mbio. Na ujue
kwamba hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu, na Mwenye hikima.
261. Mfano wa wanao tumia mali zao katika Njia ya Mwenyezi
Mungu ni kama mfano wa punje moja iliyo chipuza mashuke saba. Katika kila shuke zimo punje mia. Na Mwenyezi
Mungu humzidishia amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mwenye kujua.
262. Wanao toa
mali zao kwa Njia ya Mwenyezi Mungu, kisha hawafuatishii masimbulizi wala udhia
kwa walicho toa, wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi, wala haitakuwa khofu juu
yao wala hawatahuzunika.
263. Kauli njema
na usamehevu ni bora kuliko sadaka inayo fuatiliwa na maudhi. Na Mwenyezi Mungu
ndiye Mwenye kujitosha na Mpole.
264. Enyi mlio amini! Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi
na maudhi, kama anaye toa mali yake kwa kuwaonyesha watu, wala hamuamini
Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho. Basi mfano wake ni kama mfano wa jabali
ambalo juu yake pana udongo, kisha likapigwa na mvua kubwa, ikaliacha tupu.
Basi hawatakuwa na uweza wowote kwa walivyo chuma. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi
watu makafiri.
265. Na mfano wa wale wanao toa mali zao kwa kuitafuta
radhi ya Mwenyezi Mungu na kuzipa nguvu roho zao ni kama mfano wa bustani iliyo
mahali pa juu, ikaifikia mvua kubwa na ikaleta mazao yake mardufu; na hata kama
haifikiwi na mvua kubwa basi manyunyu hutosha. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo
yatenda.
266. Je! Yupo mmoja wenu anaye penda kuwa na kitalu cha
mitende na mizabibu ipitayo mito kati yake, naye humo hupata mazao ya kila namna,
na uzee ukamfikia naye hali ana watoto wanyonge, kikapigwa na kimbunga chenye
moto, kikaungua? Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kubainishieni Ishara ili
mpate kufikiri.
267. Enyi mlio amini! Toeni katika vile vizuri mlivyo
vichuma, na katika vile tulivyo kutoleeni katika ardhi. Wala msikusudie kutoa
vilivyo vibaya, hali nyinyi wenyewe msinge vipokea ila ingekuwa mmefumba macho.
Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha na Msifiwa.
268. Shet'ani anakutieni khofu ya ufakiri na anakuamrisheni
mambo machafu. Na Mwenyezi Mungu anakuahidini msamaha na fadhila zitokazo
kwake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua.
269. Yeye humpa hikima amtakaye; na aliye pewa hikima bila
ya shaka amepewa kheri nyingi. Na hawakumbuki ila wenye akili.
270. Na chochote mnacho toa au nadhiri mnazo weka basi
hakika Mwenyezi Mungu anajua. Na walio dhulumu hawana wa kuwanusuru.
271. Mkizidhihirisha sadaka ni vizuri; na mkizificha
mkawapa mafakiri kwa siri basi hivyo ni kheri kwenu, na yatakuondoleeni baadhi
ya maovu yenu. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
272. Si juu yako wewe kuwaongoa, lakini Mwenyezi Mungu
humwongoa amtakaye. Na kheri yoyote mnayo toa ni kwa nafsi zenu. Wala msitoe
ila kwa kutafuta wajihi wa Mwenyezi Mungu. Na kheri yoyote mtakayo toa mtalipwa
kwa ukamilifu, wala hamtadhulumiwa.
273. Nawapewe mafakiri walio zuilika katika njia za
Mwenyezi Mungu, wasio weza kusafiri katika nchi kutafuta riziki. Asiye wajua
hali zao huwadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujizuia kwao. Utawatambua
kwa alama zao; hawang'ang'analii watu kwa kuwaomba. Na kheri yoyote mnayo toa,
basi kwa yakini Mwenyezi Mungu anaijua.
274. Wale wanao toa mali zao usiku na mchana, kwa siri na
dhaahiri, wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi; wala haitakuwa khofu juu yao, wala
hawatahuzunika.
275. Wale walao riba hawasimami ila kama anavyo simama
aliye zugwa na Shet'ani kwa kumgusa. Hayo ni kwa kuwa wamesema: Biashara ni
kama riba. Lakini Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara na ameiharimisha riba.
Basi aliye fikiwa na mawaidha kutoka kwa Mola wake Mlezi, kisha akajizuia, basi
yake ni yaliyo kwisha pita, na mambo yake yako kwa Mwenyezi Mungu. Na wenye
kurudia basi hao ndio watu wa Motoni, humo watadumu.
