Chapter 2
1 Siku
zile, tangazo rasmi lilitolewa na Kaisari Augusto kuwataka watu wote chini ya
utawala wake wajiandikishe.
2
Kuandikishwa huku kulikuwa mara ya kwanza, wakati Kirenio alipokuwa mkuu wa
mkoa wa Siria.
3 Basi,
wote waliohusika walikwenda kujiandikisha, kila mtu katika mji wake.
4 Yosefu
pia alifanya safari kutoka mjini Nazareti mkoani Galilaya. Kwa kuwa alikuwa wa
jamaa na ukoo wa Daudi alikwenda mjini Bethlehemu mkoani Yuda alikozaliwa
Mfalme Daudi.
5
Alikwenda kujiandikisha pamoja na mchumba wake Maria ambaye alikuwa mja mzito.
6
Walipokuwa huko, siku yake ya kujifungua ikawadia,
7
akajifungua mtoto wake wa kwanza wa kiume, akamvika nguo za kitoto, akamlaza
horini kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni.
8 Katika
sehemu hizo, walikuwako wachungaji wakikesha usiku mbugani kulinda mifugo yao.
9 Malaika
wa Bwana akawatokea ghafla, na utukufu wa Bwana ukawaangazia pande zote.
Wakaogopa sana.
10 Malaika
akawaambia, "Msiogope! Nimewaleteeni habari njema ya furaha kuu kwa watu
wote.
11 Kwa
maana, leo hii katika mji wa Daudi, amezaliwa Mwokozi kwa ajili yenu, ndiye
Kristo Bwana.
12 Na hiki
kitakuwa kitambulisho kwenu: mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto,
amelazwa horini."
13 Mara
kundi kubwa la jeshi la mbinguni likajiunga na huyo malaika, wakamsifu Mungu
wakisema:
14
"Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, na amani duniani kwa watu aliopendezwa
nao!"
15 Baada
ya hao malaika kuondoka na kurudi mbinguni, wachungaji wakaambiana:
"Twendeni moja kwa moja mpaka Bethlehemu tukalione tukio hili Bwana
alilotujulisha."
16 Basi,
wakaenda mbio, wakamkuta Maria na Yosefu na yule mtoto mchanga amelazwa horini.
17 Hao
wachungaji walipomwona mtoto huyo wakawajulisha wote habari waliyokuwa
wamesikia juu yake.
18 Wote
waliosikia hayo walishangaa juu ya habari walizoambiwa na wachungaji.
19 Lakini
Maria aliyaweka na kuyatafakari mambo hayo yote moyoni mwake.
20 Wale
wachungaji walirudi makwao huku wakimtukuza na kumsifu Mungu kwa yote
waliyokuwa wamesikia na kuona; yote yalikuwa kama walivyokuwa wameambiwa.
21 Siku
nane baadaye, wakati wa kumtahiri mtoto ulipofika, walimpa jina Yesu, jina
ambalo alikuwa amepewa na malaika kabla hajachukuliwa mimba.
22 Siku
zilipotimia za Yosefu na Maria kutakaswa kama walivyotakiwa na Sheria ya Mose,
wazazi hao walimchukua mtoto, wakaenda naye Yerusalemu ili wamweke mbele ya
Bwana.
23 Katika
Sheria ya Bwana imeandikwa: "Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume atawekwa
wakfu kwa Bwana."
24 Pia
walikwenda ili watoe sadaka: hua wawili au makinda wawili ya njiwa, kama
ilivyotakiwa katika Sheria ya Bwana.
25 Wakati
huo huko Yerusalemu kulikuwa na mtu mmoja, mwema na mcha Mungu, jina lake
Simeoni. Yeye alikuwa akitazamia kwa hamu ukombozi wa Israeli. Roho Mtakatifu
alikuwa pamoja naye.
26 Roho
Mtakatifu alikuwa amemhakikishia kwamba hatakufa kabla ya kumwona Masiha wa
Bwana.
27 Basi,
akiongozwa na Roho Mtakatifu, Simeoni aliingia Hekaluni; na wazazi wa Yesu
walipomleta Hekaluni mtoto wao ili wamfanyie kama ilivyotakiwa na Sheria,
28 Simeoni
alimpokea mtoto Yesu mikononi mwake huku akimtukuza Mungu na kusema:
29
"Sasa Bwana, umetimiza ahadi yako, waweza kumruhusu mtumishi wako aende
kwa amani.
30 Maana
kwa macho yangu nimeuona wokovu utokao kwako,
31 ambao
umeutayarisha mbele ya watu wote:
32 Mwanga
utakaowaangazia watu wa mataifa, na utukufu kwa watu wako Israeli."
33 Baba na
mama yake Yesu walikuwa wakistaajabia maneno aliyosema Simeoni juu ya mtoto.
34 Simeoni
akawabariki, akamwambia Maria mama yake, "Mtoto huyu atakuwa sababu ya
kupotea na kuokoka kwa watu wengi katika Israeli. Naye atakuwa ishara
itakayopingwa na watu;
35 na
hivyo mawazo ya watu wengi yataonekana wazi. Nawe mwenyewe, uchungu ulio kama
upanga mkali utauchoma moyo wako."
36
Palikuwa na nabii mmoja mwanamke, mzee sana, jina lake Ana, binti Fanueli, wa
kabila la Asheri. Alikuwa ameishi na mumewe kwa miaka saba tangu alipoolewa.
37 Halafu
alibaki mjane hadi wakati huo akiwa mzee wa miaka themanini na minne. Wakati
huo wote alikaa Hekaluni akifunga na kusali usiku na mchana.
38 Saa
hiyohiyo alijitokeza mbele, akamshukuru Mungu, na akaeleza habari za huyo mtoto
kwa watu wote waliokuwa wanatazamia ukombozi wa Yerusalemu.
39 Hao
wazazi walipokwisha fanya yote yaliyoamriwa na Sheria ya Bwana, walirudi makwao
Nazareti, mkoani Galilaya.
40 Mtoto
akakua, akazidi kupata nguvu, akajaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa pamoja
naye.
41 Wazazi
wa Yesu walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kila mwaka wakati wa sikukuu
ya Pasaka.
42 Mtoto
alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, wote walikwenda kwenye sikukuu hiyo
kama ilivyokuwa desturi.
43 Baada
ya sikukuu, walianza safari ya kurudi makwao, lakini Yesu alibaki Yerusalemu
bila wazazi wake kuwa na habari.
44
Walidhani alikuwa pamoja na kundi la wasafiri, wakaenda mwendo wa kutwa, halafu
wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa na marafiki.
45 Kwa
kuwa hawakumwona, walirudi Yerusalemu wakimtafuta.
46 Siku ya
tatu walimkuta Hekaluni kati ya walimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali.
47 Wote
waliosikia maneno yake walistaajabia akili yake na majibu yake ya hekima.
48 Wazazi
wake walipomwona walishangaa. Maria, mama yake, akamwuliza, "Mwanangu, kwa
nini umetutenda hivyo? Baba yako na mimi tumekuwa tukikutafuta kwa
huzuni."
49 Yeye
akawajibu, "Kwa nini mlinitafuta? Hamkujua kwamba inanipasa kuwa katika
nyumba ya Baba yangu?"
50 Lakini
wazazi wake hawakuelewa maana ya maneno aliyowaambia.
51 Basi,
akarudi pamoja nao hadi Nazareti, akawa anawatii. Mama yake akaweka mambo hayo
yote moyoni mwake.
52 Naye
Yesu akaendelea kukua katika hekima na kimo; akazidi kupendwa na Mungu na watu.
|