101 - 150
101. Na mnapo safiri katika nchi si vibaya kwenu kama
mkifupisha Sala, iwapo mnachelea wasije wale walio kufuru wakakuleteeni maudhi.
Hakika makafiri ni maadui zenu walio wazi wazi.
102. Na unapo kuwa pamoja nao, ukawasalisha, basi kundi
moja miongoni mwao wasimame pamoja nawe na wachukue silaha zao. Na watakapo
maliza sijida zao, basi nawende nyuma yenu, na lije kundi jingine ambalo
halijasali, lisali pamoja nawe. Nao wachukue hadhari yao na silaha zao. Walio
kufuru wanapenda mghafilike na silaha zenu na vifaa vyenu ili wakuvamieni
mvamio wa mara moja. Wala si vibaya kwenu ikiwa mnaona udhia kwa sababu ya mvua
au mkawa wagonjwa, mkaziweka silaha zenu. Na chukueni hadhari yenu. Hakika
Mwenyezi Mungu amewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha.
103. Mkisha sali basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu mkisimama,
na mkikaa, na mnapo jinyoosha kwa kulala. Na mtapo tulia basi shikeni Sala kama
dasturi. Kwani hakika Sala kwa Waumini ni faradhi iliyo wekewa nyakati maalumu.
104. Wala msifanye ulegevu kuwafukuzia kaumu ya maadui.
Ikiwa mnaumia, basi nao pia wanaumia kama mnavyo umia nyinyi. Nanyi mnataraji
kwa Mwenyezi Mungu wasio yataraji wao. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na
Mwenye hikima.
105. Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu hiki kwa haki ili
upate kuhukumu baina ya watu kwa alivyo kuonyesha Mwenyezi Mungu. Wala usiwe
mtetezi wa makhaaini.
106. Na muombe maghfira Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwingi wa maghfira, Mwenye kurehemu.
107. Wala
usiwatetee wanao khini nafsi zao. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi aliye khaaini,
mwenye dhambi.
108. Wanataka
kujificha kwa watu, wala hawataki kujificha kwa Mwenyezi Mungu, naye yu pamoja
nao pale wanapo panga njama usiku kwa maneno asiyo yapenda. Na Mwenyezi Mungu
anayajua vyema wanayo yatenda.
109. Hivyo
nyinyi mmewatetea hawa katika uhai huu wa duniani. Basi nani atakaye watetea
kwa Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama? Au ni nani atakuwa wakili wao wa kumtegemea?
110. Na
anaye tenda uovu au akajidhulumu nafsi yake, kisha akaomba maghfira kwa
Mwenyezi Mungu, atamkuta Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira, Mwenye kurehemu.
111. Na
anaye chuma dhambi, basi ameichumia nafsi yake mwenyewe. Na Mwenyezi Mungu ni
Mjuzi, Mwenye hikima.
112.Na
atendaye kosa au dhambi kisha akamsingizia asiye na kosa, basi amejitwika
dhulma na dhambi iliyo wazi.
113. Na
lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yako na rehema yake, kundi moja kati
yao linge dhamiria kukupoteza. Wala hawapotezi ila nafsi zao, wala hawawezi
kukudhuru kwa lolote. Na Mwenyezi Mungu amekuteremshia Kitabu na hikima na
amekufundisha uliyo kuwa huyajui. Na fadhila za Mwenyezi Mungu zilizo juu yako
ni kubwa.
114.
Hakuna kheri katika mengi ya wanayo shauriana kwa siri, isipo kuwa kwa yule
anaye amrisha kutoa sadaka, au kutenda mema, au kupatanisha baina ya watu. Na
mwenye kufanya hayo kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi tutakuja mpa ujira
mkubwa.
115. Na
anaye mpinga Mtume baada ya kumdhihirikia uwongofu, na akafuata njia isiyo kuwa
ya Waumini, tutamuelekeza aliko elekea, na tutamuingiza katika Jahannamu. Na
hayo ni marejeo maovu.
116. Hakika Mwenyezi Mungu hasamehi kushirikishwa na kitu.
Lakini Yeye husamehe yasiyo kuwa hayo kwa amtakaye. Na anaye mshirikisha
Mwenyezi Mungu basi huyo amepotea upotovu wa mbali.
