1 - 50
1. Enyi
watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na
akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao
wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Mwenyezi Mungu ambaye kwaye
mnaombana, na jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaangalieni.
2. Na wapeni mayatima mali yao. Wala msibadilishe kibaya
kwa kizuri. Wala msile mali zao pamoja na mali zenu. Hakika yote hayo ni jukumu
kubwa.
3. Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu,
basi oeni mnao wapenda katika wanawake, wawili au watatu au wane. na mkiogopa
kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu, au wale ambao mikono yenu ya
kulia imewamiliki. Kufanya hivi ndiko kutapelekea msikithirishe wana.
4. Na wapeni wanawake mahari yao hali ya kuwa ni kipawa.
Lakini wakikutunukieni kitu katika mahari, kwa radhi yao, basi kileni kiwashuke
kwa raha.
5. Wala msiwape wasio na akili mali yenu ambayo Mwenyezi
Mungu ameyajaalia yawe ni kiamu yenu. Walisheni katika hayo na muwavike, na
mseme nao maneno mazuri.
6. Na wajaribuni mayatima mpaka wafike umri wa kuoa.
Mkiwaona ni wekevu, basi wapeni mali yao. Wala msiyale kwa fujo na pupa kwa
kuwa watakuja kuwa watu wazima. Na aliye kuwa tajiri naajizuilie, na aliye
fakiri basi naale kwa kadri ya ada. Na mtakapo wapa mali yao washuhudizieni. Na
Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mhasibu.
7. Wanaume wana sehemu katika wanayo yaacha wazazi na jamaa
walio karibia. Na wanawake wanayo sehemu katika waliyo yaacha wazazi na jamaa
walio karibia. Ikiwa kidogo au
kingi. Hizi ni sehemu zilizo faridhiwa.
8. Na wakati wa
kugawanya wakihudhuria jamaa na mayatima na masikini, wapeni katika hayo mali
ya urithi, na semeni nao maneno mema.
9. Na wachelee
wale ambao lau kuwa na wao wangeli acha nyuma yao watoto wanyonge wangeli
wakhofia. Basi nao wamche Mwenyezi Mungu, na waseme maneno yaliyo sawa.
10. Hakika wanao
kula mali ya mayatima kwa dhulma, hapana shaka yoyote wanakula matumboni mwao
moto, na wataingia Motoni.
11. Mwenyezi
Mungu anakuusieni juu ya watoto wenu: Fungu la mwanamume ni kama fungu la
wanawake wawili. Na ikiwa wanawake zaidi ya wawili, basi watapata thuluthi
mbili za alicho kiacha maiti. Lakini akiwa mtoto mwanamke ni mmoja, basi fungu
lake ni nusu. Na wazazi wake wawili, kila mmoja wao apate sudusi ya alicho
kiacha, ikiwa anaye mtoto. Akiwa hana mtoto, na wazazi wake wawili wamekuwa
ndio warithi wake, basi mama yake atapata thuluthi moja. Na akiwa anao
ndugu, basi mama yake atapata sudusi. Haya ni baada ya kutolewa alicho usia au
kulipa deni. Baba zenu na watoto wenu, nyinyi hamjui ni nani baina yao aliye
karibia zaidi kwenu kwa manufaa. Hiyo ni Sharia iliyo toka kwa Mwenyezi Mungu.
Bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hikima.
12. Na fungu lenu ni nusu walicho acha wake zenu ikiwa
hawana mtoto. Wakiwa na mtoto basi fungu lenu ni robo ya walicho acha, baada ya
wasia waliyo usia au kulipa deni. Na wake zenu watapata robo mlicho kiacha,
ikiwa hamna mtoto. Mkiwa mna mtoto basi sehemu yao ni thumni ya mlicho kiacha,
baada ya wasia mlio usia au kulipa deni. Na ikiwa mwanamume au mwanamke anaye
rithiwa hana mtoto wala wazazi, lakini anaye ndugu mume au ndugu mke, basi kila
mmoja katika hawa atapata sudusi. Na wakiwa zaidi kuliko hivyo basi
watashirikiana katika thuluthi, baada ya wasia ulio usiwa au kulipa deni, pasio
kuleta dhara. Huu ndio wasia ulio toka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni
Mjuzi na Mpole.
13. Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na anaye mt'ii
Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Yeye atamtia katika Pepo zipitazo mito kati yake,
wadumu humo. Na huko ndiko kufuzu kukubwa.
14. Na anaye muasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na
akaipindukia mipaka yake, (Mwenyezi Mungu) atamtia Motoni adumu humo, na
atapata adhabu ya kudhalilisha.
15. Na ambao wanafanya uchafu miongoni mwa wanawake wenu,
washuhudizieni watu wane katika nyinyi. Watakapo shuhudia, basi wazuieni
majumbani mpaka wafishwe na mauti au Mwenyezi Mungu awatolee njia nyengine.
16. Na wawili kati yenu wafanyao hayo waadhibuni. Na
wakitubia wakatengenea basi waacheni. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa
kupokea toba, Mwenye kurehemu.
