101 - 150
101. Yeye ndiye Muumbaji wa mbingu na ardhi bila ya ruwaza.
Itakuwaje awe na mwana naye hakuwa na mke? Naye ndiye aliye umba kila kitu.
Naye ni Mwenye kujua kila kitu.
102. Huyo ndiye Allah, Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu,
hapana mungu ila Yeye, Muumba wa kila kitu. Basi muabuduni Yeye tu. Naye ni Mtegemewa
wa kila kitu.
103. Macho hayamfikilii bali Yeye anayafikilia macho. Naye
ni Mjuzi, Mwenye khabari.
104. Zimekwisha kukujieni hoja wazi kutoka kwa Mola wenu
Mlezi. Basi anaye ona ni kwa faida yake mwenyewe, na anaye pofuka basi ni
khasara yake. Nami si mtunzaji wenu.
105. Na namna hivyo tunazisarifu Aya, na wao wakwambie:
Umesoma. Na ili tuyabainishe kwa watu wanao jua.
106. Fuata uliyo funuliwa kutoka kwa Mola wako Mlezi.
Hapana mungu ila Yeye. Na jitenge na washirikina.
107. Na lau Mwenyezi Mungu angeli penda, wasingeli shiriki.
Na Sisi hatukukufanya wewe uwe mtunzaji wao. Wala wewe si mlinzi juu yao.
108. Wala msiwatukane hao wanao waomba badala ya Mwenyezi
Mungu, wasije na wao wakamtukana Mwenyezi Mungu kwa jeuri bila ya kujua. Namna
hivyo tumewapambia kila umma vitendo vyao. Kisha marejeo yao yatakuwa kwa Mola
wao Mlezi, naye atawaambia waliyo kuwa wakiyatenda.
109. Na waliapa kwa Mwenyezi Mungu kwa ukomo wa viapo vyao,
kuwa ikiwafikia Ishara wataiamini. Sema: Ishara ziko kwa Mwenyezi Mungu. Na
nyinyi hamjui kuwa zitapo kuja hawato amini.
110. Nasi twazigeuza nyoyo zao na macho yao. Kama walivyo
kuwa hawakuamini mara ya kwanza, tunawaacha katika maasi yao wakitangatanga.
111. NA LAU kuwa tungeli wateremshia Malaika, na maiti
wakazungumza nao, na tukawakusanyia kila kitu mbele yao, bado wasingeli amini,
ila Mwenyezi Mungu atake. Lakini wengi wao wamo ujingani.
112. Na kadhaalika tumemfanyia kila Nabii maadui mashet'ani
wa kiwatu, na kijini, wakifundishana wao kwa wao maneno ya kupamba-pamba, kwa
udanganyifu. Na angeli penda Mola wako Mlezi wasingeli fanya hayo. Basi waache
na wanayo yazua.
113. Na ili nyoyo za wasio amini Akhera zielekee hayo, nao
wayaridhie na wayachume wanayo yachuma.
114. Je, nimtafute hakimu ghairi ya Mwenyezi Mungu, naye
ndiye aliye kuteremshieni Kitabu kilicho elezwa waziwazi? Na hao tulio wapa
Kitabu wanajua ya kwamba kimeteremshwa na Mola wako Mlezi kwa Haki. Basi usiwe
katika wanao tia shaka.
115. Na yametimia maneno ya Mola Mlezi wako kwa kweli na
uadilifu. Hapana awezaye kuyabadilisha maneno yake. Na Yeye ndiye Mwenye
kusikia na Mwenye kujua.
116. Na ukiwat'ii wengi katika hawa waliomo duniani
watakupoteza na Njia ya Mwenyezi Mungu. Hawa hawafuati ila dhana tu, na
hawakuwa ila ni wenye kusema uwongo tu.
117. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Mjuzi kushinda wote
kuwajua walio potea Njia yake, na ndiye Mjuzi kushinda wote kuwajua walio
hidika.
118. Basi kuleni katika walio somewa jina la Mwenyezi
Mungu, ikiwa mnaziamini Aya zake.
119. Na kwa nini msile katika walio somewa jina la Mwenyezi
Mungu, naye amekwisha kubainishieni alivyo kuharimishieni, isipo kuwa vile
mnavyo lazimishwa? Na hakika wengi wanapoteza kwa matamanio yao bila ya kuwa na
ilimu. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Mjuzi kushinda wote kuwajua wanao pindukia
mipaka.
120. Na acheni dhambi zilizo dhaahiri na zilizo fichikana.
Hakika wanao chuma dhambi watalipwa kwa waliyo kuwa wakiyachuma.
