1 - 50
1. Enyi mlio amini! Timizeni ahadi. Mmehalalishiwa wanyama
wa mifugo, ila wale mnao tajiwa. Lakini msihalalishe kuwinda nanyi mmo katika
Hija. Hakika Mwenyezi Mungu anahukumu apendavyo.
2. Enyi mlio amini! Msivunje hishima ya alama ya Dini ya
Mwenyezi Mungu wala mwezi mtakatifu, wala wanyama wanao pelekwa Makka
kuchinjwa, wala vigwe vyao, wala wanao elekea kwendea Nyumba Takatifu,
wakitafuta fadhila na radhi za Mola wao Mlezi. Na mkisha toka Hija yenu basi
windeni. Wala kuwachukia watu kwa kuwa wali- kuzuilieni kufika Msikiti
mtakatifu kusikupelekeeni kuwafanyia uadui. Na saidianeni katika wema na
uchamngu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Mwenyezi Mungu.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
3. Mmeharimishiwa nyamafu, na damu, na nyama ya nguruwe, na
mnyama aliye chinjwa si kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na aliye kufa kwa kunyongeka
koo, na aliye kufa kwa kupigwa, na aliye kufa kwa kuanguka, na aliye kufa kwa
kupigwa pembe, aliye liwa na mnyama, ila mkimdiriki kumchinja. Na pia ni haramu
kula nyama aliye chinjiwa masanamu. Na ni haramu kupiga ramli. Hayo yote ni
upotovu. Leo walio kufuru wamekata tamaa na Dini yenu; basi msiwaogope, bali
niogopeni Mimi. Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema
yangu, na nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini. Na mwenye kushurutishwa na
njaa, bila ya kupendelea dhambi, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu na
Mwenye kurehemu.
4.
Wanakuuliza wamehalalishiwa nini? Sema: Mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri na
mlicho wafundisha wanyama kukiwinda. Mnawafundisha alivyo kufunzeni Mwenyezi
Mungu. Basi kuleni walicho kukamatieni, na mkisomee jina la Mwenyezi Mungu. Na
mcheni Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.
5. Leo
mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri. Na chakula cha walio pewa Kitabu ni halali
kwenu, na chakula chenu ni halali kwao. Na pia wanawake wema miongoni mwa Waumini,
na wanawake wema miongoni mwa walio pewa Kitabu kabla yenu, mtakapo wapa mahari
yao, mkafunga nao ndoa, bila ya kufanya uhasharati wala kuwaweka kinyumba. Na
anaye kataa kuamini bila shaka a'mali yake imepotea, naye katika Akhera atakuwa
miongoni mwa wenye khasara.
6. Enyi mlio amini! Mnapo simama kwa ajili ya Sala basi
osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu, na
osheni miguu yenu mpaka vifundoni. Na mkiwa na janaba basi ogeni. Na mkiwa
wagonjwa au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni au mmewagusa wanawake,
na hamkupata maji, basi tayamamuni vumbi lilio safi, na mpake nyuso zenu na
mikono yenu. Hapendi Mwenyezi Mungu kukutieni katika taabu; bali anataka
kukutakaseni na kutimiza neema yake juu yenu ili mpate kushukuru.
7. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu, na
ahadi yake aliyo fungamana nanyi mlipo sema: Tumesikia na tumet'ii. Na mcheni
Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi sana wa yaliyomo vifuani.
8. Enyi mlio amini! Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili
ya Mwenyezi Mungu mkitoa ushahidi kwa haki. Wala kuchukiana na watu
kusikupelekeeni kutofanya uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndio kuwa karibu
mno na uchamngu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari
za mnayo yatenda.
9. Mwenyezi Mungu amewaahidi walio muamini na wakatenda
mema kwamba watapata maghfira na malipo makubwa.
10. Na wale walio kufuru na wakakanusha Ishara zetu, hao
ndio watu wa Motoni.
11. Enyi mlio amini! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu
zilizo juu yenu, walipo taka watu kukunyooshieni mikono, naye akaizuilia mikono
yao kukufikieni. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na Waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu
tu.
