Chapter 16
1 Baada ya
siku ya Sabato, Maria Magdalene, Salome na Maria mama yake Yakobo walinunua
manukato ili wakaupake mwili wa Yesu.
2 Basi,
alfajiri na mapema siku ya Jumapili, jua lilipoanza kuchomoza, walienda
kaburini.
3 Nao
wakawa wanaambiana, "Nani atakayetuondolea lile jiwe mlangoni mwa
kaburi?"
4 Lakini
walipotazama, waliona jiwe limekwisha ondolewa. (Nalo lilikuwa kubwa mno.)
5
Walipoingia kaburini, walimwona kijana mmoja aliyevaa vazi jeupe, ameketi
upande wa kulia; wakashangaa sana.
6 Lakini
huyo kijana akawaambia, "Msishangae. Mnamtafuta Yesu wa Nazareti
aliyesulubiwa. Amefufuka, hayumo hapa. Tazameni mahali walipokuwa wamemlaza.
7 Nendeni
mkawaambie wanafunzi wake pamoja na Petro ya kwamba anawatangulieni kule
Galilaya. Huko mtamwona kama alivyowaambieni."
8 Basi,
wakatoka pale kaburini mbio, maana walitetemeka kwa hofu na kushangaa.
Hawakumwambia mtu yeyote kitu, kwa sababu waliogopa mno. [[[
9 Yesu
alipofufuka mapema Jumapili, alijionyesha kwanza kwa Maria Magdalene, ambaye
Yesu alikuwa amemtoa pepo saba.
10 Maria
Magdalene akaenda, akawajulisha wale waliokuwa pamoja na Yesu, na wakati huo
walikuwa wanaomboleza na kulia.
11 Lakini
waliposikia ya kwamba Yesu yu hai na kwamba Maria Magdalene amemwona, hawakuamini.
12 Baadaye
Yesu aliwatokea wanafunzi wawili akiwa na sura nyingine. Wanafunzi hao walikuwa
wanakwenda shambani.
13 Nao pia
wakaenda wakawaambia wenzao. Hata hivyo hawakuamini.
14
Mwishowe, Yesu aliwatokea wanafunzi kumi na mmoja walipokuwa pamoja mezani.
Akawakemea sana kwa sababu ya kutoamini kwao na ukaidi wao, maana hawakuwaamini
wale waliokuwa wamemwona baada ya kufufuka.
15 Basi,
akawaambia, "Nendeni ulimwenguni kote mkahubiri Habari Njema kwa kila mtu.
16
Anayeamini na kubatizwa ataokolewa; asiyeamini atahukumiwa.
17 Na
ishara hizi zitaandamana na wale wanaoamini: kwa jina langu watatoa pepo na
watasema kwa lugha mpya.
18
Wakishika nyoka au wakinywa kitu chochote chenye sumu, hakitawadhuru.
Watawawekea wagonjwa mikono, nao watapona."
19 Basi,
Bwana Yesu alipokwisha sema nao, akachukuliwa mbinguni, akaketi upande wa kulia
wa Mungu.
20
Wanafunzi wakaenda wakihubiri kila mahali. Bwana akafanya kazi pamoja nao na
kuimarisha ujumbe huo kwa ishara zilizoandamana nao.]*fi*
|