Chapter 5
1 Siku moja
Yesu alikuwa amesimama kando ya ziwa Genesareti, na watu wengi walikuwa
wamemzunguka wakisongana wanalisikiliza neno la Mungu.
2 Akaona
mashua mbili ukingoni mwa ziwa; wavuvi wenyewe walikuwa wametoka, wanaosha
nyavu zao.
3 Baada ya
Yesu kuingia katika mashua moja, iliyokuwa ya Simoni, alimtaka Simoni aisogeze
majini, mbali kidogo na ukingo wa ziwa. Akaketi, akafundisha umati wa watu
akiwa ndani ya mashua.
4
Alipomaliza kufundisha, akamwambia Simoni, "Peleka mashua mpaka kilindini,
mkatupe nyavu zenu mpate kuvua samaki."
5 Simoni
akamjibu, "Bwana, tumejitahidi kuvua samaki usiku kucha bila kupata kitu,
lakini kwa kuwa umesema, nitatupa nyavu."
6 Baada ya
kufanya hivyo, wakavua samaki wengi, hata nyavu zao zikaanza kukatika.
7
Wakawaita wenzao waliokuwa katika mashua nyingine waje kuwasaidia. Wakaja,
wakazijaza mashua zote mbili samaki, hata karibu zingezama.
8 Simoni
Petro alipoona hayo, akapiga magoti mbele ya Yesu akisema, "Ondoka mbele
yangu, ee Bwana, kwa kuwa mimi ni mwenye dhambi!"
9 Simoni
pamoja na wenzake wote walishangaa kwa kupata samaki wengi vile.
10 Hali
kadhalika Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, waliokuwa wavuvi wenzake Simoni.
Yesu akamwambia Simoni, "Usiogope; tangu sasa utakuwa ukivua watu."
11 Basi,
baada ya kuzileta zile mashua ukingoni mwa ziwa, wakaacha yote, wakamfuata.
12 Ikawa,
Yesu alipokuwa katika mmojawapo wa miji ya huko, mtu mmoja mwenye ukoma mwili
mzima akamwona. Basi, mtu huyo akaanguka kifudifudi akamwomba Yesu:
"Mheshimiwa, ukitaka, waweza kunitakasa."
13 Yesu
akaunyosha mkono wake, akamgusa na kusema, "Nataka, takasika!" Mara
ule ukoma ukamwacha.
14 Yesu
akamwamuru: "Usimwambie mtu yeyote; bali nenda ukajionyeshe kwa kuhani,
ukatoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama inavyotakiwa na Sheria ya
Mose, iwe uthibitisho kwao kwamba umepona."
15 Lakini
habari za Yesu zilizidi kuenea kila mahali. Watu makundi mengi wakakusanyika
ili kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao.
16 Lakini
yeye alikwenda zake mahali pasipo na watu, akawa anasali huko.
17 Siku
moja Yesu alikuwa akifundisha. Mafarisayo na walimu wa Sheria kutoka katika
kila kijiji cha Galilaya, Yudea na Yerusalemu, walikuwa wameketi hapo. Nguvu ya
Bwana ilikuwa pamoja naye kwa ajili ya kuponyea wagonjwa.
18 Mara
watu wakaja wamemchukua mtu mmoja aliyepooza maungo, amelala kitandani;
wakajaribu kumwingiza ndani wamweke mbele ya Yesu.
19 Lakini
kwa sababu ya wingi wa watu, hawakuweza kuingia ndani. Basi, wakapanda juu ya
dari, wakaondoa vigae, wakamshusha huyo aliyepooza pamoja na kitanda chake,
wakamweka mbele ya Yesu.
20 Yesu
alipoona jinsi walivyokuwa na imani kubwa, akamwambia huyo mtu, "Rafiki,
umesamehewa dhambi zako."
21 Walimu
wa Sheria na Mafarisayo wakaanza kujiuliza: "Nani huyu anayemkufuru Mungu
kwa maneno yake? Hakuna mtu awezaye kusamehe dhambi ila Mungu peke yake!"
22 Yesu
alitambua mawazo yao, akawauliza, "Mnawaza nini mioyoni mwenu?
23 Ni lipi
lililo rahisi zaidi: kusema, `Umesamehewa dhambi,` au kusema, `Simama utembee`?
24 Basi,
nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anao uwezo wa kusamehe dhambi duniani."
Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza, "Simama, chukua kitanda chako uende
zako nyumbani."
25 Mara, huyo
mtu aliyepooza akasimama mbele yao wote, akachukua kitanda chake akaenda zake
nyumbani huku akimtukuza Mungu.
26 Wote
wakashangaa na kushikwa na hofu; wakamtukuza Mungu wakisema: "Tumeona
maajabu leo."
27 Baada
ya hayo, Yesu akatoka nje, akamwona mtoza ushuru mmoja aitwaye Lawi, ameketi
ofisini. Yesu akamwambia, "Nifuate!"
28 Lawi
akaacha yote, akamfuata.
29 Kisha
Lawi akamwandalia Yesu karamu kubwa nyumbani mwake; na kundi kubwa la watoza
ushuru na watu wengine walikuwa wameketi pamoja nao.
30
Mafarisayo na walimu wa Sheria wakawanung`unikia wafuasi wake wakisema:
"Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?"
31 Yesu
akawajibu, "Wenye afya hawahitaji daktari, lakini wanaomhitaji ni wale
walio wagonjwa.
32 Sikuja
kuwaita watu wema, bali wenye dhambi, ili wapate kutubu."
33 Watu
wengine wakamwambia Yesu, "Wafuasi wa Yohane mbatizaji hufunga mara nyingi
na kusali; hata wafuasi wa Mafarisayo hufanya vivyo hivyo. Lakini wafuasi wako
hula na kunywa."
34 Yesu
akawajibu, "Je, mnaweza kuwataka wale walioalikwa arusini wafunge hali
bwana arusi yuko pamoja nao?
35 Lakini
wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kati yao, na wakati huo ndipo
watakapofunga."
36 Yesu
akawaambia mfano huu: "Hakuna mtu akataye kiraka cha nguo mpya na kukitia
katika vazi kuukuu; kama akifanya hivyo, atakuwa amelikata hilo vazi jipya, na
hicho kiraka hakitachukuana na hilo vazi kuukuu.
37 Wala
hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; kwani hiyo divai mpya
itavipasua hivyo viriba, divai itamwagika, na viriba vitaharibika.
38 Divai
mpya hutiwa katika viriba vipya!
39 Wala
hakuna mtu ambaye hutamani kunywa divai mpya baada ya kunywa ya zamani, kwani
husema: `Ile ya zamani ni nzuri zaidi."`
|