12. Na Mwenyezi Mungu alifanya agano na Wana wa Israili. Na
tukawateulia kutokana nao wakuu kumi na mbili. Na Mwenyezi Mungu akasema: Kwa
yakini Mimi ni pamoja nanyi. Mkisali, na mkatoa Zaka, na mkawaamini Mitume
wangu, na mkawasaidia, na mkamkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema, hapana shaka
nitakufutieni maovu yenu na nitakuingizeni katika mabustani yapitayo mito kati
yake. Lakini atakaye kufuru miongoni mwenu baada ya hayo bila ya shaka atakuwa
amepotea njia iliyo sawa.
13. Basi kwa sababu ya kuvunja agano lao tuliwalaani, na
tukazifanya nyoyo zao kuwa ngumu. Wanayabadilisha maneno kutoka pahala pake, na
wamesahau sehemu ya yale waliyo kumbushwa. Na huachi kuvumbua khiana kutokana
nao, isipo kuwa wachache miongoni mwao. Basi wasamehe na waache. Hakika
Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.
14. Na kutoka kwa wale walio sema: Sisi ni Manasara,
tulichukua ahadi yao, lakini wakasahau sehemu ya waliyo kumbushwa. Kwa hivyo
tukaweka kati yao uadui na chuki mpaka Siku ya Kiyama. Na hapo Mwenyezi Mungu atawaambia
waliyo kuwa wakiyafanya.
15. Enyi
Watu wa Kitabu! Amekwisha kujieni Mtume wetu anaye kufichulieni mengi mliyo
kuwa mkiyaficha katika Kitabu, na anaye samehe mengi. Bila shaka imekujieni
kutoka kwa Mwenyezi Mungu nuru na Kitabu kinacho bainisha.
16.
Mwenyezi Mungu huwaongoa wenye kufuata radhi yake katika njia za salama, na
huwatoa katika giza kuwapeleka kwenye nuru kwa amri yake, na huwaongoa kwenye
njia iliyo nyooka.
17. Hakika
wamekufuru walio sema: Mwenyezi Mungu ni Masihi mwana wa Maryamu. Sema: Ni nani
mwenye kumiliki cho chote mbele ya Mwenyezi Mungu ikiwa Yeye angetaka
kumuangamiza Masihi mwana wa Maryamu, na mama yake, na wote waliomo katika
ardhi? Na mamlaka ya mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ni vya Mwenyezi
Mungu. Huumba apendavyo. Na Mwenyezi Mungu anao uweza juu ya kila kitu.
18. Na
Mayahudi na Wakristo wanasema: Sisi ni wana wa Mwenyezi Mungu na vipenzi vyake.
Sema: Basi kwa nini anakuadhibuni kwa ajili ya dhambi zenu? Bali nyinyi ni watu
tu kama wale wengine alio waumba. Humsamehe amtakaye na humuadhibu amtakaye. Na
ni wa Mwenyezi Mungu tu ufalme wa mbingu na ardhi. Na marejeo ni kwake Yeye.
19. Enyi
Watu wa Kitabu! Bila ya shaka amekujilieni Mtume wetu akikubainishieni katika
wakati usio kuwa na Mitume, msije mkasema: Hakufika kwetu mbashiri wala mwonyaji.
Basi amekujieni mbashiri na mwonyaji. Na Mwenyezi Mungu anao uweza wa
kila kitu.
20. Na pale Musa alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu!
Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilizo juu yenu, alipo wateuwa Manabii kati
yenu, na akakufanyeni watawala, na akakupeni ambayo hakuwapa wowote katika
walimwengu.
21. Enyi watu
wangu! Ingieni katika nchi takatifu ambayo Mwenyezi Mungu amekuandikieni. Wala
msirudi nyuma, msije mkawa wenye kukhasirika.
22.
Wakasema: Ewe Musa! Huko wako watu majabari. Nasi hatutaingia huko mpaka wao
watoke humo. Wakitoka humo hapo tutaingia.
