51 - 100
51. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi na ni Mola
wenu Mlezi. Basi muabudni Yeye. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.
52. Isa alipo hisi kuwa kati yao pana ukafiri alisema: Nani
wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu? Wanafunzi wake wakasema: Sisi ni wasaidizi
wa Mwenyezi Mungu. Tumemuamini Mwenyezi Mungu, na shuhudia kwamba sisi hakika
ni Waislamu.
53. Mola wetu Mlezi! Tumeyaamini uliyo yateremsha, na
tumemfuata huyu Mtume, basi tuandike pamoja na wanao shuhudia.
54. Na Makafiri walipanga mipango na Mwenyezi Mungu
akapanga mipango, na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa wenye kupanga.
55. Pale Mwenyezi Mungu alipo sema: Ewe Isa! Mimi
nitakufisha, na nitakunyanyua kwangu, na nitakutakasa na wale walio kufuru, na
nitawaweka wale walio kufuata juu ya wale walio kufuru, mpaka Siku ya Kiyama.
Kisha marejeo yenu yatakuwa kwangu, nikuhukumuni katika yale mliyo kuwa
mkikhitalifiana.
56. Ama wale walio kufuru, nitawaadhibu adhabu kali katika
dunia na Akhera, wala hawatapata wa kuwanusuru.
57. Na ama wale walio amini na wakatenda mema basi Mwenyezi
Mungu atawalipa ujira wao kaamili. Na Mwenyezi Mungu hawapendi madhaalimu.
58. Haya tunayo kusomea ni katika Aya na Ukumbusho wenye
hikima.
59. Hakika mfano wa Isa kwa Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa
Adam; alimuumba kwa udongo kisha akamwambia: Kuwa! Basi akawa.
60. Hii ni kweli itokayo kwa Mola wako Mlezi. Basi usiwe
miongoni mwa wanao fanya shaka.
61. Watakao kuhoji katika haya baada ya kukufikilia ilimu hii
waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wake zetu na wake zenu,
na sisi wenyewe na nyinyi wenyewe, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya
Mwenyezi Mungu iwashukie waongo.
62. Hakika haya ndiyo maelezo ya kweli. Na hakuna mungu ila
Mwenyezi Mungu tu, na hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu na Mwenye
hikima.
63. Na kama wakigeuka basi Mwenyezi Mungu anawajua
waharibifu.
64. Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lilio
sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu,
wala tusimshirikishe na chochote; wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa Waola
Walezi badala ya Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka basi semeni: Shuhudi- eni ya
kwamba sisi ni Waislamu.
65. Enyi
Watu wa Kitabu! Mbona mnabishana juu ya Ibrahim, na hali Taurati na Injili
hazikuteremshwa ila baada yake? Basi hamzingatii?
66. Angalieni! Nyinyi mlibishana katika yale mliyo yajua.
Mbona sasa mnabishana katika yale msiyo yajua? Na Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye,
na nyinyi hamjui.
67. Ibrahim hakuwa Yahudi wala Mkristo, lakini alikuwa
mwongofu Muislamu, wala hakuwa katika washirikina.
68. Watu wanao mkaribia zaidi Ibrahim ni wale walio mfuata
yeye na Nabii huyu na walio amini. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wa Waumini.
69. Kipo kikundi katika Watu wa Kitabu wanao penda
kukupotezeni; lakini hawapotezi ila nafsi zao, nao wenyewe hawatambui.
70. Enyi
Watu wa Kitabu! Mbona mnazikataa Ishara za Mwenyezi Mungu ilhali nyinyi
mnashuhudia?
71. Enyi
Watu wa Kitabu! Mbona kweli mnaivisha uwongo, na kweli mnaificha na hali
mnajua?
72. Na
kikundi katika Watu wa Kitabu walisema: Yaaminini yale waliyo teremshiwa wenye
kuamini mwanzo wa mchana, na yakataeni mwisho wake; huenda wakarejea.
73. Wala msimuamini ila anaye fuata dini yenu. Sema: Hakika
uwongofu ni uwongofu wa Mwenyezi Mungu, kuwa apewe mtu mfano wa mlio pewa
nyinyi au wakuhojini mbele ya Mola wenu Mlezi. Sema: Hakika fadhila zimo
mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa
na Mjuzi.
74. Yeye humchagua kumpa rehema zake amtakaye; na Mwenyezi
Mungu ndiye Mwenye fadhila kubwa.
75. Na miongoni mwa Watu wa Kitabu yupo ambaye ukimpa amana
ya mrundi wa mali atakurudishia, na miongoni mwao yupo ambaye ukimpa amana ya
dinari moja hakurudishii isipo kuwa ukimsimamia kumdai. Haya ni kwa kuwa
wakisema: Hatuna lawama kwa ajili ya hawa wasio jua kusoma. Na wanamzulia
uwongo Mwenyezi Mungu, hali nao wanajua.
76. Sivyo hivyo, bali anaye timiza ahadi yake na
akamchamngu basi Mwenyezi Mungu huwapenda wachamngu.
77. Hakika wanao uza ahadi ya Mwenyezi Mungu na viapo vyao
thamani ndogo, hao hawatakuwa na sehemu ya kheri yoyote katika Akhera, wala
Mwenyezi Mungu hatasema nao wala hatawatazama Siku ya Kiyama, wala
hatawatakasa, nao watapata adhabu chungu.
