Chapter 8
1 Wakati huo umati mkubwa wa watu ulikusanyika tena, na
hawakuwa na chakula. Basi, Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia,
2 "Nawahurumia watu hawa kwa sababu wamekuwa nami kwa
muda wa siku tatu, wala hawana chakula.
3 Nikiwaacha waende nyumbani wakiwa na njaa watazimia
njiani, maana baadhi yao wametoka mbali."
4 Wanafunzi wake wakamwuliza, "Hapa nyikani
itapatikana wapi mikate ya kuwashibisha watu hawa wote?"
5 Yesu
akawauliza, "Mnayo mikate mingapi?" Nao wakamjibu, "Saba."
6 Basi,
akawaamuru watu wakae chini. Akaitwaa ile mikate saba, akamshukuru Mungu,
akaimega, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu, nao wakawagawia.
7 Walikuwa
pia na visamaki vichache. Yesu akavibariki, akaamuru vigawiwe watu vilevile.
8 Watu
wakala, wakashiba. Wakaokota mabaki yaliyosalia wakajaza makapu saba.
9 Nao
waliokula walikuwa watu wapatao elfu nne. Yesu akawaaga,
10 na mara
akapanda mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda wilaya ya Dalmanutha.
11
Mafarisayo walikuja, wakaanza kujadiliana na Yesu. Kwa kumjaribu, wakamtaka
awafanyie ishara kuonyesha anayo idhini kutoka mbinguni.
12 Yesu
akahuzunika rohoni, akasema, "Mbona kizazi hiki kinataka ishara? Kweli
nawaambieni, kizazi hiki hakitapewa ishara yoyote!"
13 Basi,
akawaacha, akapanda tena mashua, akaanza safari kwenda ng`ambo ya pili ya ziwa.
14
Wanafunzi walikuwa wamesahau kuchukua mikate; walikuwa na mkate mmoja tu katika
mashua.
15 Yesu akawaonya, "Angalieni sana! Jihadharini na
chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode."
16 Wanafunzi wakaanza kujadiliana wao kwa wao,
"Anasema hivyo kwa kuwa hatuna mikate."
17 Yesu alitambua hayo, akawaambia, "Mbona
mnajadiliana juu ya kutokuwa na mikate? Je, bado hamjafahamu, wala hamjaelewa?
Je, mioyo yenu imeshupaa?
18 Je, Mnayo macho na hamwoni? Mnayo masikio na hamsikii?
Je, hamkumbuki
19 wakati ule nilipoimega ile mikate mitano na kuwapa watu
elfu tano? Mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki ya makombo?" Wakamjibu,
"Kumi na viwili."
20 "Na nilipoimega ile mikate saba na kuwapa watu elfu
nne, mlikusanya makapu mangapi ya makombo?" Wakamjibu, "Saba."
21 Basi,
akawaambia, "Na bado hamjaelewa?"
22 Yesu
alifika Bethsaida pamoja na wanafunzi wake. Huko watu wakamletea kipofu mmoja,
wakamwomba amguse.
23 Yesu
akamshika mkono huyo kipofu, akampeleka nje ya kijiji. Akamtemea mate machoni,
akamwekea mikono, akamwuliza, "Je, unaweza kuona kitu?"
24 Huyo
kipofu akatazama, akasema, "Ninawaona watu wanaoonekana kama miti
inayotembea."
25 Kisha
Yesu akamwekea tena mikono machoni, naye akakaza macho, uwezo wake wa kuona
ukamrudia, akaona kila kitu sawasawa.
26 Yesu
akamwambia aende zake nyumbani na kumwamuru, "Usirudi kijijini!"
27 Kisha
Yesu na wanafunzi wake walikwenda katika vijiji vya Kaisarea Filipi. Walipokuwa
njiani, Yesu aliwauliza wanafunzi wake, "Watu wanasema mimi ni nani?"
28
Wakamjibu, "Wengine wanasema wewe ni Yohane Mbatizaji, wengine Eliya na
wengine mmojawapo wa manabii."
29 Naye
akawauliza, "Na ninyi je, mnasema mimi ni nani?" Petro akamjibu,
"Wewe ndiwe Kristo."
30 Kisha
Yesu akawaonya wasimwambie mtu yeyote habari zake.
31 Yesu
alianza kuwafundisha wanafunzi wake: "Ni lazima Mwana wa Mtu apatwe na
mateso mengi na kukataliwa na wazee na makuhani wakuu na walimu wa Sheria.
Atauawa na baada ya siku tatu atafufuka."
32 Yesu
aliwaambia jambo hilo waziwazi. Basi, Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea.
33 Lakini
Yesu akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro akisema,
"Ondoka mbele yangu, Shetani! Fikira zako si za kimungu ila ni za
kibinadamu!"
34 Kisha
akauita umati wa watu pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, "Mtu yeyote
akitaka kuwa mfuasi wangu, lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake,
anifuate.
35 Maana
mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza, lakini mtu
atakayepoteza maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Habari Njema,
atayaokoa.
36 Je,
kuna faida gani mtu kuupata ulimwengu wote na kuyapoteza maisha yake?
37 Ama mtu
atatoa kitu gani badala ya maisha yake?
38 Mtu
yeyote katika kizazi hiki kiovu na kisichomjali Mungu anayenionea aibu mimi na
mafundisho yangu, Mwana wa Mtu atamwonea aibu mtu huyo wakati atakapokuja
katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu."
|