Luke
Chapter 1
1
Mheshimiwa Theofilo: Watu wengi wamejitahidi kuandika juu ya mambo yale
yaliyotendeka kati yetu.
2
Waliandika kama tulivyoelezwa na wale walioyaona kwa macho yao tangu mwanzo, na
waliotangaza ujumbe huo.
3 Inafaa
nami pia, Mheshimiwa, baada ya kuchunguza kwa makini mambo yote tangu mwanzo,
nikuandikie kwa mpango,
4 ili nawe
uweze kujionea mwenyewe ukweli wa mambo yale uliyofundishwa.
5 Wakati
Herode alipokuwa mfalme wa Yudea, kulikuwa na kuhani mmoja jina lake Zakaria,
wa kikundi cha Abia. Mke wake alikuwa anaitwa Elisabeti, naye alikuwa wa ukoo
wa kuhani Aroni.
6 Wote
wawili walikuwa wanyofu mbele ya Mungu, wakiishi kwa kufuata amri na maagizo
yote ya Bwana bila lawama.
7 Lakini
hawakuwa wamejaliwa watoto kwa vile Elisabeti alikuwa tasa, nao wote wawili
walikuwa wazee sana.
8 Siku
moja, ilipokuwa zamu yake ya kutoa huduma ya ukuhani mbele ya Mungu,
9 Zakariya
alichaguliwa kwa kura, kama ilivyokuwa desturi, kuingia hekaluni ili afukize
ubani.
10 Watu,
umati mkubwa, walikuwa wamekusanyika nje wanasali wakati huo wa kufukiza ubani.
11 Malaika
wa Bwana akamtokea humo ndani, akasimama upande wa kulia wa madhabahu ya
kufukizia ubani.
12
Zakariya alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia.
13 Lakini
malaika akamwambia, "Zakariya, usiogope, kwa maana sala yako imesikilizwa,
na Elisabeti mkeo atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yohane.
14 Utakuwa
na furaha kubwa na watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake.
15 Atakuwa
mkuu mbele ya Bwana. Hatakunywa divai wala kileo, atajazwa Roho Mtakatifu tangu
tumboni mwa mama yake.
16
Atawaelekeza wengi wa watu wa Israeli kwa Bwana Mungu wao.
17
Atamtangulia Bwana akiongozwa na nguvu na roho kama Eliya. Atawapatanisha kina
baba na watoto wao; atawafanya wasiotii wawe na fikira za uadilifu, na hivyo
amtayarishie Bwana watu wake."
18
Zakariya akamwambia huyo malaika, "Ni kitu gani kitakachonihakikishia
jambo hilo? Mimi ni mzee, hali kadhalika na mke wangu."
19 Malaika
akamjibu, "Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele ya Mungu, na nimetumwa
niseme nawe, nikuletee hii habari njema.
20
Sikiliza, utakuwa bubu kwa sababu huyasadiki haya maneno yatakayotimia kwa
wakati wake. Hutaweza kusema mpaka hayo niliyokuambia yatakapotimia."
21 Wakati
huo, wale watu walikuwa wanamngoja Zakariya huku wakishangaa juu ya kukawia
kwake Hekaluni.
22
Alipotoka nje, hakuweza kusema nao. Ikawa dhahiri kwao kwamba alikuwa ameona
maono Hekaluni. Lakini akawa anawapa ishara kwa mikono, akabaki bubu.
23 Zamu
yake ya kuhudumu ilipokwisha, alirudi nyumbani.
24 Baadaye
Elisabeti mkewe akapata mimba. Akajificha nyumbani kwa muda wa miezi mitano,
akisema:
25
"Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana; ameniangalia na kuniondolea aibu
niliyokuwa nayo mbele ya watu."
26 Mnamo
mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao
Nazareti huko Galilaya,
27 kwa
msichana mmoja aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa
Daudi.
28 Malaika
akamwendea, akamwambia, "Salamu Maria! Umejaliwa neema nyingi! Bwana yu
pamoja nawe."
29 Maria
aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: maneno haya yanamaanisha
nini?
30 Malaika
akamwambia, "Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema.
31
Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume na utampa jina Yesu.
32 Yeye
atakuwa mkuu na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme
Daudi, babu yake.
33 Kwa
hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na
mwisho."
34 Maria
akamjibu, "Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?"
35 Malaika
akamjibu, "Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia
kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa
Mungu.
36 Ujue
pia kwamba hata Elisabeti, jamaa yako, naye amepata mimba ingawa ni mzee, na
sasa ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa.
37 Kwa
maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu."
38 Maria
akasema, "Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema."
Kisha yule malaika akaenda zake.