276. Mwenyezi Mungu huiondolea baraka riba, na huzibariki
sadaka. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila mwenye kukanya na afanyae dhambi.
277. Hakika wale walio amini na wakatenda mema na wakashika
Sala na wakatoa Zaka, wao watapata ujira wao kwa Mola wao Mlezi, wala haitakuwa
khofu juu yao, wala hawatahuzunika.
278. Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na acheni riba
zilizo bakia, ikiwa nyinyi ni Waumini.
279. Basi mkitofanya jitangazieni vita na Mwenyezi Mungu na
Mtume wake. Na mkitubu, basi haki yenu ni rasilmali zenu. Msidhulumu wala
msidhulumiwe.
280. Na akiwa (mdaiwa) ana shida, basi (mdai) angoje mpaka
afarijike. Na mkiifanya deni kuwa ni sadaka, basi ni bora kwenu, ikiwa mnajua.
281. Na iogopeni Siku ambayo mtarudishwa kwa Mwenyezi
Mungu, kisha kila nafsi italipwa ilicho chuma. Nao hawatadhulumiwa.
282. Enyi mlio amini! Mnapo kopeshana deni kwa muda ulio
wekwa, basi andikeni. Na mwandishi aandike baina yenu kwa uadilifu, wala
mwandishi asikatae kuandika. Aandike kama alivyo mfunza Mwenyezi Mungu. Na mwenye
deni juu yake aandikishe; naye amche Mwenyezi Mungu, Mola wake Mlezi. Wala
asipunguze chochote ndani yake. Na akiwa mwenye kudaiwa ni mtu aliye pumbaa au
mnyonge au hawezi kuandikisha mwenyewe, basi aandikishe mlinzi wake kwa
uadilifu. Na mshuhudishe mashahidi wawili katika wanaume wenu. Ikiwa hapana
wanaume wawili, basi mwanamume mmoja na wanawake wawili katika mnao waridhia
kuwa mashahidi. Ili ikiwa mmoja wao akipotea, mmoja wao amkumbushe mwengine. Na
mashahidi wasikatae waitwapo. Wala msipuuze kuliandika deni likiwa dogo au
kubwa mpaka muda wake. Hayo ndiyo haki zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu, na ndiyo
sawa zaidi kwa ushahidi, na vyema zaidi ili msiwe na shaka. Ila ikiwa ni
biashara ya mkono-kwa-mkono baina yenu, basi hapo si vibaya kwenu msipo iandika.
Lakini mnapo uziana wekeni mashahidi. Wala asitiwe matatani mwandishi wala
shahidi. Na mkifanya hivyo basi hakika hilo ni kosa kwenu. Na mcheni Mwenyezi
Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
283. Na mkiwa safarini na hamkupata mwandishi, yatosha
kukabidhiwa rahani. Na mmoja wenu akimwekea amana mwenziwe basi aliye aminiwa
airudishe amana ya mwenzake, na amche Mwenyezi Mungu, Mola wake Mlezi. Wala
msifiche ushahidi. Na atakaye ficha basi hakika moyo wake ni wenye kutenda
dhambi. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mnayo yatenda.
284. Viliomo mbinguni na viliomo duniani ni vya Mwenyezi
Mungu. Na mkidhihirisha yaliyomo katika nafsi zenu au mkayaficha, Mwenyezi
Mungu atakuhisabuni kwayo. Kisha amsamehe amtakaye na amuadhibu amtakaye. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
285. Mtume ameamini yaliyo teremshwa kwake kutoka kwa Mola
Mlezi wake, na Waumini vile vile. Wote wamemuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika
wake, na Vitabu vyake na Mitume wake. Hatutafautishi baina ya yeyote katika
Mitume wake, na (Waumini) husema: Tumesikia na tumet'ii. Tunakutaka maghfira
Mola Mlezi wetu! Na marejeo ni kwako.
286. Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa
kadiri ya iwezavyho. Faida ya iliyo yachuma ni yake, na khasara ya iliyo
yachuma ni juu yake pia. (Ombeni:)Mola wetu Mlezi! Usituchukulie tukisahau au tukikosea. Mola
wetu Mlezi! Usitubebeshe mzigo kama ulio wabebesha wale walio kuwa kabla yetu.
Mola wetu Mlezi Usitutwike tusiyo yaweza, na utusamehe, na utughufirie, na
uturehemu. Wewe ndiye Mlinzi wetu. Basi tupe ushindi tuwashinde kaumu ya
makafiri.
|