101 - 150
101. Na vipi mkufuru hali nyinyi mnasomewa Aya za Mwenyezi
Mungu na Mtume yuko kati yenu? Na mwenye kushikamana na Mwenyezi Mungu basi
huyo ameongozwa kwenye Njia Iliyo Nyooka.
102. Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu kama ipasavyo
kumcha; wala msife ila nanyi ni Waislamu.
103. Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote
pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu:
vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa
neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto, naye akakuokoeni
nalo. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Ishara zake ili mpate
kuongoka.
104. Na uwe kutokana na nyinyi umma unao lingania kheri na
unao amrisha mema na unakataza maovu. Na hao ndio walio fanikiwa.
105. Wala msiwe kama wale walio farikiana na kukhitalifiana
baada ya kuwafikia hoja zilizo wazi. Na hao ndio watakao kuwa na adhabu kubwa.
106. Siku ambayo nyuso zitanawiri na nyuso zitasawijika.
Ama hao ambao nyuso zao zitasawijika wataambiwa: Je! Mlikufuru baada ya kuamini
kwenu? Basi onjeni adhabu kwa vile mlivyo kuwa mnakufuru.
107. Ama wale ambao nyuso zao zitanawiri watakuwa katika
rehema ya Mwenyezi Mungu. Wao
humo watadumu.
108. Hizi
ni Aya za Mwenyezi Mungu tunakusomea kwa haki. Na Mwenyezi Mungu hataki kuwadhulumu
walimwengu.
109. Na
kila kilichomo mbinguni na kilichomo ardhini ni cha Mwenyezi Mungu; na mambo
yote yatarejea kwa Mwenyezi Mungu.
110.
Nyinyi mmekuwa bora ya umma walio tolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na
mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa Watu wa Kitabu nao
wameamini ingeli kuwa bora kwao. Wapo miongoni mwao waumini, lakini wengi wao
wapotovu.
111. Maadui hawatakudhuruni ila ni maudhi tu. Na wakipigana
nanyi watakupeni mgongo, na tena hawatanusuriwa.
112. Wamepigwa na udhalili popote wanapo kutikana, isipo
kuwa wakishika kamba ya Mwenyezi Mungu na kamba ya watu. Na wakastahiki ghadhabu
ya Mwenyezi Mungu, na wamepigwa na unyonge. Hayo ni kwa sababu walikuwa
wakizikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, na wakiwauwa Manabii pasina haki; hayo ni
kwa sababu waliasi na walikuwa wakiruka mipaka.
113. Wote hao si sawa sawa. Miongoni mwa Watu wa Kitabu
wamo watu walio simama baraabara, wanasoma Aya za Mwenyezi Mungu nyakati za
usiku, na pia wanasujudu.
114. Wanamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na
wanaamrisha mema na wanakataza maovu na wanakimbilia katika mambo ya kheri. Na
hao ndio miongoni mwa watenda mema.
115. Na kheri yoyote wanayo ifanya hawatanyimwa malipwa
yake. Na Mwenyezi Mungu anawajua wachamngu.
116. Hakika wale walio kufuru hazitawafaa kitu mali zao
wala watoto wao mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio watu wa Motoni - humo
watadumu.
117. Mfano wa vile wanavyo vitoa katika uhai wao wa duniani
ni kama upepo ambao ndani yake ipo baridi ya barafu, ukalisibu shamba la watu
walio dhulumu nafsi zao, ukaliteketeza. Na Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu, bali
wao wenyewe wanadhulumu nafsi zao.
118. Enyi mlio amini! Msiwafanye wasiri wenu watu wasio
kuwa katika nyinyi. Hawataacha kukufanyieni ubaya. Wanayapenda yanayo
kudhuruni. Imekwisha fichuka chuki yao katika midomo yao. Na yanayo ficha vifua
vyao ni makubwa zaidi. Tumekwisha kubainishieni Ishara ikiwa nyinyi mtayatia
akilini.
119. Hivyo basi nyinyi ndio mnawapenda watu hao, wala wao
hawakupendeni. Nanyi mnaviamini Vitabu vyote. Na wanapo kutana nanyi husema:
Tumeamini. Na wanapo kuwa peke yao wanakuumieni vidole kwa chuki. Sema: Kufeni
kwa chuki yenu! Hakika Mwenyezi Mungu anayajua yaliomo vifuani.
120. Ikikupateni kheri huwaudhi. Na ikikupateni shari
wanafurahia. Na nyinyi mkisubiri na mkajizuilia, hila zao hazitakudhuruni kitu.
Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyazunguka yote wayatendayo.
121. Na pale ulipo toka asubuhi, ukaacha ahali zako
uwapange Waumini kwenye vituo kwa ajili ya vita - na Mwenyezi Mungu anasikia na
anajua.
122. Makundi mawili miongoni mwenu yakaingiwa na woga kuwa
watashindwa - na hali Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wao; na Waumini wamtegemee
Mwenyezi Mungu tu.
123. Na Mwenyezi Mungu alikwisha kunusuruni katika Badri
nanyi mlikuwa wanyonge. Basi mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kushukuru.
