Matthew
Chapter 1
1 Yesu
Kristo alikuwa mzawa wa Daudi, mzawa wa Abrahamu. Hii ndiyo orodha ya ukoo
wake:
2 Abrahamu
alimzaa Isaka, Isaka alimzaa Yakobo, Yakobo alimzaa Yuda na ndugu zake,
3 Yuda
alimzaa Faresi na Zera (mama yao alikuwa Tamari), Faresi alimzaa
Hesroni, Hesroni alimzaa Rami,
4 Rami
alimzaa Aminadabu, Aminadabu alimzaa Nashoni, Nashoni alimzaa Salmoni,
5 Salmoni
alimzaa Boazi (mama yake Boazi alikuwa Rahabu). Boazi na Ruthi walikuwa wazazi
wa Obedi, Obedi alimzaa Yese,
6 naye
Yese alimzaa Mfalme Daudi. Daudi alimzaa Solomoni (mama yake Solomoni alikuwa
mke wa Uria).
7 Solomoni
alimzaa Rehoboamu, Rehoboamu alimzaa Abiya, Abiya alimzaa Asa,
8 Asa
alimzaa Yehoshafati, Yehoshafati alimzaa Yoramu, Yoramu alimzaa Uzia,
9 Uzia
alimzaa Yothamu, Yothamu alimzaa Ahazi, Ahazi alimzaa Hezekia,
10 Hezekia alimzaa Manase, Manase alimzaa Amoni, Amoni
alimzaa Yosia,
11 Yosia
alimzaa Yekonia na ndugu zake. Huo ulikuwa wakati Wayahudi walipopelekwa
uhamishoni Babuloni.
12 Baada
ya Wayahudi kupelekwa uhamishomi Babuloni: Yekonia alimzaa Shealtieli,
Shealtieli alimzaa Zerobabeli,
13
Zerobabeli alimzaa Abiudi, Abiudi alimzaa Eliakimu, Eliakimu alimzaa Azori,
14 Azori
alimzaa Zadoki, Zadoki alimzaa Akimu, Akimu alimzaa Eliudi,
15 Eliudi
alimzaa Eleazeri, Eleazeri alimzaa Mathani, Mathani alimzaa Yakobo,
16 Yakobo
alimzaa Yosefu, aliyekuwa mume wake Maria, mama yake Yesu, aitwaye Kristo.
17 Basi,
kulikuwa na vizazi kumi na vinne tangu Abrahamu mpaka Daudi, vizazi kumi na
vinne tangu Daudi mpaka Wayahudi walipochukuliwa mateka Babuloni, na vizazi
kumi na vinne tangu kuchukuliwa mateka mpaka wakati wa Kristo.
18 Basi,
hivi ndivyo Yesu Kristo alivyozaliwa: Maria, mama yake, alikuwa ameposwa na
Yosefu. Lakini kabla hawajakaa pamoja kama mume na mke, alionekana kuwa mja
mzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
19 Yosefu,
mumewe, kwa vile alikuwa mwadilifu, hakutaka kumwaibisha hadharani; hivyo
alikusudia kumwacha kwa siri.
20
Alipokuwa bado anawaza jambo hilo, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto,
akamwambia, "Yosefu, mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke
wako, maana amekuwa mja mzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
21
Atajifungua mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu, kwa kuwa yeye atawaokoa watu
wake kutoka katika dhambi zao."
22 Basi,
haya yote yalitukia ili litimie lile neno Bwana alilosema kwa njia ya nabii:
23
"Bikira atachukua mimba, atamzaa mtoto wa kiume, naye ataitwa
Emanueli" (maana yake, "Mungu yu pamoja nasi").
24 Hivyo,
Yosefu alipoamka usingizini alifanya kama malaika huyo alivyomwambia,
akamchukua mke wake nyumbani.
25 Lakini
hakumjua kamwe kimwili hata Maria alipojifungua mtoto wa kiume. Naye Yosefu
akampa jina Yesu.
|