1 - 50
1. ALIF
LAM MYM 'SAAD
2. Kitabu
kilicho teremshwa kwako - basi isiwe dhiki kifuani kwako kwa ajili yake, upate
kuonya kwacho, na kiwe ni ukumbusho kwa Waumini.
3. Fuateni
mliyo teremshiwa kutoka kwa Mola Mlezi wenu, wala msifuate rafiki au walinzi
wengine badala yake. Ni machache mnayo yakumbuka.
4. Na miji
mingapi tuliiangamiza, ikaifikia adhabu yetu usiku au walipo kuwa wamelala
adhuhuri.
5. Basi
hakikuwa kilio chao ilipo wafikia adhabu yetu, isipo kuwa kusema: Hakika sisi
tulikuwa wenye kudhulumu.
6. Na kwa
yakini tutawauliza wale walio pelekewa Ujumbe, na pia tutawauliza hao Wajumbe.
7. Tena tutawasimulia kwa ilimu; wala Sisi hatukuwa mbali.
8. Na Siku hiyo kipimo kitakuwa kwa Haki. Basi watakao kuwa
na uzani mzito, hao ndio watakao fanikiwa.
9. Na watakao kuwa na uzani khafifu, basi hao ndio walio
zitia khasarani nafsi zao kwa sababu ya kuzipinga Ishara zetu.
10. Na hakika tumekuwekeni katika ardhi, na tumekujaalieni
humo njia za kupatia maisha. Ni
kuchache kushukuru kwenu.
11. Na hakika
tulikuumbeni, kisha tukakutieni sura, kisha tukawaambia Malaika: Msujudieni
Adam. Basi wakasujudu isipo kuwa Iblisi, hakuwa miongoni mwa walio sujudu.
12. Mwenyezi
Mungu akasema: Nini kilicho kuzuia kumsujudia nilipo kuamrisha? Akasema:
Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, naye umemuumba kwa udongo.
13. Akasema: Basi teremka kutoka humo! Haikufalii kufanya
kiburi humo. Basi toka! Hakika wewe u miongoni mwa walio duni.
14. Akasema: Nipe muhula mpaka siku watakapo fufuliwa.
15. Akasema: Utakuwa miongoni mwa walio pewa muhula.
16. Akasema: Kwa kuwa umenihukumia upotofu, basi
nitawavizia katika Njia yako Iliyo Nyooka.
17. Kisha nitawazukia mbele yao na nyuma yao na kuliani
kwao na kushotoni kwao. Wala hutawakuta wengi wao wenye shukrani.
18. Akasema: Toka humo, nawe umekwisha fedheheka, umekwisha
fukuzwa. Hapana shaka atakaye kufuata miongoni mwao, basi nitaijaza Jahannam
kwa nyinyi nyote.
19. Na
wewe, Adam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani hii, na kuleni humo mpendapo. Wala msiukaribie
mti huu, mkawa katika wale walio dhulumu.
20. Basi
Shet'ani aliwatia wasiwasi ili kuwafichulia tupu zao walizo fichiwa, na
akasema: Mola Mlezi wenu hakukukatazeni mti huu ila msije mkawa Malaika, au
msije mkawa katika wanao ishi milele.
21. Naye
akawaapia: Kwa yakini mimi ni miongoni wa wanao kunasihini.
22. Basi
akawateka kwa khadaa. Walipo uonja ule mti, tupu zao zilifichuka na wakaingia
kujibandika majani ya Bustanini. Mola wao Mlezi akawaita: Je, sikukukatazeni
mti huo, na kukwambieni ya kwamba Shet'ani ni adui yenu wa dhaahiri?
23.
Wakasema: Mola wetu Mlezi! tumejidhulumu nafsi zetu, na kama hutusamehe na
kuturehemu, hakika tutakuwa katika wenye kukhasirika.
24. Akasema: Teremkeni! Mtakuwa nyinyi kwa nyinyi maadui.
Na kwenye ardhi itakuwa ndio makao yenu na starehe yenu mpaka ufike muda.
25. Akasema: Humo mtaishi, na humo mtakufa, na kutoka humo
mtatolewa.
26. Enyi
wanaadamu! Tumekuteremshieni nguo za kuficha tupu zenu, na nguo za pambo. Na
nguo za uchamngu ndio bora. Hayo ni katika Ishara za Mwenyezi Mungu mpate
kukumbuka.
27. Eny
wanaadamu! Asije Shet'ani kukufitinini kama alivyo watoa wazazi wenu Peponi,
akawavua nguo zao kuwaonyesha tupu zao. Hakika yeye na kabila yake wanakuoneni,
na nyinyi hamuwaoni. Hakika Sisi tumewafanya Mashet'ani kuwa ni marafiki wa
wasio amini.
28. Na
wanapo fanya mambo machafu husema: Tumewakuta nayo baba zetu, na Mwenyezi Mungu
ametuamrisha hayo. Sema: Hakika Mwenyezi Mungu haamrishi mambo machafu.
Mnamzulia Mwenyezi Mungu msiyo yajua?
29. Sema:
Mola Mlezi wangu ameamrisha uadilifu, na mumuelekeze nyuso zenu kila mnapo
sujudu, na muombeni Yeye kwa kumsafia Dini. Kama alivyo kuumbeni mwanzo ndivyo
mtavyo rudi,
30. Hali
ya kuwa kundi moja amelihidi, na kundi jengine limethibitikiwa na upotofu. Kwa
hakika hao waliwafanya mashet'ani kuwa ndio marafiki walinzi badala ya Mwenyezi
Mungu, na wanadhani kuwa wao wameongoka.