121. Wala msile katika wale wasio somewa jina la Mwenyezi
Mungu. Kwani huo ni upotofu. Na kwa yakini mashet'ani wanawafunza marafiki zao
kubishana nanyi. Na mkiwafuata basi hapana shaka nyinyi mtakuwa washirikina.
122. Je, aliye kuwa maiti kisha tukamhuisha, na tukamjaalia
nuru inakwenda naye mbele za watu, mfano wake ni kama aliyoko gizani akawa hata
hawezi kutoka humo? Kama hivyo makafiri wamepambiwa waliyo kuwa wakiyafanya.
123. Kadhaalika katika kila mji tumewajaalia wakubwa wa
wakosefu wao wafanye vitimbi ndani yake. Na wala hawafanyii vitimbi isipo kuwa
nafsi zao, nao hawatambui.
124. Na inapo wajia Ishara, wao husema: Hatutoamini mpaka
tupewe mfano wa walio pewa Mitume wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi
kuliko wote kujua wapi anaweka ujumbe wake. Itawafikia hao walio kosa udhalili
na adhabu kali kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu ya vitimbi walivyo kuwa
wakivifanya.
125. Basi yule ambaye Mwenyezi Mungu anataka kumhidi
humfungulia kifua chake kwa Uislamu. Na anaye taka apotee hukifanya kifua chake
kina dhiki, kimebana, kama kwamba anapanda mbinguni. Namna hivi Mwenyezi Mungu
anajaalia uchafu juu ya wasio amini.
126. Na hii ndiyo Njia ya Mola wako Mlezi Iliyo nyooka.
Tumezipambanua Aya kwa watu wanao kumbuka.
127. Hao watapata nyumba ya salama kwa Mola Mlezi wao. Naye
ndiye Rafiki Mlinzi wao kwa sababu ya waliyo kuwa wakiyatenda.
128. Na ile Siku atapo wakusanya wote awaambie: Enyi
makundi ya majini! Hakika nyinyi mmechukua wafuasi wengi katika wanaadamu. Na
marafiki zao katika wanaadamu waseme: Mola Mlezi wetu! Tulinufaishana sisi na
wao. Na tumefikia ukomo wetu ulio tuwekea. Basi Mwenyezi Mungu atasema: Moto
ndio makaazi yenu, mtadumu humo, ila apendavyo Mwenyezi Mungu. Hakika Mola wako
Mlezi ni Mwenye hikima, na Mwenye kujua.
129. Ndio kama hivi tunawaelekeza madhaalimu wapendane wao
kwa wao kwa sababu ya waliyo kuwa wakiyachuma.
130. Enyi makundi ya majini na watu! Je, hawakukujieni
Mitume kutokana na nyinyi wenyewe wakikubainishieni Aya zangu, na wakikuonyeni
mkutano wa Siku yenu hii. Nao watasema: Tumeshuhudia juu ya nafsi zetu. Na
yaliwadanganya maisha ya dunia. Nao watajishuhudia wenyewe ya kwamba walikuwa
makafiri.
131. Hayo ni kwa sababu ya kuwa Mola wako Mlezi hakuwa wa
kuiangamiza miji kwa dhulma, hali wenyewe wameghafilika.
132. Na wote wana daraja mbali mbali kutokana na yale
waliyo yatenda. Na Mola wako Mlezi si mwenye kughafilika na yale wanayo
yatenda.
133. Na Mola wako Mlezi ndiye Mkwasi, Mwenye rehema.
Akipenda atakuondoeni na awaweke wengine awapendao badala yenu, kama vile
alivyo kutoeni kutokana na uzazi wa watu wengine.
134. Bila ya shaka hayo mnayo ahidiwa yatafika tu, wala
nyinyi hamtaweza kuyaepuka.
135. Sema: Enyi watu wangu! Fanyeni muwezayo, na hakika mimi
nafanya. Mtakuja jua nani atakuwa na makaazi mema mwishoni. Hakika madhaalimu
hawatafanikiwa.
136. Na wamemwekea sehemu Mwenyezi Mungu katika mimea na
wanyama alio umba, nao husema: Hii ni sehemu ya Mwenyezi Mungu - kwa madai yao
- na hii ni ya miungu tunao washirikisha. Basi vile walivyo wakusudia miungu
yao havimfikii Mwenyezi Mungu, na vilivyo kuwa vya Mwenyezi Mungu huwafikia
miungu yao. Ni uovu kabisa hayo wanayo yahukumu.
137. Na kadhaalika hao washirika wao wamewapambia wengi
katika washirikina kuwauwa watoto wao ili kuwaangamiza na kuwavurugia dini yao.
Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli penda wasinge fanya hayo. Basi waache na hayo
wanayo yazua.