17. Hakika toba inayo kubaliwa na Mwenyezi Mungu ni ya wale
wafanyao uovu kwa ujinga, kisha wakatubia kwa haraka. Hao ndio Mwenyezi Mungu
huwakubalia toba yao, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na ni Mwenye hikima.
18. Wala hawana toba wale wafanyao maovu mpaka yakamfikia
mmoja wao mauti, kisha hapo akasema: Hakika mimi sasa nimetubia. Wala wale
wanao kufa na hali wao ni makafiri. Hao tumewaandalia adhabu chungu.
19. Enyi mlio amini! Si halali kwenu kuwarithi wanawake kwa
nguvu. Wala msiwadhikishe ili mwapokonye baadhi ya mlivyo wapa - isipo kuwa
wakifanya uchafu ulio wazi. Na kaeni nao kwa wema, na ikiwa mmewachukia, basi
huenda mkakichukia kitu, na Mwenyezi Mungu ametia kheri nyingi ndani yake.
20. Na mkitaka kubadilisha mke mahali pa mke, na hali mmoja
wao mmempa chungu ya mali, basi msichukue katika hayo kitu chochote. Je,
mtachukua kwa dhulma na kosa lilio wazi?
21. Na mtachukuaje na ilhali mmekwisha ingiliana nyinyi kwa
nyinyi, na wao wanawake wamechukua kwenu ahadi iliyo madhubuti?
22. Wala msiwaoe wake walio waoa baba zenu, ila yaliyo
kwisha pita. Hakika huo ni uchafu na uchukizo na ni njia mbaya.
23. Mmeharimishiwa mama zenu, na binti zenu, na dada zenu,
na shangazi zenu, na khaalati zenu, na binti wa ndugu mume, na binti wa dada,
na mama zenu walio kunyonyesheni, na dada zenu kwa kunyonya, na mama wa wake
zenu, na watoto wenu wa kambo walio katika ulinzi wenu walio zaliwa na wake
zenu mlio waingilia. Ikiwa hamkuwaingilia basi hapana lawama juu yenu. (Pia
mmeharimishwa) wake wa watoto wenu walio toka katika migongo yenu. Na kuwaoa
pamoja dada wawili isipo kuwa yale yaliyo kwisha pita. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
24. NA WANAWAKE wenye waume, isipo kuwa walio milikiwa na
mikono yenu ya kulia. Ndiyo Sharia ya Mwenyezi Mungu juu yenu. Na
mmehalilishiwa wasio kuwa hao, mtafute kwa mali yenu kwa kuowa pasina kuzini.
Kama mnavyo starehe nao, basi wapeni mahari yao kwa kuwa ni waajibu. Wala
hapana lawama juu yenu kwa mtakacho kubaliana baada ya kutimiza waajibu. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua na Mwenye hikima.
25. Na asiyeweza kati yenu kupata mali ya kuolea wanawake
wa kiungwana Waumini, na aoe katika vijakazi Waumini iliyo wamiliki mikono yenu
ya kulia. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa imani yenu. Nyinyi mmetokana wenyewe
kwa wenyewe. Basi waoeni kwa idhini ya watu wao, na wapeni mahari yao kama ada,
wawe wanawake wema, si makahaba wala si mahawara. Na wanapo olewa kisha
wakafanya uchafu basi adhabu yao itakuwa ni nusu ya adhabu waliyo wekewa
waungwana. Hayo ni kwa yule miongoni mwenu anaye ogopa kuingia katika zina. Na
mkisubiri ndio bora kwenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye
kurehemu.
26. Mwenyezi Mungu anataka kukubainishieni na kukuongozeni
nyendo za walio kuwa kabla yenu, na akurejezeni kwenye ut'iifu wake. Na
Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hikima.
27. Na Mwenyezi Mungu anataka kukurejezeni kwenye ut'iifu
wake, na wanao taka kufuata matamanio wanataka mkengeuke makengeuko makubwa.
28. Mwenyezi Mungu anataka kukupunguzieni taabu, na
mwanaadamu ameumbwa dhaifu.
29. Enyi mlio amini! Msiliane mali yenu kwa dhulma, isipo
kuwa iwe biashara kwa kuridhiana wenyewe. Wala msijiuwe. Hakika Mwenyezi Mungu
ni Mwenye kuwarehemuni.
30. Na mwenye kutenda hayo kwa uadui na udhaalimu, basi
huyo tutamwingiza Motoni. Na hilo ni jepesi kwa Mwenyezi Mungu.
31. Mkiyaepuka makubwa mnayo katazwa, tutakufutieni makosa
yenu madogo, na tutakuingizeni mahali patukufu.
32. Wala msitamani alicho wafadhili Mwenyezi Mungu baadhi
yenu kuliko wengine. Wanaume wana fungu katika walio vichuma, na wanawake wana
fungu katika walio vichuma. Na muombeni Mwenyezi Mungu fadhila zake. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
33. Na kila mmoja tumemwekea warithi katika waliyo yaacha
wazazi wawili na jamaa. Na mlio fungamana nao ahadi wapeni fungu lao. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Shahidi wa kila kitu.