31. Enyi
wanaadamu! Chukueni pambo lenu kwenye kila pahala wakati wa ibada, na kuleni,
na kunyweni na wala msifanye ubadhirifu. Kwa hakika Yeye hapendi wanao fanya
israfu.
32. Sema:
Ni nani aliye harimisha pambo la Mwenyezi Mungu alilo watolea waja wake, na
vilivyo vizuri katika riziki. Sema hivyo ni kwa walio amini katika uhai wa
duniani, na Siku ya Kiyama vitakuwa vyao wao tu. Namna hivi tunazieleza Ishara
kwa watu wanao jua.
33. Sema:
Mola Mlezi wangu ameharimisha mambo machafu ya dhaahiri na ya siri, na dhambi, na
uasi bila ya haki, na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na asicho kiletea
uthibitisho, na kumzulia Mwenyezi Mungu msiyo yajua.
34. Na kila umma una muda wake. Utakapo fika muda wao basi
hawatakawia hata saa moja, wala hawatatangulia.
35. Enyi
wanaadamu! Watakapo kufikieni Mitume miongoni mwenu wakakuelezeni Ishara zangu,
basi watakao mchamngu na wakatengenea haitakuwa khofu kwao, wala
hawatahuzunika.
36. Na wale
watakao kanusha Ishara zetu na wakazifanyia kiburi, hao ni watu wa Motoni; humo
watadumu.
37. Basi
ni nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo, au
anaye zikanusha Ishara zake? Hao itawafikia sehemu yao waliyo andikiwa, mpaka
watakapo wafikia wajumbe wetu kuwafisha, watawaambia: Wako wapi mlio kuwa
mkiwaomba badala ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Wametupotea! Na watajishuhudia
wenyewe kwamba walikuwa makafiri.
38.
Mwenyezi Mungu atasema: Ingieni Motoni pamoja na umma zilizo pita kabla yenu za
majini na watu. Kila utakapo ingia umma utawalaani wenzake. Mpaka
watakapo kusanyika wote humo, wa mwisho wao watawasema wa mwanzo wao: Mola wetu
Mlezi! Hawa ndio walio tupoteza; basi wape adhabu ya Motoni marudufu. Atasema:
Itakuwa kwenu nyote marudufu, lakini nyinyi hamjui tu.
39. Na wa mwanzo wao watawaambia wa mwisho wao: Basi nyinyi
pia hamkuwa na ubora kuliko sisi. Basi onjeni adhabu kwa sababu ya mliyo kuwa
mkiyachuma.
40. Hakika wale wanao zikanusha Ishara zetu na wakazifanyia
kiburi hawatafunguliwa milango ya mbingu, wala hawataingia Peponi mpaka apite
ngamia katika tundu ya sindano. Na hivi ndivyo tunavyo walipa wakosefu.
41. Jahannamu itakuwa kitanda chao na juu yao nguo za moto
za kujifunika. Na hivi ndivyo tunavyo walipa madhaalimu.
42. Na wale wanao amini na wakatenda mema - hatumkalifishi
mtu yoyote ila kwa kiasi cha uwezo wake - hao ndio watu wa Peponi. Wao watadumu humo.
43. Na
tutaondoa chuki vifuani mwao, na mbele yao iwe inapita mito. Na watasema:
Alhamdulillah! Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu, ambaye aliye tuhidi kufikia
haya. Wala hatukuwa wenye kuhidika wenyewe ingeli kuwa Mwenyezi Mungu
hakutuhidi. Hakika Mitume wa Mola wetu Mlezi walileta Haki. Na watanadiwa
kwamba: Hiyo ndiyo Pepo mliyo rithishwa kwa sababu ya mliyo kuwa mkiyafanya.
44. Na
watu wa Peponi watawanadia watu wa Motoni: Sisi tumekuta aliyo tuahidi Mola
wetu Mlezi kuwa ni kweli. Je, na nyinyi pia mmekuta aliyo kuahidini Mola wenu
Mlezi kuwa ni kweli? Watasema: Ndiyo! Basi mtangazaji atawatangazia: Laana ya
Mwenyezi Mungu iwapate walio dhulumu,
45. Wale
ambao walikuwa wakizuilia Njia ya Mwenyezi Mungu, na wakataka kuipotosha, nao
wanaikanusha Akhera.
46. Na baina ya makundi mawili hayo patakuwapo pazia. Na
juu ya Mnyanyuko patakuwa watu watakao wajua wote kwa alama zao, na wao
watawaita watu wa Peponi: Assalamu Alaykum, Amani juu yenu! Wao bado
hawajaingia humo, lakini wanatumai.
47. Na yanapo geuzwa macho yao kuelekea watu wa Motoni,
watasema: Mola Mlezi wetu! Usitujaalie kuwa pamoja na watu walio dhulumu.
48. Na hao watu wa Mnyanyukoni watawaita watu wanao wajua
kwa alama zao. Watasema: Kujumuika kwenu hakukufaini kitu, wala hicho mlicho
kuwa mnafanyia kiburi.
49. Je, hawa sio wale mlio kuwa mkiwaapia kuwa Mwenyezi
Mungu hatawafikishia rehema. Ingieni Peponi, hapana khofu kwenu, wala
hamtahuzunika!
50. Na watu wa Motoni watawaita watu wa Peponi: Tumimieni
maji, au chochote alicho kuruzukuni Mwenyezi Mungu. Nao watasema: Hakika
Mwenyezi Mungu ameviharimisha hivyo kwa makafiri,
|