78. Na wapo baadhi yao wanao pindua ndimi zao katika kusoma
Kitabu ili mdhanie kuwa hayo yanatoka Kitabuni, na wala hayatoki Kitabuni. Na
husema: Haya yametoka kwa Mwenyezi Mungu. Na wala hayatoki kwa Mwenyezi Mungu.
Na wanamsingizia Mwenyezi Mungu uwongo na wao wanajua.
79. Haiwezi kuwa mtu aliye pewa na Mwenyezi Mungu Kitabu na
hikima na Unabii kisha awaambie watu: Kuweni wa kuniabudu mimi badala ya
Mwenyezi Mungu. Bali atawaambia: Kuweni wenye kumuabudu Mola Mlezi wa viumbe
vyote, kwa kuwa nyinyi mnafundisha Kitabu na kwa kuwa mnakisoma.
80. Wala hatakuamrisheni kuwafanya Malaika na Manabii kuwa
ni miungu. Je, atakuamrisheni ukafiri baada ya kuwa nyinyi Waislamu?
81. Na pale Mwenyezi Mungu alipo chukua ahadi kwa Manabii:
Nikisha kupeni Kitabu na hikima, kisha akakujieni Mtume mwenye kusadikisha
mliyo nayo, ni juu yenu mumuamini na mumsaidie. Akasema: Je, mmekiri na
mmekubali kushika agizo langu juu ya hayo? Wakasema: Tumekubali. Akasema: Basi
shuhudieni, na Mimi ni pamoja nanyi katika kushuhudia.
82. Watakao geuka baada ya haya basi hao ndio wapotovu.
83. Je, wanataka dini isiyo kuwa ya Mwenyezi Mungu, na hali
kila kilichomo mbinguni na katika ardhi kimesilimu kwa kumt'ii Yeye kikipenda
kisipende, na kwake Yeye watarejeshwa?
84. Sema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu, na tuliyo teremshiwa
sisi, na aliyo teremshiwa Ibrahim, na Ismail, na Is-haak na Yaakub na wajukuu zao,
na aliyo pewa Musa na Isa na Manabii wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi.
Hatubagui baina yao hata mmoja, na sisi ni wenye kusilimu kwake.
85. Na anaye tafuta dini isiyo kuwa Uislamu haitakubaliwa
kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye kukhasiri.
86.Mwenyezi Mungu atawaongoaje watu walio kufuru baada ya
kuamini kwao, na wakashuhudia ya kuwa Mtume huyu ni wa haki, na zikawafikia
hoja zilizo wazi? Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu.
87. Hao malipo yao ni kuwa ipo juu yao laana ya Mwenyezi
Mungu na ya Malaika na ya watu wote.
88. Humo watadumu. Hawatapunguziwa adhabu wala hawatapewa
nafasi.
89. Isipo kuwa wale walio tubu baada ya hayo na
wakatengenea; kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.
90. Hakika wale walio kufuru baada ya kuamini kwao, kisha
wakazidi kukufuru, toba yao haitakubaliwa, na hao ndio walio potea.
91. Hakika wale walio kufuru, na wakafa hali ni makafiri
haitakubaliwa kutoka kwa yeyote wao fidia ya dhahabu ya kujaza dunia nzima lau
wangeli itoa. Hao watapata adhabu chungu, wala hawatakuwa na wa kuwanusuru.
92. KABISA HAMTAFIKIA wema mpaka mtoe katika vile mnavyo
vipenda. Na kitu chochote mnacho kitoa basi hakika Mwenyezi Mungu anakijua.
93. Kila chakula kilikuwa halali kwa Wana wa Israili isipo
kuwa alicho jizuilia Israili mwenyewe kabla haijateremshwa Taurati. Sema:
Leteni Taurati muisome ikiwa nyinyi ni wasema kweli.
94. Na wanao mzulia uwongo Mwenyezi Mungu baada ya hayo,
basi hao ndio madhaalimu.
95. Sema: Mwenyezi Mungu amesema kweli. Basi fuateni mila
ya Ibrahim mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.
96. Hakika Nyumba ya kwanza walio wekewa watu kwa ibada ni
ile iliyoko Bakka, iliyo barikiwa na yenye uwongofu kwa walimwengu wote.
97. Ndani yake zipo Ishara zilizo wazi - masimamio ya
Ibrahim, na mwenye kuingia humo anakuwa katika amani. Na kwa ajili ya Mwenyezi
Mungu imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae njia ya
kwendea. Na atakaye kanusha basi Mwenyezi Mungu si mhitaji kwa walimwengu.
98. Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Kwa nini mnakanusha ishara
za Mwenyezi Mungu, na ilhali kuwa Mwenyezi Mungu ni Shahidi kwa yote mnayo
yatenda?
99. Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Kwa nini mnamzuilia aliye
amini Njia ya Mwenyezi Mungu mkiitafutia kosa, na hali nyinyi mnashuhudia? Na
Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na mnayo yatenda.
100. Enyi mlio amini! Mkiwat'ii baadhi ya walio pewa Kitabu
watakurudisheni kuwa makafiri baada ya Imani yenu.
|