117. Wao hawawaombi badala yake Yeye ila wanawake, wala
hawamuombi ila Shet'ani aliye asi.
118. Mwenyezi Mungu amemlaani. Naye Shet'ani alisema: Kwa
yakini nitawachukua sehemu maalumu katika waja wako.
119. Na hakika nitawapoteza na nitawatia matamanio, na
nitawaamrisha, basi watakata masikio ya wanyama, na nitawaamrisha, basi
watabadili aliyo umba Mwenyezi Mungu. Na mwenye kumfanya Shet'ani kuwa ni
mlinzi wake badala ya Mwenyezi Mungu, basi huyo amekhasiri khasara ya dhaahiri.
120. Anawaahidi na anawatia tamaa. Na Shet'ani hawaahidi
ila udanganyifu.
121. Hao makao yao ni Jahannamu, na wala hawapati
makimbilio kutoka humo.
122. Na wale walio amini na wakatenda mema, tutawaingiza
katika Bustani zipitayo mito kati yake. Watadumu humo milele. Ndiyo ahadi ya
Mwenyezi Mungu iliyo kweli. Na nani mkweli zaidi kwa usemi kuliko Mwenyezi
Mungu.
123. Si kwa matamanio yenu, wala matamanio ya Watu wa
Kitabu! Anaye fanya ubaya atalipwa kwalo, wala hatajipatia mlinzi wala wa
kumnusuru, isipo kuwa Mwenyezi Mungu.
124. Na anaye fanya mema, akiwa mwanamume au mwanamke, naye
ni Muumini - basi hao wataingia Peponi wala hawatadhulumiwa hata kadiri ya
tundu ya kokwa ya tende.
125. Na nani aliye bora kwa dini kuliko yule aliye
usilimisha uso wake kwa Mwenyezi Mungu, naye akawa mwema, na anafuata mila ya
Ibrahim mwongofu? Na Mwenyezi Mungu alimfanya Ibrahim kuwa ni rafiki mwendani.
126. Ni vya Mwenyezi Mungu tu vyote vilivyomo mbinguni na
vilivyomo duniani. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuvizunguka vitu vyote.
127. Wanakuuliza
nini sharia ya wanawake. Sema: Mwenyezi Mungu ana kutoleeni fatwa juu yao, na
mnayo somewa humu Kitabuni kukhusu mayatima wanawake ambao hamwapi walicho
andikiwa, na mnapenda kuwaoa, na kukhusu wanyonge katika watoto, na kwamba
mwasimamie mayatima kwa uadilifu. Na kheri yoyote mnayo fanya Mwenyezi Mungu
anaijua.
128. Na
mwanamke akichelea kutupwa au kutojaliwa na mumewe, basi si vibaya kwao
wakisikizana kwa suluhu. Na suluhu ni bora. Na nafsi zimewekewa machoni
mwake tamaa na choyo. Na mkifanya wema na mkamchamngu basi hakika Mwenyezi
Mungu anazo khabari za yote mnayo yatenda.
129. Wala hamtaweza kufanya uadilifu baina ya wake, hata
mkikakamia. Kwa hivyo msimili moja kwa moja mkamwacha (mmojapo) kama aliye
tundikwa. Na mkisikizana na mkamchamngu basi Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa
maghfira na Mwenye kurehemu.
130. Na wakitengana Mwenyezi Mungu atamtosheleza kila mmoja
katika wao kwa ukunjufu wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu Mwenye hikima.
131. Na ni vya Mwenyezi Mungu tu vyote viliomo katik mbingu
na viliomo katika dunia. Na kwa hakika tuliwausia walio pewa Kitabu kabla yenu,
na nyinyi pia, kwamba mumche Mwenyezi Mungu. Na mkikataa, basi ni vya Mwenyezi
Mungu viliomo mbinguni na viliomo duniani. Na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi,
anajitosha, na Msifiwa.
132. Na ni vya Mwenyezi Mungu viliomo katika mbingu na
viliomo katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mlinzi.
133. Akitaka atakuondoeni, enyi watu! Na awalete wengineo.
Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa hayo.
134. Anaye taka malipo ya dunia, basi kwa Mwenyezi Mungu yapo
malipo ya dunia na Akhera. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona.
