Chapter 7
1 Baada ya
kusema yale aliyotaka watu wasikie, Yesu alikwenda Kafarnaumu.
2 Huko
kulikuwa na jemadari mmoja Mroma ambaye alikuwa na mtumishi wake aliyempenda
sana. Huyu mtumishi alikuwa mgonjwa karibu kufa.
3 Yule
jemadari aliposikia habari za Yesu, aliwatuma wazee fulani Wayahudi waende
kumwomba aje amponye mtumishi wake.
4
Walipofika kwa Yesu, walimsihi sana, wakasema: "Huyu anastahili afanyiwe
jambo hilo,
5 maana
analipenda taifa letu, na ndiye aliyetujengea lile sunagogi."
6 Basi,
Yesu akaenda pamoja nao. Alipokuwa karibu kufika nyumbani kwa yule jemadari
Mroma, yule jemadari aliwatuma marafiki zake wamwambie Yesu: "Bwana,
usijisumbue zaidi, maana mimi sistahili uingie nyumbani mwangu.
7 Ndio
maana sikujiona nastahili hata kuja kwako; amuru tu, na mtumishi wangu atapona.
8 Mimi pia
ni mtu niliye chini ya mamlaka, na ninao askari chini yangu. Namwambia mmoja,
`Nenda!`, naye huenda; namwambia mwingine, `Njoo!` naye huja; na nikimwambia
mtumishi wangu, `Fanya hiki!`, hufanya."
9 Yesu
aliposikia hayo, alishangaa; halafu akauelekea ule umati wa watu uliokuwa
unamfuata, akasema, "Sijaona imani kubwa namna hii hata katika
Israeli."
10 Wale
watu walipowasili nyumbani walimkuta yule mtumishi hajambo kabisa.
11 Baadaye
kidogo Yesu alikwenda katika mji mmoja uitwao Naini, na wafuasi wake pamoja na
kundi kubwa la watu waliandamana naye.
12 Basi,
alipokuwa anakaribia lango la mji, walitokea watu wamebeba maiti ya kijana
mmoja, mtoto wa pekee wa mama mjane. Watu wengi wa mji ule walikuwa pamoja na
huyo mama.
13 Bwana
alipomwona mama huyo, alimwonea huruma, akamwambia, "Usilie."
14 Kisha
akaenda, akaligusa lile jeneza, na wale waliokuwa wanalichukua wakasimama.
Halafu akasema, "Kijana! Nakuamuru, amka!"
15 Yule
aliyekufa akaketi, akaanza kuongea. Na Yesu akamkabidhi kwa mama yake.
16 Watu
wote walishikwa na hofu, wakawa wanamtukuza Mungu wakisema: "Nabii mkuu
ametokea kati yetu. Mungu amekuja kuwakomboa watu wake."
17 Habari
hizo zikaenea kote katika Uyahudi na katika nchi za jirani.
18
Wanafunzi wa Yohane walimpa habari Yohane juu ya mambo hayo yote. Naye Yohane,
baada ya kuwaita wawili kati ya wanafunzi wake,
19
aliwatuma kwa Bwana wamwulize: "Wewe ndiye yule ajaye, au tumtazamie
mwingine?"
20 Wale
wanafunzi walipomfikia Yesu wakamwambia, "Yohane Mbatizaji ametutuma kwako
tukuulize: `Wewe ndiye yule ajaye, au tumtazamie mwingine?"`
21 Wakati
huohuo, Yesu alikuwa anawaponya watu wengi waliokuwa wanateseka kwa magonjwa na
waliopagawa na pepo wabaya, akawawezesha vipofu wengi kuona tena.
22 Basi,
Yesu akawajibu, "Nendeni mkamwambie Yohane yale mliyojionea na kuyasikia:
vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia,
wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa Habari njema.
23 Heri
mtu yule ambaye hana mashaka nami!"
24 Hapo
wajumbe wa Yohane walipokwisha kwenda zao, Yesu alianza kuyaambia makundi ya
watu juu ya Yohane: "Mlikwenda kule jangwani, hivi mlitaka kuona kitu
gani? Mlitaka kuona unyasi unaotikiswa na upepo?
25 Basi,
mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona mtu aliyevalia mavazi maridadi?
La hasha! Wanaovaa mavazi maridadi na kuishi maisha ya anasa, hukaa katika
majumba ya wafalme!
26 Basi, niambieni, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona
nabii? Naam, hakika ni zaidi ya nabii.