124. Ulipo waambia Waumini: Je, haitakutosheni ikiwa Mola
wenu atakusaidieni kwa Malaika elfu tatu walio teremshwa?
125.
Kwani! Ikiwa mtavumilia na mkamchamngu na hata maadui wakikutokeeni kwa ghafla,
basi hapo Mola wenu Mlezi atakusaidieni kwa Malaika elfu tano wanao shambulia
kwa nguvu.
126. Na
Mwenyezi Mungu hakufanya haya ila kuwa ni bishara kwenu, na ili nyoyo zenu
zipate kutua. Na msaada hautoki isipo kuwa kwa Mwenyezi Mungu, Aliye tukuka,
Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
127. Haya
ni kwa ajili awakate sehemu katika walio kufuru, au awahizi wapate kurejea
nyuma nao wamepwelewa.
128. Wewe
huna lako jambo katika haya - ama atawahurumia au atawaadhibu, kwani wao ni
madhaalimu.
129. Na ni
vya Mwenyezi Mungu vyote vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi.
Yeye humsamehe na humuadhibu amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Msamehevu Mwenye
kurehemu.
130. Enyi mlio amini! Msile riba mkizidisha juu kwa juu, na
mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufanikiwa.
131. Na uogopeni Moto ambao umeandaliwa kwa ajili ya
makafiri.
132. Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume ili mpate
kurehemewa.
133. Na yakimbilieni maghfira ya Mola wenu Mlezi, na Pepo
ambayo upana wake ni mbingu na ardhi, iliyo wekwa tayari kwa wachamngu,
134. Ambao hutoa wanapo kuwa na wasaa na wanapo kuwa na
dhiki, na wanajizuia ghadhabu, na wasamehevu kwa watu; na Mwenyezi Mungu
huwapenda wafanyao wema;
135. Na ambao pindi wafanyapo uchafu au wakajidhulumu nafsi
zao humkumbuka Mwenyezi Mungu na wakamwomba msamaha kwa dhambi zao - na nani
anaye futa dhambi isipo kuwa Mwenyezi Mungu? - na wala hawaendelei na waliyo
yafanya na hali wanajua.
136. Hao malipo yao ni msamaha kwa Mola wao Mlezi, na
Bustani zipitazo mito kati yake. Humo watadumu, na mwema mno ujira wa watendao.
137. Kabla yenu zimepita nyendo nyingi; basi tembeeni
katika ulimwengu muangalie vipi ulikuwa mwisho wa wanao kanusha.
138. Hii ni bayana kwa watu wote, na ni uwongofu, na
mawaidha kwa wachamngu.
139. Wala msilegee, wala msihuzunike, kwani nyinyi ndio wa
juu mkiwa ni Waumini.
140. Kama yamekupateni majaraha, basi na hao watu wengine
yamewapata majaraha mfano wa haya. Na siku za namna hii tunaweletea watu kwa
zamu, ili Mwenyezi Mungu awapambanue walio amini na awateuwe miongoni mwenu
mashahidi. Na Mwenyezi Mungu hawapendi madhaalimu;
141. Na pia ili Mwenyezi Mungu awasafishe walio amini na
awafutilie mbali makafiri.
142. Je! Mnadhani mtaingia Peponi na hali Mwenyezi Mungu
hajawapambanua wale miongoni mwenu walio pigana Jihadi, na hajawapambanua walio
subiri?
143. Na nyinyi mlikuwa mkitamani mauti kabla hamjakutana
nayo. Basi sasa mmekwisha yaona na huku mnayatazama.
144. Na Muhammad hakuwa ila ni Mtume tu. Wamekwisha pita
kabla yake Mitume. Je, akifa au akauwawa ndiyo mtageuka mrudi nyuma? Na atakaye
geuka akarudi nyuma huyo hatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu
atawalipa wanao mshukuru.
145. Na haiwezi nafsi kuwa ife ila kwa idhini ya Mwenyezi
Mungu kama ilivyo andikwa ajali yake. Na mwenye kutaka malipo ya duniani
tutampa; na mwenye kutaka malipo ya Akhera tutampa. Na tutawalipa wenye
kushukuru.
146. Na Manabii wangapi walipigana na pamoja nao Waumini
wengi wenye ikhlasi! Hawakufanya woga kwa yaliyo wasibu katika Njia ya Mwenyezi
Mungu, wala hawakudhoofika wala hawakuwa wanyonge. Na Mwenyezi Mungu huwapenda
wanao subiri.
147. Wala kauli yao haikuwa ila ni kusema: Mola wetu Mlezi!
Tughufirie madhambi yetu na kupita kwetu kiasi katika mambo yetu, na isimamishe
imara miguu yetu na utunusuru tuwashinde kaumu ya makafiri.
148. Basi Mwenyezi Mungu akawapa malipo ya duniani na bora
ya malipo ya Akhera. Na Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao mema.
149. Enyi mlio amini! Ikiwa mtawat'ii walio kufuru
watakurudisheni nyuma, na hapo mtageuka kuwa wenye kukhasiri.
150. Bali Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wenu, naye ndiye bora
wa wasaidizi.
|