135. Enyi mlio amini! Kuweni wenye kusimamisha uadilifu,
mtowao ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, ijapo kuwa ni juu ya nafsi zenu,
au wazazi wawili na jamaa zenu. Akiwa tajiri au masikini Mwenyezi Mungu
anawastahikia zaidi. Basi msifuate matamanio, mkaacha kufanya uadilifu. Na
mkiupotoa au mkajitenga nao basi Mwenyezi Mungu anajua vyema mnayo yatenda.
136. Enyi mlio amini! Muaminini Mwenyezi Mungu, na Mtume
wake, na Kitabu alicho kiteremsha juu ya Mtume wake, na Kitabu alicho kiteremsha
kabla yake. Na anaye mkataa Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake,
na Mitume wake, na Siku ya Akhera, basi huyo amekwisha potelea mbali.
137. Hakika walio amini, kisha wakakufuru, kisha wakaamini,
kisha wakazidi ukafiri, Mwenyezi Mungu hakuwa wa kuwaghufiria wala wa kuwaongoa
njia.
138. Wabashirie wanaafiki kwamba watapata adhabu chungu,
139. Wale ambao huwafanya makafiri kuwa ndio marafiki
badala ya Waumini. Je! Wanataka wapate kwao utukufu? Basi hakika utukufu wote
ni wa Mwenyezi Mungu.
140. Naye amekwisha kuteremshieni katika Kitabu hiki ya
kwamba mnapo sikia Aya za Mwenyezi Mungu zinakanushwa na zinafanyiwa kejeli,
basi msikae pamoja nao, mpaka waingie katika mazungumzo mengine. Hivyo mtakuwa
nanyi mfano wao hao. Hakika Mwenyezi Mungu atawakusanya wanaafiki na makafiri
wote pamoja katika Jahannamu,
141. Wale ambao wanakungojeeni, mkipata ushindi unao toka
kwa Mwenyezi Mungu wao husema: Si tulikuwa pamoja nanyi vile? Na ikiwa ni
sehemu ya makafiri kushinda wao huwaambia: Hatukuwa ni waweza wa kukushindeni,
nasi tukakukingeni na hawa Waumini? Basi Mwenyezi Mungu atahukumu baina yenu
Siku ya Kiyama, wala Mwenyezi Mungu hatawapa makafiri njia ya kuwashinda
Waumini.
142. Hakika wanaafiki wanamkhadaa Mwenyezi Mungu, na hali
ni Yeye ndiye mwenye kuwakhadaa wao. Na wanapo inuka kusali huinuka kwa
unyong'onyo, wanajionyesha kwa watu tu, wala hawamdhukuru Mwenyezi Mungu ila
kidogo tu.
143. Wanayumba yumba baina ya huku na huko. Huku hawako na
huko hawako. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea, kabisa hutompatia
njia.
144. Enyi mlio amini! Msiwafanye makafiri kuwa ndio
marafiki badala ya Waumini. Je, mnataka Mwenyezi Mungu awe na hoja iliyo wazi
juu yenu?
145. Hakika wanaafiki watakuwa katika t'abaka ya chini
kabisa Motoni, wala hutompata yeyote wa kuwanusuru.
146. Isipo kuwa wale walio tubu, na wakatengeneza na
wakashikamana na Mwenyezi Mungu, na wakamtakasia Dini yao Mwenyezi Mungu. Basi
hao ni pamoja na Waumini. Na Mwenyezi Mungu atakuja wapa Waumini ujira mkubwa.
147. Mwenyezi Mungu hakuadhibuni mkimshukuru na mkamuamini.
Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kupokea shukrani na ndiye Mwenye kujua.
148. MWENYEZI MUNGU hapendi uovu uenezwe kwa maneno ila kwa
mwenye kudhulumiwa. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua.
149. Mkidhihirisha wema au mkiuficha, au mkiyasamehe maovu,
hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira na Muweza.
150. Hakika wale wanao mkataa Mwenyezi Mungu na Mitume
wake, na wanataka kufarikisha baina ya Mwenyezi Mungu na Mitume wake, kwa
kusema: Wengine tunawaamini na wengine tunawakataa. Na wanataka kushika njia
iliyo kati kati ya haya,
|