27 Huyu Yohane ndiye anayesemwa katika Maandiko Matakatifu:
`Hapa ni mtumishi wangu, asema Bwana; ninamtuma akutangulie, akutayarishie
njia."`
28 Yesu akamalizia kwa kusema, "Nawaambieni, kati ya
binadamu wote hakuna aliye mkubwa zaidi kuliko Yohane Mbatizaji. Hata hivyo,
yule aliye mdogo kabisa katika ufalme wa Mungu ni mkubwa zaidi kuliko
yeye."
29 Waliposikia hayo watu wote na watoza ushuru waliusifu
wema wa Mungu; hao ndio wale waliokuwa wameupokea ubatizo wa Yohane.
30 Lakini Mafarisayo na walimu wa Sheria walikataa mpango
wa Mungu uliowahusu wakakataa kubatizwa na Yohane.
31 Yesu akaendelea kusema, "Basi, nitawafananisha watu
wa kizazi hiki na kitu gani? Ni watu wa namna gani?
32 Ni kama vijana waliokuwa wamekaa sokoni na kuambiana,
kikundi kimoja na kingine: `Tumewapigieni ngoma, lakini hamkucheza!
Tumeomboleza, lakini hamkulia!`
33 Kwa maana Yohane alikuja, yeye alifunga na hakunywa
divai, nanyi mkasema: `Amepagawa na pepo!`
34 Akaja Mwana wa Mtu; anakula na kunywa, mkasema:
`Mwangalieni mlafi huyu na mlevi; rafiki ya watoza ushuru na wenye dhambi!`
35 Hata hivyo, hekima ya Mungu imethibitishwa kuwa njema na
wote wale wanaoikubali."
36 Mfarisayo mmoja alimwalika Yesu kula chakula nyumbani
kwake. Akaingia nyumbani mwa huyo Mfarisayo, akakaa kula chakula.
37 Basi, katika mji ule kulikuwa na mama mmoja aliyekuwa
anaishi maisha mabaya. Alipopata habari kwamba Yesu yuko nyumbani kwa huyo
Mfarisayo, alichukua chupa ya alabasta yenye marashi.
38 Akaja, akasimama karibu na miguu yake Yesu, akilia, na
machozi yake yakamdondokea Yesu miguuni. Huyo mwanamke akaipangusa miguu ya
Yesu kwa nywele zake. Kisha akaibusu na kuipaka yale marashi.
39 Yule Mfarisayo aliyemwalika Yesu alipoona hayo, akawaza
moyoni mwake, "Kama mtu huyu angekuwa kweli nabii angejua huyu mwanamke ni
wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi."
40 Yesu akamwambia huyo Mfarisayo, "Simoni, ninacho
kitu cha kukwambia." Naye Simoni akamwambia, "Ndio Mwalimu,
sema." Yesu akasema,
41 "Watu wawili walikuwa wamemkopa mtu fedha: mmoja
alikuwa amekopa dinari mia tano, na mwingine hamsini.
42 Waliposhindwa kulipa madeni yao, huyo mtu aliwasamehe
wote wawili. Sasa ni yupi kati ya hao wawili atampenda zaidi huyo bwana?"
43 Simoni akamjibu, "Ni dhahiri kwamba yule
aliyesamehewa deni kubwa zaidi atampenda zaidi yule bwana." Yesu
akamwambia, "Sawa."
44 Halafu akamgeukia yule mwanamke na kumwambia Simoni,
"Unamwona huyu mwanamke, sivyo? Basi, mimi nilipoingia hapa nyumbani kwako
hukunipa maji ya kunawa miguu yangu; lakini mwanamke huyu ameniosha miguu yangu
kwa machozi yake na kunipangusa kwa nywele zake.
45 Wewe hukunisalimu kwa kunibusu, lakini huyu mwanamke
tangu nilipoingia hapa amekuwa akiibusu miguu yangu.
46 Wewe hukunionyesha ukarimu wako kwa kunipaka mafuta
kichwani, lakini huyu mwanamke amefanya hivyo kwa kunipaka mafuta miguu yangu.
47 Kwa hiyo nakwambia amesamehewa dhambi zake nyingi kwa
kuwa ameonyesha upendo mkubwa. Mwenye kusamehe kidogo, hupenda kidogo."
48 Basi, Yesu akamwambia yule mwanamke, "Umesamehewa
dhambi zako."
49 Na hapo wale waliokuwa pamoja naye mezani wakaulizana,
"Ni mtu wa namna gani huyu awezaye kusamehe dhambi?"
50 Naye Yesu akamwambia yule mwanamke, "Imani yako
imekuokoa; nenda kwa amani."
|