Chapter 6
1 Siku
moja ya Sabato, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano, na wanafunzi
wake wakaanza kukwanyua masuke ya ngano, wakaondoa punje zake kwa mikono,
wakala.
2 Baadhi
ya Mafarisayo wakawauliza, "Mbona mnafanya jambo ambalo si halali siku ya
Sabato?"
3 Yesu
akawajibu, "Je, hamjasoma jinsi alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati
walipokuwa na njaa?
4 Yeye
aliingia ndani ya nyumba ya Mungu, akachukua ile mikate iliyowekwa mbele ya
Mungu, akala na kuwapa wenzake. Kisheria, ni makuhani tu peke yao ndio
walioruhusiwa kula mikate hiyo."
5 Hivyo
akawaambia, "Mwana wa Mtu ni Bwana wa Sabato."
6 Siku
nyingine ya Sabato, Yesu aliingia katika sunagogi, akafundisha. Mle ndani
mlikuwa na mtu ambaye mkono wake wa kuume ulikuwa umepooza.
7 Walimu
wa Sheria na Mafarisayo walitaka kupata kisingizio cha kumshtaki Yesu na hivyo
wakawa wanangojea waone kama angemponya mtu siku ya Sabato.
8 Lakini
Yesu alijua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, "Inuka,
simama katikati." Yule mtu akaenda akasimama katikati.
9 Kisha
Yesu akawaambia, "Nawaulizeni, je, ni halali siku ya Sabato kutenda jambo
jema au kutenda jambo baya; kuokoa maisha au kuyaangamiza?"
10 Baada
ya kuwatazama wote waliokuwa pale, akamwambia yule mtu, "Nyosha mkono
wako." Naye akafanya hivyo, na mkono wake ukawa mzima tena.
11 Lakini
wao wakakasirika sana, wakajadiliana jinsi ya kumtendea Yesu maovu.
12 Siku
moja Yesu alikwenda mlimani kusali, akakesha huko usiku kucha akimwomba Mungu.
13 Kesho
yake aliwaita wanafunzi wake, na miongoni mwao akachagua kumi na wawili ambao
aliwaita mitume:
14 Simoni
(ambaye Yesu alimpa jina Petro) na Andrea ndugu yake, Yakobo na Yohane, Filipo
na Bartholomayo,
15 Mathayo
na Thoma, Yakobo wa Alfayo na Simoni (aliyeitwa Zelote),
16 Yuda wa
Yakobo na Yuda Iskarioti ambaye baadaye alikuwa msaliti.
17 Baada
ya kushuka mlimani pamoja na mitume, Yesu alisimama mahali palipokuwa
tambarare. Hapo palikuwa na kundi kubwa la wanafunzi wake na umati wa watu
waliotoka pande zote za Yudea na Yerusalemu na pwani ya Tiro na Sidoni. Wote
walifika kumsikiliza Yesu na kuponywa magonjwa yao.
18
Aliwaponya pia wote waliokuwa wanasumbuliwa na pepo wachafu.
19 Watu
wote walitaka kumgusa, kwa maana nguvu ilikuwa inatoka ndani yake na kuwaponya
wote.
20 Yesu
akawageukia wanafunzi wake, akasema: "Heri ninyi mlio maskini, maana
Ufalme wa Mungu ni wenu.
21 Heri
ninyi mnaosikia njaa sasa, maana baadaye mtashiba. Heri ninyi mnaolia sasa,
maana baadaye mtacheka kwa furaha.
22
"Heri yenu ninyi iwapo watu watawachukia, watawatenga, watawatukana na
kuwaharibieni jina kwa ajili ya Mwana wa Mtu!
23 Wakati
hayo yatakapotokea, furahini na kucheza, maana hakika tuzo lenu ni kubwa mbinguni.
Kwa maana wazee wao waliwatendea manabii vivyo hivyo.
24 Lakini
ole wenu ninyi mlio matajiri, maana mmekwisha pata faraja yenu.
25 Ole
wenu ninyi mnaoshiba sasa, maana baadaye mtasikia njaa. Ole wenu ninyi
mnaocheka kwa furaha sasa, maana baadaye mtaomboleza na kulia.
26 Ole
wenu ninyi iwapo watu wote wanawasifu, maana wazee wao waliwafanyia manabii wa
uongo vivyo hivyo.