138. Nao husema: Wanyama hawa na mimea hii ni mwiko.
Hawatokula ila wale tuwapendao - kwa madai yao tu. Na wanyama hawa
imeharimishwa migongo yao kupandwa. Na wanyama wengine hawalitaji jina la
Mwenyezi Mungu juu yao. Wanamzulia uwongo tu Mwenyezi Mungu. Atawalipa kwa hayo
wanayo mzulia.
139. Na husema: Waliomo matumboni mwa wanyama hawa ni kwa
ajili ya wanaume wetu tu, na wameharimishwa kwa wake zetu. Lakini ikiwa nyamafu
basi wanashirikiana. Mwenyezi Mungu atawalipa kwa maelezo yao hayo. Hakika Yeye
ni Mwenye hikima, Mwenye kujua.
140. Hakika wamekhasirika wale ambao wamewauwa watoto wao
kwa upumbavu pasipo kujua, na wakaharimisha alivyo waruzuku Mwenyezi Mungu kwa
kumzulia Mwenyezi Mungu. Hakika wamepotea, wala hawakuwa wenye kuongoka.
141. Na Yeye ndiye aliye ziumba bustani zenye kutambaa juu
ya chanja, na zisio tambaa, na mitende, na mimea yenye matunda mbali mbali, na
mizaituni na mikomamanga inayo fanana na isiyo fanana. Kuleni matunda yake
inapo zaa, na toeni haki yake siku ya kuvunwa kwake. Wala msitumie kwa fujo.
Hakika Yeye hawapendi watumiayo kwa fujo.
142. Na katika wanyama amekujaalieni wenye kubeba mizigo na
kutoa matandiko. Kuleni katika alivyo kuruzukuni Mwenyezi Mungu, wala msifuate
nyayo za Shet'ani. Hakika yeye ni
adui yenu dhaahiri.
143.
Amekuumbieni namna nane za wanyama: Wawili katika kondoo, na wawili katika
mbuzi. Sema je, ameharimisha yote madume wawili au majike wawili, au waliomo
matumboni mwa majike yote mawili? Niambieni kwa ilimu ikiwa nyinyi mnasema
kweli.
144.Na wawili
katika ngamia, na wawili katika ng'ombe. Sema: Je, ameharimisha yote madume
wawili au majike wawili, au waliomo matumboni mwa yote majike? Au, nyinyi
mlikuwapo Mwenyezi Mungu alipo kuusieni haya? Basi ni nani dhaalimu mkubwa
kuliko yule aliye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo, kwa ajili ya kuwapoteza watu
bila ya ilimu? Hakika Mwenyezi Mungu hawahidi watu madhaalimu.
145. Sema: Sioni
katika yale niliyo funuliwa mimi kitu kilicho harimishwa kwa mlaji kukila isipo
kuwa kiwe ni nyamafu, au damu inayo mwagika, au nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni
uchafu; au kwa upotofu kimechinjwa kwa jina la asiye kuwa Mwenyezi Mungu.
Lakini mwenye kushikwa na dharura, bila ya kutamani wala kupita mipaka, basi
hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
146. Na wale
walio fuata dini ya Kiyahudi tumewaharimishia kila mwenye kucha. Na katika
ng'ombe na kondoo na mbuzi tumewaharimishia shahamu yao, isipo kuwa ile iliyo
beba migongo yao au matumbo yao, au iliyo gandamana na mifupa. Tuliwalipa hivyo
kwa sababu ya uasi wao. Na bila ya shaka Sisi ndio wasema kweli.
147. Wakikukanusha basi wewe sema: Mola Mlezi wenu ni
Mwenye rehema iliyo enea. Wala haizuiliki adhabu yake kwa watu wakhalifu.
148. Watasema walio shirikisha: Lau kuwa Mwenyezi Mungu
ange taka tusingeli shiriki sisi, wala baba zetu; wala tusingeli harimisha kitu
chochote. Vivi hivi walikanusha walio kuwa kabla yao mpaka walipo onja adhabu
yetu. Sema: Je, nyinyi mnayo ilimu mtutolee? Nyinyi hamfuati ila dhana. Wala
hamsemi ila uwongo tu.
149. Sema: Basi Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye hoja ya kukata.
Na kama angeli penda angeli kuhidini nyote.
150. Sema: Leteni mashahidi wenu watao shuhudia kuwa
Mwenyezi Mungu ameharimisha hawa. Basi wakishuhudia, wewe usishuhudie pamoja
nao. Wala usifuate matamanio ya walio zikanusha Ishara zetu, wala hawaiamini
Akhera, na ambao wanamlinganisha Mola Mlezi wao na wengine.
|