Chapter 15
1 Kulipopambazuka, makuhani wakuu walifanya shauri pamoja
na wazee, walimu wa Sheria na Baraza lote, wakamfunga Yesu pingu, wakampeleka
na kumkabidhi kwa Pilato.
2 Pilato akamwuliza Yesu, "Je, wewe ni mfalme wa
Wayahudi?" Yesu akajibu, "Wewe umesema."
3 Makuhani wakuu wakamshtaki Yesu mambo mengi.
4 Pilato
akamwuliza tena Yesu, "Je, hujibu neno? Tazama wanavyotoa mashtaka mengi
juu yako."
5 Lakini
Yesu hakujibu neno, hata pilato akashangaa.
6 Kila
wakati wa sikukuu ya Pasaka, Pilato alikuwa na desturi ya kuwafungulia mfungwa
mmoja waliyemtaka.
7 Basi,
kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Baraba, ambaye alikuwa amefungwa pamoja na waasi
wengine kwa kusababisha uasi na mauaji.
8 Watu
wengi wakamwendea Pilato wakamwomba awafanyie kama kawaida yake.
9 Pilato
akawauliza, "Je, mwataka niwafungulieni Mfalme wa Wayahudi?"
10 Alisema
hivyo kwa sababu alijua wazi kwamba makuhani wakuu walimkabidhi Yesu kwake kwa
sababu ya wivu.
11 Lakini
makuhani wakuu wakawachochea watu wamwombe Pilato awafungulie Baraba.
12 Pilato
akawauliza tena, "Basi, sasa mwataka nifanye nini na mtu huyu mnayemwita
Mfalme wa Wayahudi?"
13 Watu
wote wakapaaza sauti tena: "Msulubishe!"
14 Lakini
Pilato akawauliza, "Kwa nini! Amefanya kosa gani?" Lakini wao
wakazidi kupaaza sauti, "Msulubishe!"
15 Pilato
alitaka kuuridhisha huo umati wa watu; basi, akamwachilia Baraba kutoka
gerezani. Akaamuru Yesu apigwe viboko, kisha akamtoa asulubiwe.
16 Kisha
askari walimpeleka Yesu ndani ukumbini, katika ikulu, wakakusanya kikosi kizima
cha askari.
17
Wakamvika vazi la rangi ya zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamwekea
kichwani.
18
Wakaanza kumsalimu, "Shikamoo Mfalme wa Wayahudi!"
19
Wakampiga kichwani kwa mwanzi, wakamtemea mate; wakampigia magoti na
kumsujudia.
20 Baada ya
kumdhihaki, walimvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka
kumsulubisha.
21
Walipokuwa njiani, walikutana na mtu mmoja aitwaye Simoni, mwenyeji wa Kurene.
Yeye alikuwa baba wa Aleksanda na Rufo, na wakati huo alikuwa akitoka shambani.
Basi, wakamlazimisha auchukue msalaba wa Yesu.
22 Kisha
wakampeleka Yesu mpaka mahali palipoitwa Golgotha, maana yake, "Mahali pa
Fuvu la Kichwa."
23 Wakampa
divai iliyochanganywa na manemane, lakini yeye akaikataa.
24 Basi,
wakamsulubisha, wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura waamue nani angepata
nini.
25 Ilikuwa
saa tatu asubuhi walipomsulubisha.
26 Na
mshtaka wake ulikuwa umeandikwa: "Mfalme wa Wayahudi."
27 Pamoja
naye waliwasulubisha wanyang`anyi wawili, mmoja upande wake wa kulia na
mwingine upande wake wa kushoto.*fh* Matakatifu yanayosema, "Aliwekwa
kundi moja na waovu."
28 missing
29 Watu
waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana, wakitikisa vichwa vyao na kusema,
"Aha! Wewe mwenye kuvunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu!
30 Sasa,
shuka msalabani ujiokoe mwenyewe!"
31 Nao
makuhani wakuu pamoja na walimu wa Sheria walimdhihaki wakisema,
"Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi!
32 Eti
yeye ni Kristo, Mfalme wa Israeli! Basi, na ashuke msalabani ili tuone na
kuamini." Hata watu wale waliosulubiwa pamoja naye walimtukana.
33 Tangu
saa sita mchana mpaka saa tisa kulikuwa giza nchini kote.
34 Saa
tisa alasiri Yesu akalia kwa sauti kubwa, "Eloi, Eloi, lema
sabakthani?" Maana yake, "Mungu wangu, Mungu wangu, mbona
umeniacha?"
35 Baadhi
ya watu waliosimama pale waliposikia hivyo, walisema, "Sikiliza! Anamwita
Eliya!"
36 Mtu
mmoja akakimbia, akachovya sifongo katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa
anywe akisema, "Hebu tuone kama Eliya atakuja kumteremsha msalabani!"
37 Yesu
akapaaza sauti kubwa, akakata roho.
38 Basi,
pazia la Hekalu likapasuka vipande viwili toka juu mpaka chini.
39
Jemadari mmoja aliyekuwa amesimama mbele yake aliona jinsi Yesu alivyolia kwa
sauti na kukata roho, akasema, "Kweli mtu huyu alikuwa Mwana wa
Mungu!"
40
Walikuwako pia wanawake waliotazama kwa mbali, miongoni mwao akiwa Maria toka
mji wa Magdala, Salome, na Maria mama wa kina Yakobo mdogo na Yose.
41 Hawa
walimfuata Yesu alipokuwa Galilaya na kumtumikia. Kulikuwa na wanawake wengine
wengi waliokuja Yerusalemu pamoja naye.
42 Wakati
wa jioni ulikuwa umekwisha fika. Hiyo ilikuwa siku ya Maandalio, yaani siku
inayotangulia Sabato.
43 Hapo
akaja Yosefu mwenyeji wa Armathaya, mjumbe wa Baraza Kuu, aliyeheshimika sana.
Yeye pia alikuwa anatazamia kuja kwa Ufalme wa Mungu. Basi, alimwendea Pilato
bila uoga, akaomba apewe mwili wa Yesu.
44 Pilato
alishangaa kusikia kwamba Yesu alikuwa amekwisha kufa. Basi, akamwita jemadari,
akamwuliza kama Yesu alikuwa amekufa kitambo.
45 Pilato
alipoarifiwa na huyo jemadari kwamba Yesu alikuwa amekwisha kufa, akamruhusu
Yosefu auchukue mwili wake.
46 Hapo
Yosefu akanunua sanda ya kitani, akauteremsha chini huo mwili, akauzungushia
sanda. Akauweka katika kaburi lililokuwa limechongwa mwambani, kisha
akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango.
47 Nao
Maria Magdalene na Maria mama yake Yose walipaona hapo alipolazwa.
|