27
"Lakini nawaambieni ninyi mnaonisikiliza: wapendeni adui zenu, watendeeni
mema wale wanaowachukieni.
28
Watakieni baraka wale wanaowalaani, na waombeeni wale wanaowatendea vibaya.
29 Mtu
akikupiga shavu moja mgeuzie na la pili. Mtu akikunyang`anya koti lako mwachie
pia shati lako.
30 Yeyote
anayekuomba mpe, na mtu akikunyang`anya mali yako usimtake akurudishie.
31
Watendeeni wengine kama mnavyotaka wawatendee ninyi.
32
"Na ikiwa mnawapenda tu wale wanaowapenda ninyi, je, mtapata tuzo gani?
Hakuna! Kwa maana hata wenye dhambi huwapenda wale wanaowapenda wao.
33 Tena, kama mkiwatendea mema wale tu wanaowatendeeni
mema, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi hufanya vivyo hivyo!
34 Na kama mnawakopesha wale tu mnaotumaini watawalipeni,
je, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi wenzao ili
warudishiwe kima kilekile!
35 Ila nyinyi wapendeni adui zenu, na kuwatendea mema;
kopesheni bila kutazamia malipo, na tuzo lenu litakuwa kubwa, nanyi mtakuwa
watoto wa Mungu aliye juu. Kwa maana yeye ni mwema kwa wale wasio na shukrani
na walio wabaya.
36 Muwe na
huruma kama Baba yenu alivyo na huruma.
37 "Msiwahukumu
wengine, nanyi hamtahukumiwa; msiwalaumu wengine, nanyi hamtalaumiwa;
wasameheni wengine, nanyi mtasamehewa.
38 Wapeni
wengine wanavyohitaji, nanyi mtapewa. Naam, mtapokea mikononi mwenu kipimo
kilichojaa, kikashindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika. Kwa maana kipimo
kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho ambacho Mungu atatumia kwenu."
39
Akawaambia mfano huu: "Je, kipofu anaweza kumwongoza kipofu mwenzake? La!
Wote wataanguka shimoni.
40 Mwanafunzi
hamshindi mwalimu wake, lakini kila mwanafunzi akisha hitimu huwa kama mwalimu
wake.
41
Unawezaje kukiona kibanzi kilicho katika jicho la mwenzio, usione boriti iliyo
katika jicho lako mwenyewe?
42 Au,
unawezaje kumwambia mwenzako, `Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi katika jicho
lako,` na huku huioni boriti iliyoko katika jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe!
Toa kwanza boriti iliyoko jichoni mwako, na hivyo utaona sawasawa kiasi cha
kuweza kuondoa kibanzi kilicho katika jicho la ndugu yako.
43
"Mti mwema hauzai matunda mabaya, wala mti mbaya hauzai matunda mazuri.
44 Watu
huutambua mti kutokana na matunda yake. Ni wazi kwamba watu hawachumi tini
katika michongoma, wala hawachumi zabibu katika mbigili.
45 Mtu
mwema hutoa yaliyo mema kutoka katika hazina bora iliyo moyoni mwake; na mtu
mbaya hutoa yaliyo mabaya katika hazina mbaya iliyo moyoni mwake, kwa maana mtu
huongea kutokana na yale yaliyojaa moyoni mwake.
46
"Mbona mwaniita `Bwana, Bwana,` na huku hamtimizi yale ninayosema?
47
Nitawapeni mfano unaofaa kuonyesha alivyo yeyote yule anayekuja kwangu,
akasikia maneno yangu na kuyatimiza:
48 Huyo
anafanana na mtu ajengaye nyumba, ambaye amechimba chini na kuweka msingi wake
juu ya mwamba; kukatokea mafuriko ya mto, mkondo wa maji ukaipiga nyumba ile,
lakini haukuweza kuitikisa, kwa sababu ilikuwa imejengwa imara.
49 Lakini
yeyote anayesikia maneno yangu lakini asifanye chochote, huyo anafanana na mtu
aliyejenga nyumba juu ya udongo, bila msingi. Mafuriko ya mto yakatokea, mkondo
wa maji ukaipiga nyumba ile, ikaanguka na kuharibika kabisa!"
|