151 - 176
151. Hao ndio makafiri kweli. Na tumewaandalia makafiri
adhabu ya kudhalilisha.
152. Na walio muamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, wala
wasimfarikishe yeyote kati yao, hao atawapa ujira wao. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwingi wa maghfira, na Mwenye kurehemu.
153. Watu wa Kitabu wanakutaka uwateremshia kitabu kutoka
mbinguni. Na kwa hakika walikwisha mtaka Musa makubwa kuliko hayo. Walisema:
Tuonyeshe Mwenyezi Mungu wazi wazi. Wakapigwa na radi kwa hiyo dhulma yao.
Kisha wakamchukua ndama kumuabudu, baada ya kwisha wajia hoja zilizo wazi. Nasi
tukasamehe hayo, na tukampa Musa nguvu zilizo dhaahiri.
154. Na tukanyanyua mlima juu yao kwa kufanya agano nao. Na
tukawaambia: Ingilieni mlangoni kwa unyenyekevu. Na tukawaambia: Msiivunje Siku
ya Sabato (Jumaa mosi). Na tukachukua kwao ahadi iliyo madhubuti.
155. Basi kwa sababu ya kuvunja kwao ahadi zao, na
kuzikataa kwao ishara za Mwenyezi Mungu, na kuwauwa kwao Manabii bila ya haki,
na kusema kwao: Nyoyo zetu zimefumbwa; bali Mwenyezi Mungu amezipiga muhuri kwa
kufuru zao, basi hawaamini ila kidogo tu -
156. Na pia kwa kufuru zao na kumsingizia kwao Maryamu
uwongo mkubwa,
157. Na kwa kusema kwao: Sisi tumemuuwa Masihi Isa, mwana
wa Maryamu, Mtume wa Mwenyezi Mungu - nao hawakumuuwa wala hawakumsalibu, bali
walifananishiwa tu. Na hakika walio khitalifiana katika haya wamo katika shaka
nayo. Wao hawana ujuzi nayo wowote, ila ni kufuata dhana tu. Wala hawakumuuwa
kwa yakini.
158. Bali Mwenyezi Mungu alim- tukuza kwake, na hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
159. Na hawi katika Watu wa Kitabu ila hakika atamuamini
yeye kabla ya kufa kwake. Naye Siku ya Kiyama atakuwa shahidi juu yao.
160. Basi kwa dhulma yao Mayahudi tuliwaharimishia vitu
vizuri walivyo halalishiwa. Na kwa sababu ya kuwazuilia kwao watu wengi na Njia
ya Mwenyezi Mungu,
161. Na kuchukua kwao riba, nao wamekatazwa, na kula kwao
mali ya watu kwa dhulma. Basi tumewaandalia makafiri katika wao adhabu yenye
uchungu.
162. Lakini walio bobea katika ilimu miongoni mwao, na
Waumini, wanayaamini uliyo teremshiwa wewe, na yaliyo teremshwa kabla yako. Na
wanao shika Sala, na wakatoa Zaka, na wanao muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya
Mwisho - hao tutawapa malipo makubwa.
163. Hakika Sisi tumekuletea wahyi wewe kama tulivyo
wapelekea wahyi Nuhu na Manabii walio kuwa baada yake. Na tulimpelekea wahyi
Ibrahim na Ismail na Is-haka na Yaakub na wajukuu zake, na Isa na Ayub na Yunus
na Harun na Suleiman, na Daud tukampa Zaburi.
164. Na Mitume tulio kwisha kukuhadithia kabla yake, na
Mitume wengine hatukukuhadithia. Na Mwenyezi Mungu alinena na Musa kwa maneno.
165. Mitume hao ni wabashiri na waonyaji, ili watu wasiwe
na hoja juu ya Mwenyezi Mungu baada ya kuletewa Mitume. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
166. Lakini Mwenyezi Mungu anayashuhudia aliyo kuteremshia
wewe. Ameyateremsha kwa kujua kwake - na Malaika pia wanashuhudia. Na Mwenyezi
Mungu anatosha kuwa shahidi.
167. Hakika walio kufuru na wakazuilia Njia ya Mwenyezi
Mungu, wamekwisha potelea mbali.
168. Hakika wale walio kufuru na wakadhulumu hawi Mwenyezi
Mungu kuwasamehe wala kuwaongoa njia.
169. Isipo kuwa njia ya Jahannamu. Humo watadumu milele. Na
hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.
170. Enyi
Watu! Amekwisha kujieni Mtume huyu na haki itokayo kwa Mola wenu Mlezi. Basi
aminini, ndiyo kheri yenu. Na mkikakanusha basi hakika viliomo mbinguni na
duniani ni vya Mwenyezi Mungu tu. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye
hikima.
171. Enyi
Watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini yenu, wala msimseme Mwenyezi Mungu
ila kwa lilio kweli. Hakika Masihi Isa mwana wa Maryamu ni Mtume wa Mwenyezi
Mungu, na neno lake tu alilo mpelekea Maryamu, na ni roho iliyo toka kwake. Basi
Muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume wake. Wala msiseme: Utatu. Komeni! Itakuwa kheri kwenu. Hakika Mwenyezi Mungu
ni Mungu mmoja tu. Ametukuka Yeye na kuwa na mwana. Ni vyake Yeye vyote viliomo
katika mbingu na katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni Mtegemewa wa kutosha.
172. Masihi
hataona uvunjifu kuwa mtumwa wa Mwenyezi Mungu, wala Malaika walio karibishwa.
Na watakao ona uvunjifu utumwa wa Mwenyezi Mungu na kufanya kiburi, basi
atawakusanya wote kwake.
173. Na ama walio
amini na wakatenda mema atawalipa ujira wao sawa sawa, na atawazidishia kwa
fadhila yake. Na ama wale walio ona uvunjifu na wakafanya kiburi, basi
atawaadhibu adhabu iliyo chungu. Wala hawatopata mlinzi wala wa kuwanusuru
asiye kuwa Mwenyezi Mungu.
174. Enyi
watu! Umekufikieni ushahidi kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Na
tumekuteremshieni Nuru iliyo wazi.
175. Ama wale walio muamini Mwenyezi Mungu, na
wakashikamana naye, basi atawatia katika rehema yake na fadhila, na atawaongoa
kwenye Njia Iliyo Nyooka.
176. Wanakuomba uhukumu, sema: Mwenyezi Mungu anakupeni
hukumu juu ya mkiwa. Ikiwa mtu amekufa, naye hana mtoto, lakini anaye ndugu wa
kike, basi huyo atapata nusu alicho acha maiti. Na mwanamume atamrithi ndugu wa
kike ikiwa hana mwana. Na ikiwa wao ni ndugu wa kike wawili, basi watapata
thuluthi mbili za alicho acha maiti. Na wakiwa ndugu wanaume na wanawake, basi
mwanamume atapata sehemu iliyo sawa na ya wanawake wawili. Mwenyezi Mungu
anakubainishieni ili msipotee; na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
|