Chapter 10
1 Yesu
alitoka hapo akaenda mkoani Yudea na hata ng`ambo ya mto Yordani. Umati wa watu
ukamwendea tena, naye akawafundisha tena kama ilivyokuwa desturi yake.
2 Basi,
Mafarisayo wakamwendea, na kwa kumjaribu wakamwuliza, "Je, ni halali mtu
kumpa talaka mkewe?"
3 Yesu
akawajibu, "Mose aliwapa maagizo gani?"
4 Nao
wakasema, "Mose aliagiza mume kumpatia mkewe hati ya talaka na
kumwacha."
5 Yesu
akawaambia, "Mose aliwaandikia amri hiyo kwa sababu ya ugumu wa mioyo
yenu.
6 Lakini
tangu kuumbwa ulimwengu, Mungu aliumba mwanamume na mwanamke.
7 Hivyo
mwanamume atawaacha baba yake na mama yake, ataungana na mkewe,
8 nao
wawili watakuwa mwili mmoja. Kwa hiyo, wao si wawili tena bali mwili mmoja.
9 Basi,
alichounganisha Mungu, binadamu asitenganishe."
10
Walipoingia tena ndani ya nyumba, wanafunzi wake walimwuliza juu ya jambo hilo.
11 Naye
akawaambia, "Anayemwacha mkewe na kuoa mwingine, anazini dhidi ya mkewe.
12 Na
mwanamke anayemwacha mumewe na kuolewa na mwingine anazini."
13 Watu
walimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse, lakini wanafunzi wakawakemea.
14 Yesu
alipoona hivyo, alikasirika akawaambia, "Waacheni hao watoto waje kwangu,
wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu walio kama
watoto hawa.
15
Nawaambieni kweli, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo
hataingia katika Ufalme huo."
16 Kisha
akawapokea watoto hao, akawawekea mikono, akawabariki.
17 Yesu
alipoanza tena safari yake, mtu mmoja alimjia mbio, akapiga magoti mbele yake,
akamwuliza, "Mwalimu mwema, nifanyeje ili niupate uzima wa milele?"
18 Yesu
akamjibu, "Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila Mungu peke yake.
19 Unazijua
amri: `Usizini; Usiue; Usiibe; Usitoe ushahidi wa uongo; Usidanganye; Waheshimu
baba na mama yako."`
20 Naye
akamjibu, "Mwalimu, hayo yote nimeyazingatia tangu ujana wangu."
21 Yesu
akamtazama, akampenda, akamwambia, "Umepungukiwa na kitu kimoja: nenda
ukauze vitu ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha
njoo unifuate."
22
Aliposikia hayo, alisikitika, akaenda zake akiwa na huzuni, kwa maana alikuwa
na mali nyingi.
23 Yesu
akatazama pande zote, akawaambia wanafunzi wake, "Jinsi gani itakavyokuwa
vigumu kwa matajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu!"
24
Wanafunzi walishangazwa na maneno yake. Yesu akawaambia tena, "Watoto
wangu, ni vigumu sana kuingia katika Ufalme wa Mungu!
25 Ni
rahisi zaidi ngamia kupenya katika tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia
katika Ufalme wa Mungu."
26
Wanafunzi wake wakashangaa sana wakaulizana, "Ni nani basi, atakayeweza
kuokoka?"
27 Yesu
akawatazama, akawaambia, "Kwa binadamu haiwezekani, lakini kwa Mungu si
hivyo, maana kwa Mungu mambo yote huwezekana."
28 Petro
akamwambia, "Na sisi je? Tumeacha yote, tukakufuata!"
29 Yesu akasema,
"Kweli nawaambieni, kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu, au dada, au mama,
au baba, au watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Habari Njema,
30
atapokea mara mia zaidi wakati huu wa sasa nyumba, ndugu, dada, mama, watoto na
mashamba pamoja na mateso; na katika wakati ujao atapokea uzima wa milele.
31 Lakini
wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa
kwanza."
32 Basi,
walikuwa njiani kwenda Yerusalemu, na Yesu alikuwa anawatangulia. Wanafunzi
wake walijawa na hofu, na watu waliofuata waliogopa. Yesu akawachukua tena
kando wale kumi na wawili, akaanza kuwaambia yale yatakayompata:
33
"Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu, na huko Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa
makuhani wakuu na walimu wa Sheria, nao watamhukumu auawe na kumkabidhi kwa
watu wa mataifa.
34 Nao
watamdhihaki; watamtemea mate, watampiga mijeledi na kumwua. Na baada ya siku
tatu atafufuka."
35 Yakobo
na Yohane, wana wa Zebedayo, walimwendea Yesu wakamwambia, "Mwalimu,
tunataka utufanyie kitu tutakachokuomba."
36 Yesu
akawauliza, "Mnataka niwafanyie nini?"
37
Wakamjibu, "Uturuhusu tuketi mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande
wako wa kushoto katika utukufu wa Ufalme wako."
38 Yesu
akawaambia, "Hamjui mnachoomba! Je, mnaweza kunywa kikombe
nitakachokunywa, au kubatizwa kama nitakavyobatizwa?"
39
Wakamjibu, "Tunaweza." Yesu akawaambia, "Kikombe nitakachokunywa
mtakinywa kweli, na mtabatizwa kama nitakavyobatizwa.
40 Lakini
ni nani atakayeketi kulia au kushoto kwangu si wajibu wangu kupanga, bali
nafasi hizo watapewa wale waliotayarishiwa."
41 Wale
wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, walianza kuchukizwa na Yakobo na
Yohane.
42 Yesu
akawaita, akawaambia, "Mnajua kwamba wale wanaofikiriwa kuwa watawala wa
mataifa huwatawala watu wao kwa mabavu, na wakuu hao huwamiliki watu wao.
43 Lakini
kwenu isiwe hivyo, ila anayetaka kuwa mkuu kati yenu, sharti awe mtumishi wenu.
44
Anayetaka kuwa wa kwanza, sharti awe mtumishi wa wote.
45 Maana
Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, ila alikuja kutumikia, na kutoa maisha yake
kuwa fidia ya watu wengi."
46 Basi,
wakafika Yeriko, naye Yesu alipokuwa anatoka katika mji huo akiwa na wanafunzi
wake pamoja na umati mkubwa wa watu, kipofu mwombaji aitwaye Bartimayo mwana wa
Timayo alikuwa ameketi kando ya barabara.
47
Aliposikia kwamba ni Yesu wa Nazareti aliyekuwa anapita mahali hapo, alianza
kupaaza sauti, "Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!"
48 Watu
wengi walimkemea ili anyamaze, lakini yeye akazidi kupaaza sauti, "Mwana
wa Daudi, nihurumie!"
49 Yesu
alisimama, akasema, "Mwiteni." Basi, wakamwita huyo kipofu,
wakamwambia, "Jipe moyo! Simama, anakuita."
50 Naye
akatupilia mbali vazi lake, akaruka juu, akamwendea Yesu.
51 Yesu
akamwuliza, "Unataka nikufanyie nini?" Huyo kipofu akamwambia,
"Mwalimu, naomba nipate kuona."
52 Yesu
akamwambia, "Nenda, imani yako imekuponya." Mara huyo kipofu akaweza
kuona, akamfuata Yesu njiani.
|