101 - 150
101. Miji hiyo, tunakusimulia baadhi ya khabari zake. Na
hapana shaka Mitume wao waliwafikia kwa hoja zilizo waziwazi. Lakini hawakuwa
wenye kuamini waliyo yakanusha zamani. Namna hivi Mwenyezi Mungu anazipiga
muhuri nyoyo za makafiri.
102. Wala hatukuwaona wengi wao kuwa wanatimiza ahadi; bali
kwa hakika tuliwakuta wengi wao ni wapotofu.
103. Kisha baada yao tukamtuma Musa na Ishara zetu kwa
Firauni na waheshimiwa wake. Nao wakazikataa. Basi tazama ulikuwaje mwisho wa
waharibifu.
104. Na Musa alisema: Ewe Firauni! Hakika mimi ni Mtume
nitokaye kwa Mola Mlezi wa viumbe vyote.
105. Inafaa nisiseme juu ya Mwenyezi Mungu ila lilio la
Haki. Nami hakika nimekujieni na dalili waziwazi kutokana na Mola Mlezi wenu. Basi waache Wana wa Israili wende nami.
106. Akasema
Firauni: Ikiwa umekuja na Ishara, basi ilete ukiwa ni katika wasemao kweli.
107. Basi
akaitupa fimbo yake, na mara ikawa nyoka dhaahiri.
108. Na akatoa
mkono wake, mara ukawa mweupe kwa watazamao.
109. Wakasema
waheshimiwa wa kaumu ya Firauni: Hakika huyo ni mchawi mjuzi.
110. Anataka
kukutoeni katika nchi yenu. Basi mnatoa shauri gani?
111. Wakasema: Mwache kidogo yeye na nduguye, na watume
mijini wakusanyao,
112. Wakuletee kila mchawi mjuzi.
113. Wakaja wachawi kwa Firauni, wakasema: Hakika tutapata
ujira ikiwa tutashinda.
114. Akasema: Naam! Nanyi bila ya shaka mtakuwa katika wa
karibu nami.
115. Wakasema: Ewe Musa! Je, utatupa wewe, au tutakuwa sisi
tutao tupa?
116. Akasema: Tupeni! Basi walipo tupa waliyazuga macho ya
watu na wakawatia khofu, na wakaleta uchawi mkubwa.
117. Nasi tukamfunulia Musa kumwambia: Tupa fimbo yako.
Mara ikavimeza vyote vile walivyo vibuni.
118. Kweli ikathibiti na yakabat'ilika waliyo kuwa
wakiyatenda.
119. Kwa hivyo walishindwa hapo, na wakageuka kuwa wadogo.
120. Na wachawi wakapoomoka wakisujudu.
121. Wakasema: Tumemuamini Mola Mlezi wa viumbe vyote,
122. Mola Mlezi wa Musa na Haarun.
123. Akasema Firauni: Mmemuamini kabla sijakupeni idhini?
Hizi ni njama mlizo panga mjini mpate kuwatoa wenyewe. Lakini karibu mtajua!
124. Lazima nitaikata mikono yenu na miguu yenu mbali
mbali. Kisha nitakutundikeni misalabani.
125. Wakasema: Sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi.
126. Nawe hukuudhika nasi ila kwa kuwa tumeziamini Ishara
za Mola Mlezi wetu zilipo tujia. Ewe Mola Mlezi wetu! Tumiminie uvumilivu na
utufishe hali ni Waislamu.
127. Wakasema waheshimiwa wa kaumu ya Firauni: Unamuacha
Musa na watu wake walete uharibifu katika nchi na wakuache wewe na miungu yako?
Akasema: Tutawauwa wavulana wao, na tutawaacha hai wanawake wao. Na bila ya
shaka sisi ni wenye nguvu juu yao.
128. Musa akawaambia watu wake: Ombeni msaada kwa Mwenyezi
Mungu, na subirini. Hakika ardhi ni ya Mwenyezi Mungu. Naye humrithisha
amtakaye katika waja wake. Na mwisho ni wa wachamngu.
129. Wakasema: Tumeudhiwa kabla hujatufikia, na baada ya
wewe kutujia! Musa akasema: Huenda Mola wenu Mlezi akamhiliki adui wenu, na
akakufanyeni nyinyi ndio wa kufuatia kushika nchi, ili atazame mtavyo kuja
tenda nyinyi.
130. Na hakika tuliwaadhibu watu wa Firauni kwa miyaka (ya
ukame) na kwa upungufu wa mazao, ili wapate kukumbuka.
131. Likiwafika jema wakisema: Haya ni haki yetu. Na
likiwafika ovu husema: Musa na walio pamoja naye ni wakorofi. Hakika ukorofi
wao huo unao wafikia unatoka kwa Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui.
132. Na
wakisema: Hata ukituletea Ishara yoyote kutuzuga hatuto kuamini.
133. Basi
tukawapelekea tufani, na nzige, na chawa, na vyura, na damu, kuwa ni Ishara
mbali mbali. Nao wakapanda kiburi, na wakawa watu wakosefu.
