Chapter 13
1 Yesu alipokuwa anatoka Hekaluni, mmoja wa wanafunzi wake
alimwambia, "Mwalimu, tazama jinsi mawe haya na majengo haya yalivyo ya
ajabu!"
2 Yesu akamwambia, "Je, unayaona majengo haya makubwa?
Hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu
kitabomolewa."
3 Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni
akielekea Hekalu, Petro, Yakobo, Yohane na Andrea wakamwuliza kwa faragha,
4 "Twambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani
itakayoonyesha kwamba mambo haya karibu yatimizwe?"
5 Yesu akaanza kuwaambia, "Jihadharini msije
mkadanganywa na mtu.
6 Maana wengi watakuja wakilitumia jina langu, wakisema,
`Mimi ndiye!` nao watawapotosha watu wengi.
7 Mtakaposikia juu ya vita na fununu za vita, msifadhaike.
Mambo hayo lazima yatokee, lakini mwisho wenyewe ungali bado.
8 Taifa moja litapigana na taifa lingine; utawala mmoja
utapigana na utawala mwingine; kila mahali kutakuwa na mitetemeko ya ardhi na
njaa. Mambo haya ni kama tu maumivu ya kwanza ya kujifungua mtoto.
9 "Lakini ninyi jihadharini. Maana watu watawapelekeni
mahakamani, na kuwapigeni katika masunagogi. Mtapelekwa mbele ya watawala na
wafalme kwa sababu yangu ili mpate kunishuhudia kwao.
10 Lakini lazima kwanza Habari Njema ihubiriwe kwa mataifa
yote.
11 Nao watakapowatieni nguvuni na kuwapeleka mahakamani,
msiwe na wasiwasi juu ya yale mtakayosema; saa ile itakapofika, semeni chochote
mtakachopewa, maana si ninyi mtakaosema, bali Roho Mtakatifu.
12 Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe; baba atamsaliti
mwanae; watoto watawashambulia wazazi wao na kuwaua.
13 Watu wote watawachukieni ninyi kwa sababu ya jina langu.
Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa.
14 "Mtakapoona `Chukizo Haribifu` limesimama mahali
ambapo si pake, (msomaji na atambue maana yake!) Hapo watu walioko Yudea
wakimbilie milimani.
15 Mtu aliye juu ya paa la nyumba asishuke kuingia nyumbani
mwake kuchukua kitu.
16 Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake.
17 Ole wao waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo!
18 Ombeni ili mambo hayo yasitukie nyakati za baridi.
19 Maana wakati huo kutakuwa na dhiki ambayo haijatokea
tangu Mungu alipoumba ulimwengu mpaka leo, wala haitatokea tena.
20 Kama Bwana asingepunguza siku hizo, hakuna binadamu
ambaye angeokolewa. Lakini kwa ajili ya wateule wake, Bwana amezipunguza siku
hizo.
21 "Basi mtu akiwaambieni, `Tazama, Kristo yupo hapa!`
au `Yupo pale!` msimsadiki.
22 Maana watatokea kina Kristo wa uongo na manabii wa
uongo, watafanya ishara na maajabu, ili kuwapotosha wateule wa Mungu, kama
ikiwezekana.
23 Lakini ninyi jihadharini. Mimi nimewaambieni mambo yote
kabla hayajatokea.
24 "Basi, siku hizo baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa
giza na mwezi hautaangaza.
25 Nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu
zitatikiswa.
26 Hapo watamwona Mwana wa Mtu akija katika mawingu kwa
nguvu nyingi na utukufu.
27 Kisha atawatuma malaika wake; atawakusanya wateule wake
kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho wa dunia mpaka mwisho wa mbingu.
28 "Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake
yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa kiangazi
umekaribia.
29 Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo hayo yakitendeka,
jueni kwamba Mwana wa Mtu yuko karibu sana.
30 Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo
hayo yote kutukia.
31 Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita
kamwe.
32 "Lakini hakuna mtu ajuaye siku au saa hiyo itakuja
lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana; Baba peke yake ndiye ajuaye.
33 Muwe waangalifu na kesheni, maana hamjui wakati huo
utafika lini.
34 Itakuwa kama mtu anayeondoka nyumbani kwenda safari
akiwaachia watumishi wake madaraka, kila mmoja na kazi yake; akamwambia mlinzi
wa mlango awe macho.
35 Kesheni, basi, kwa maana hamjui mwenye nyumba atarudi
lini; huenda ikawa jioni, usiku wa manane, alfajiri au asubuhi.
36 Kesheni ili akija ghafla asije akawakuta mmelala.
37 Ninayowaambieni ninyi, nawaambia wote: Kesheni!"
|