23. Watu wawili miongoni mwa wachamngu ambao Mwenyezi Mungu
amewaneemesha, walisema: Waingilieni kwa mlangoni. Mtakapo waingilia basi kwa
yakini nyinyi mtashinda. Na mtegemeeni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni Waumini.
24. Wakasema: Ewe Musa! Sisi hatutaingia humo kamwe maadamu
wao wamo humo. Basi nenda wewe na Mola wako Mlezi mkapigane. Sisi tutakaa hapa
hapa.
25. Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi similiki ila
nafsi yangu na ndugu yangu. Basi tutenge na hawa watu wapotovu.
26.(Mwenyezi Mungu) akasema: Basi nchi hiyo wameharimishiwa
muda wa miaka arubaini, watakuwa wakitanga-tanga katika ardhi. Basi wewe
usiwasikitikie watu wapotovu.
27. Na wasomee khabari za wana wawili wa Adam kwa kweli.
Walipo toa mhanga, ukakubaliwa wa mmoja wao, na wa mwengine haukukubaliwa.
Akasema: Nitakuuwa. Akasema mwengine: Mwenyezi Mungu huwapokelea wachamngu.
28.Ukininyooshea mkono wako kuniuwa, mimi sitakunyooshea
mkono wangu kukuuwa. Hakika mimi namwogopa Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu
wote.
29. Mimi nataka ubebe dhambi zangu na dhambi zako, kwani
wewe utakuwa miongoni mwa watu wa Motoni. Na hayo ndiyo malipo ya wenye
kudhulumu.
30. Basi nafsi yake ikampelekea kumuuwa nduguye, akamuuwa
na akawa miongoni mwa wenye kukhasirika.
31. Hapo Mwenyezi Mungu akamleta kunguru anaye fukua katika
ardhi ili amwonyeshe vipi kumsitiri nduguye. Akasema: Ole wangu! Nimeshindwa kuwa kama kunguru huyu nikamsitiri ndugu
yangu? Basi akawa miongoni mwa wenye kujuta.
32. Kwa sababu ya hayo tuliwaandikia Wana wa Israili ya
kwamba aliye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi katika nchi,
basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama
amewaokoa watu wote. Na hakika waliwajia Mitume wetu na hoja zilizo wazi. Kisha
wengi katika wao baada ya haya wakawa waharibifu katika nchi.
33.Basi malipo ya wale wanao mpiga vita Mwenyezi Mungu na
Mtume wake na wakawania kufanya uchafuzi katika nchi, ni kuuwawa, au
kusalibiwa, au kukatwa mikono yao na miguu yao kwa mabadilisho, au kutolewa
nchi. Hii ndiyo hizaya yao katika dunia; na katika Akhera watapata adhabu
kubwa.
34. Isipo kuwa wale walio tubu kabla hamjawatia nguvuni. Na
jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu.
35. Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na tafuteni
njia ya kumfikilia. Na wanieni kwa juhudi kwa ajili yake ili mpate kuokoka.
36. Hakika walio kufuru lau wange kuwa na yote yaliyomo
duniani, na mengine kama hayo, ili watoe fidia ya kuepukana na adhabu ya Siku
ya Kiyama, yasingeli pokelewa kwao; na watapata adhabu chungu.
37. Watataka watoke Motoni, lakini hawatatoka humo, na
watakuwa na adhabu inayo dumu.
38. Na mwizi mwanamume na mwizi mwanamke, ikateni mikono
yao, hayo ni malipo ya waliyo yachuma, ndiyo adhabu ya mfano itokayo kwa
Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
39. Lakini mwenye kutubia baada ya dhulma yake, na
akatengenea, basi Mwenyezi Mungu atapokea toba yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu.
40. Hujui ya kwamba Mwenyezi Mungu anao ufalme wa mbingu na
ardhi? Humuadhibu amtakaye, na humsamehe amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza
wa kila kitu.