134. Na
ilipo waangukia adhabu wakasema: Ewe Musa! Tuombee kwa Mola wako Mlezi kwa
aliyo kuahidi. Ukituondolea adhabu hii hapana shaka tutakuamini, na
tutawaachilia Wana wa Israili wende nawe.
135.
Lakini tukiwaondolea adhabu mpaka muda fulani wao waufikie, mara wakivunja
ahadi yao.
136. Basi
tuliwapatiliza, tuka- wazamisha baharini kwa sababu walizikanusha Ishara zetu,
na wakaghafilika nazo.
137. Na
tukawarithisha watu walio kuwa wanadharauliwa mashariki na magharibi ya ardhi
tuliyo ibariki. Na likatimia neno jema la Mola Mlezi wako juu ya Wana wa
Israili, kwa vile walivyo subiri. Na tukayaangamiza aliyo kuwa akiyafanya
Firauni na kaumu yake, na waliyo kuwa wakiyajenga.
138. Na
tukawavusha bahari Wana wa Israili, wakafika kwa watu wanao abudu masanamu yao.
Wakasema: Ewe Musa! Hebu
tufanyie na sisi miungu kama hawa walivyo kuwa na miungu. Musa akasema: Hakika
nyinyi ni watu msio jua kitu.
139. Hakika haya
waliyo nayo watu hawa yatakuja angamia, na hayo waliyo kuwa wakiyafanya
yamepotea bure.
140. Akasema:
Je, nikutafutieni mungu asiye kuwa Mwenyezi Mungu, na Yeye ndiye aliye
kufadhilisheni juu ya viumbe vyote?
141. Na pale tulipo
kuokoeni kwa watu wa Firauni walio kupeni adhabu za mwisho wa uovu. Wakiwauwa
wavulana wenu, na wakawaacha hai wanawake wenu. Na katika hayo yalikuwa
majaribio makubwa kutokana na Mola wenu Mlezi.
142. Tulimuahidi
Musa masiku thalathini na tukayatimiza kwa kumi; ikatimia miadi ya Mola wake
Mlezi masiku arubaini. Na Musa akamwambia nduguye Haarun: Shika mahala pangu
kwa watu wangu na utengeneze wala usifuate njia ya waharibifu.
143. Na alipo
kuja Musa kwenye miadi yetu, na Mola wake Mlezi akamsemeza, alisema: Mola wangu
Mlezi! Nionyeshe nikutazame. Mwenyezi Mungu akasema: Hutoniona. Lakini
utazame huo mlima. Ukibaki pahala pake basi utaniona. Basi alipo jionyesha Mola
Mlezi wake kwa mlima, aliufanya uvurugike, na Musa akaanguka chini amezimia.
Alipo zindukana alisema: Subhanaka, Umetakasika! Natubu kwako, na mimi ni wa
kwanza wa Waumini.
144. (Mwenyezi Mungu) akasema: Ewe Musa! Mimi nimekuteuwa
wende kwa watu na Ujumbe wangu na maneno yangu. Basi chukua niliyo kupa na uwe
katika wanao shukuru.
145. Na tukamuandikia katika mbao kila kitu, mawaidha na maelezo
ya mambo yote. (Tukamwambia): Basi yashike kwa nguvu na uwaamrishe watu wako
wayashike kwa ubora wake. Nami nitakuonyesheni makaazi ya wapotofu.
146. Nitawatenga na Ishara zangu wale wanao fanya kiburi
katika nchi bila ya haki. Na wao wakiona kila Ishara hawaiamini. Wakiiona njia
ya uwongofu hawaishiki kuwa ndiyo njia; lakini wakiiona njia ya upotofu
wanaishika kuwa ndiyo njia. Hayo ni kwa sababu wamezikanusha Ishara zetu, na
wameghafilika nazo.
147. Na walio zikanusha Ishara zetu na mkutano wa Akhera
a'mali zao zimeharibika. Kwani watalipwa ila kwa yale waliyo kuwa wakiyatenda?
148. Na baada yake walimfanya ndama kutokana na mapambo yao
(kumuabudu), kiwiliwili tu kilicho kuwa na sauti. Hivyo, hawakuona kuwa hawasemezi
wala hawaongoi njia? Wakamuabudu, na wakawa wenye kudhulumu.
149. Na walipo juta na wakaona ya kwamba wamekwisha potea,
walisema: Ikiwa Mola wetu Mlezi hakuturehemu na akatusamehe, bila ya shaka
tutakuwa miongoni mwa walio khasiri.
150. Na alipo rudi Musa kwa watu wake, naye amekasirika na
kuhuzunika, alisema: Ni maovu yalioje mlio nifanyia nyuma yangu! Je,
mmeitangulia amri ya Mola wenu Mlezi? Na akaziweka chini zile mbao, na
akamkamata kichwa ndugu yake akimvutia kwake. (Haarun) akasema: Ewe mwana wa
mama yangu! Hakika hawa watu wamenidharau, na wakakaribia kuniuwa. Basi
usiwafurahishe maadui juu yangu, wala usinifanye pamoja na watu madhaalimu.
|