34. Wanaume ni wasimamizi wa wanawake, kwa kufadhiliwa na
Mwenyezi Mungu baadhi yao juu ya baadhi, na kwa mali yao wanayo yatoa. Basi
wanawake wema ni wale wenye kut'ii na wanao jilinda hata katika siri kwa kuwa
Mwenyezi Mungu ameamrisha wajilinde. Na ambao mnachelea kutoka katika ut'iifu
wanasihini, muwahame katika malazi na wapigeni. Wakikut'iini msiwatafutie njia
ya kuwaudhi bure. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye aliye juu na Mkuu.
35. Na mkichelea kutakuwapo mfarakano baina ya mke na mume
basi pelekeni muamuzi kutokana na jamaa za mume, na muamuzi kutokana na jamaa
za mke. Wakitaka mapatano Mwenyezi Mungu atawawezesha. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mjuzi Mwenye khabari.
36. Muabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na
chochote. Na wafanyieni wema wazazi wawili na jamaa na mayatima na masikini na
jirani wa karibu na jirani wa mbali, na rafiki wa ubavuni na mpita njia, na
walio milikiwa na mikono yenu ya kulia. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wenye
kiburi wanao jifakhiri,
37. Ambao wanafanya ubakhili na wanaamrisha watu ubakhili,
na wanaficha fadhila alizo wapa Mwenyezi Mungu. Na tumewaandalia makafiri
adhabu ya fedheha,
38. Na ambao hutoa mali yao kwa kuonyesha watu, wala
hawamuamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho; na yule ambaye Shet'ani amekuwa
ndiye rafiki yake, basi ana rafiki mbaya mno.
39. Na ingeli wadhuru nini wao lau wangeli muamini Mwenyezi
Mungu na Siku ya Mwisho, na wakatoa katika aliyo waruzuku Mwenyezi Mungu? Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kuwajua vyema.
40. Hakika Mwenyezi Mungu hadhulumu hata uzito wa chembe
moja. Na ikiwa ni jambo jema basi Yeye hulizidisha na hutoa kutoka kwake malipo
makubwa.
41. Basi itakuwaje pindi tukiwaletea kutoka kila umma
shahidi, na tukakuleta wewe kuwa shahidi wa hawa?
42. Siku hiyo walio kufuru na wakamuasi Mtume watatamani
ardhi isawazishwe juu yao. Wala hawataweza kumficha Mwenyezi Mungu neno lolote.
43. Enyi mlio amini! Msikaribie Sala, hali mmelewa, mpaka
myajue mnayo yasema, wala hali mna janaba - isipo kuwa mmo safarini - mpaka
mkoge. Na mkiwa wagonjwa, au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni, au mmewagusa
wanawake - na msipate maji, basi ukusudieni mchanga safi, mpake nyuso zenu na
mikono yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu na Mwenye kughufiria.
44. Huwaoni wale walio pewa sehemu ya Kitabu wananunua
upotovu na wanakutakeni nanyi mpotee njia?
45. Na Mwenyezi Mungu anawajua vyema maadui zenu. Na
Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni Mlinzi, na anatosha kuwa ni Mwenye
kukunusuruni.
46. Miongoni mwa Mayahudi wamo ambao hubadilisha maneno
kuyatoa mahala pake, na husema: Tumesikia na tumeasi, na sikia bila ya
kusikilizwa. Na husema: "Raai'naa", kwa kuzipotoa ndimi zao ili
kuitukana Dini. Na lau kama wangeli sema: Tumesikia na tumet'ii, na usikie na
"Undhurna" (Utuangalie), ingeli kuwa ni kheri kwao na sawa zaidi.
Lakini Mwenyezi Mungu amewalaani kwa kufuru yao; basi hawaamini ila wachache
tu.
47. Enyi mlio pewa Kitabu! Aminini tuliyo yateremsha yenye
kusadikisha yale mliyo nayo, kabla hatujazigeuza nyuso tukazipeleka kisogoni,
au tukawalaani kama tulivyo walaani watu wa Sabato (Jumaamosi). Na amri ya
Mwenyezi Mungu ni lazima ifanyike.
48. Hakika Mwenyezi Mungu hasamehe kushirikishwa, na
husamehe yaliyo duni ya hilo kwa amtakaye. Na anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu
basi hakika amezua dhambi kubwa.
49. Jee huwaoni wale wanao dai kuwa ati wametakasika? Bali
Mwenyezi Mungu humtakasa amtakaye. Na hawatadhulumiwa hata kadiri ya kijiuzi
kilichomo ndani ya uwazi wa kokwa ya tende.
50. Tazama vipi wanavyo mzulia uwongo Mwenyezi Mungu, na
haya yatosha kuwa dhambi iliyo dhaahiri.
|