39 Siku
kadhaa baadaye, Maria alifunga safari akaenda kwa haraka hadi mji mmoja ulioko
katika milima ya Yuda.
40 Huko,
aliingia katika nyumba ya Zakariya, akamsalimu Elisabeti.
41 Mara tu
Elisabeti aliposikia sauti ya Maria, mtoto mchanga tumboni mwake Elisabeti
akaruka. Naye Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifiu,
42 akasema
kwa sauti kubwa, "Umebarikiwa kuliko wanawake wote, naye utakayemzaa
amebarikiwa.
43 Mimi ni
nani hata mama wa Bwana wangu afike kwangu?
44
Nakwambia, mara tu niliposikia sauti yako, mtoto mchanga tumboni mwangu aliruka
kwa furaha.
45 Heri
yako wewe uliyesadiki kwamba yatatimia yale Bwana aliyokwambia."
46 Naye
Maria akasema,
47
"Moyo wangu wamtukuza Bwana, roho yangu inafurahi kwa sababu ya Mungu
Mwokozi wangu.
48 Kwa
kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mnyenyekevu. Hivyo tangu sasa watu
wote wataniita mwenye heri.
49 Kwa
kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu, jina lake ni takatifu.
50 Huruma
yake kwa watu wanaomcha hudumu kizazi hata kizazi.
51
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake: amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya
mioyo yao;
52
amewashusha wenye nguvu kutoka vitu vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu.
53 Wenye
njaa amewashibisha mema, matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
54
Amemsaidia Israeli mtumishi wake, akikumbuka huruma yake.
55 Kama
alivyowaahidia wazee wetu Abrahamu na wazawa wake hata milele."
56 Maria
alikaa na Elisabeti kwa muda upatao miezi mitatu, halafu akarudi nyumbani
kwake.
57 Wakati
wa kujifungua kwake Elisabeti ulifika, akajifungua mtoto wa kiume.
58 Jirani
na watu wa jamaa yake walipopata habari kwamba Bwana amemwonea huruma kubwa,
walifurahi pamoja naye.
59 Halafu
siku ya nane walifika kumtahiri mtoto, wakataka kumpa jina la baba yake,
Zakariya.
60 Lakini
mama yake akasema, "La, sivyo, bali ataitwa Yohane."
61 Wakamwambia,
"Mbona hakuna yeyote katika ukoo wake mwenye jina hilo?"
62 Basi,
wakamwashiria baba yake wapate kujua alitaka mtoto wake apewe jina gani.
63 Naye
akaomba kibao cha kuandikia, akaandika hivi: "Yohane ndilo jina lake."
Wote wakastaajabu.
64 Papo
hapo midomo na ulimi wake Zakariya vikafunguliwa, akawa anaongea akimsifu
Mungu.
65 Hofu
ikawaingia jirani wote, na habari hizo zikaenea kila mahali katika milima ya
Yudea.
66 Wote
waliosikia mambo hayo waliyatafakari mioyoni mwao wakisema: "Mtoto huyu
atakuwa mtu wa namna gani?" Maana, hakika nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja
naye.
67
Zakariya, baba yake mtoto, akajazwa Roho Mtakatifu, akatamka ujumbe wa Mungu:
68
"Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli, kwani amekuja kuwasaidia na kuwakomboa
watu wake.
69
Ametupatia Mwokozi shujaa, mzawa wa Daudi mtumishi wake.
70
Aliahidi hapo kale kwa njia ya manabii wake watakatifu,
71 kwamba
atatuokoa mikononi mwa adui zetu na kutoka mikononi mwa wote wanaotuchukia.
72 Alisema
atawahurumia wazee wetu, na kukumbuka agano lake takatifu.
73 Kiapo
alichomwapia Abrahamu baba yetu, ni kwamba atatujalia sisi
74
tukombolewe kutoka adui zetu, tupate kumtumikia bila hofu,
75 kwa
unyofu na uadilifu mbele yake, siku zote za maisha yetu.
76 Nawe
mwanangu, utaitwa, nabii wa Mungu Mkuu, utamtangulia Bwana kumtayarishia njia
yake;
77
kuwatangazia watu kwamba wataokolewa kwa kuondolewa dhambi zao.
78 Mungu
wetu ni mpole na mwenye huruma. Atasababisha pambazuko angavu la ukombozi
litujie kutoka juu,
79 na
kuwaangazia wote wanaokaa katika giza kuu la kifo, aongoze hatua zetu katika
njia ya amani."
80 Mtoto
akakua, akapata nguvu rohoni. Alikaa jangwani mpaka alipojionyesha rasmi kwa
watu wa Israeli.
|