41. Ewe
Mtume! Wasikuhuzunishe wa fanyao haraka kukufuru, miongoni mwa wanao sema kwa
vinywa vyao: Tumeamini, na hali nyoyo zao hazikuamini, na miongoni mwa
Mayahudi, wanao sikiliza kwa ajili ya uwongo, wanao sikiliza kwa ajili ya watu
wengine wasio kufikia. Wao huyabadilisha maneno kutoka pahala pake. Wanasema:
Mkipewa haya basi yashikeni, na msipo pewa haya tahadharini. Na mtu ambaye
Mwenyezi Mungu anataka kumfitini huwezi kuwa na madaraka naye mbele ya Mwenyezi
Mungu. Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu hataki kuzitakasa nyoyo zao. Watakuwa na
hizaya duniani, na Akhera watakuwa na adhabu kubwa.
42. Hao ni
wasikilizaji kwa ajili ya kusema uwongo, na ni walaji mno vya haramu! Basi
wakikujia, wahukumu baina yao au jipuuze nao. Na ukijipuuza nao, basi wao
hawatakudhuru kitu. Na ukiwahukumu, basi hukumu baina yao kwa uadilifu. Hakika
Mwenyezi Mungu anawapenda waadilifu.
43. Na
huwaje wakufanye wewe hakimu nao wanayo Taurati yenye hukumu za Mwenyezi Mungu?
Kisha baada ya hayo wanageuka. Na hao si wenye kuamini.
44. Hakika Sisi tuliteremsha Taurati yenye uwongofu na
nuru, ambayo kwayo Manabii walio nyenyekea kiislamu, na wachamngu, na
wanazuoni, waliwahukumu Mayahudi; kwani walikabidhiwa kukihifadhi Kitabu cha
Mwenyezi Mungu. Nao wakawa ni mashahidi juu yake. Basi msiwaogope watu, bali
niogopeni Mimi. Wala msibadilishe Aya zangu kwa thamani chache. Na wasio hukumu
kwa aliyo teremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri.
45. Na humo tuliwaandikia ya kwamba roho kwa roho, na jicho
kwa jicho, na pua kwa pua, na sikio kwa sikio, na jino kwa jino, na kwa
majaraha kisasi. Lakini atakaye samehe basi itakuwa ni kafara kwake. Na wasio
hukumu kwa yale aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio madhaalimu.
46. Na tukawafuatishia hao Isa bin Maryamu kuyahakikisha
yaliyo kuwa kabla yake katika Taurati, na tukampa Injili iliyomo ndani yake
uwongofu, na nuru na inayo sadikisha yaliyo kuwa kabla yake katika Taurati, na
uwongofu na mawaidha kwa wachamngu.
47. Na wahukumu Watu wa Injili kwa yale aliyo teremsha
Mwenyezi Mungu ndani yake. Na wasio hukumu kwa yale aliyo yateremsha Mwenyezi
Mungu basi hao ndio wapotofu.
48. Na tumekuteremshia wewe, kwa haki, Kitabu hichi kinacho
sadikisha yaliyo kuwa kabla yake katika Vitabu na kuyalinda. Basi hukumu baina
yao kwa aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao ukaacha
Haki iliyo kujia. Kila mmoja katika nyinyi tumemwekea sharia yake na njia yake.
Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka ange kufanyeni nyote umma mmoja, lakini
ni kukujaribuni kwa aliyo kupeni. Basi shindaneni kwa mambo ya kheri. Kwa
Mwenyezi Mungu ndio marejeo yenu nyote, na atakuja kuwaambieni yale mliyo kuwa
mkikhitalifiana.
49. Na wahukumu baina yao kwa aliyo yateremsha Mwenyezi
Mungu, wala usifuate matamanio yao. Nawe tahadhari nao wasije kukufitini
ukaacha baadhi ya aliyo kuteremshia Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka, basi jua
kwamba hakika Mwenyezi Mungu anataka kuwasibu kwa baadhi ya dhambi zao. Na
hakika wengi wa watu ni wapotofu.
50. Je, wao wanataka hukumu za Kijahiliya? Na nani aliye
mwema zaidi katika kuhukumu kuliko Mwenyezi Mungu kwa watu wenye yakini?
|