Chapter 9
1 Yesu aliwaita wale kumi na wawili, akawapa uwezo juu ya
pepo wote, na uwezo wa kuponya wagonjwa.
2 Halafu akawatuma waende kuhubiri Ufalme wa Mungu na
kuponya wagonjwa.
3 Akawaambia, "Mnaposafiri msichukue chochote:
msichukue fimbo, wala mkoba, wala chakula, wala fedha, wala hata koti la ziada.
4 Nyumba yoyote mtakayoingia na kukaribishwa, kaeni humo
mpaka mtakapoondoka katika kijiji hicho.
5 Watu wakikataa kuwakaribisha, tokeni katika mji huo,
nanyi mnapotoka kung`uteni mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao."
6 Basi, wakaanza safari, wakapitia vijijini wakihubiri
Habari Njema na kuponya wagonjwa kila mahali.
7 Sasa, mtawala Herode, alipata habari za mambo yote
yaliyokuwa yanatendeka, akawa na wasiwasi kwa vile walikuwa wakisema:
"Yohane amefufuka kutoka wafu!"
8 Wengine walisema kwamba Eliya ametokea, na wengine
walisema kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amerudi duniani.
9 Lakini Herode akasema, "Huyo Yohane nilimkata
kichwa; sasa ni nani huyu ninayesikia habari zake?" Akawa na hamu ya
kumwona.
10 Wale mitume waliporudi, walimweleza yote waliyoyafanya.
Yesu akawachukua, wakaenda peke yao mjini Bethsaida.
11 Lakini wale watu walipojua alikokwenda, walimfuata. Yesu
akawakaribisha akawazungumzia juu ya Ufalme wa Mungu, akawaponya wale
waliohitaji kuponywa.
12 Jua lilipokuwa linaanza kutua, wale kumi na wawili
walimwendea wakamwambia, "Waage watu waende kwenye vijiji na mashamba ya
karibu, wakajipatie chakula na mahali pa kulala, kwa maana hapa tulipo ni
nyikani."
13 Lakini Yesu akawaambia, "Wapeni ninyi
chakula." Wakamjibu, "Hatuna chochote ila mikate mitano na samaki
wawili. Labda twende wenyewe tukawanunulie chakula watu wote hawa!"
14 (Walikuwepo pale wanaume wapatao elfu tano.) Basi, Yesu
akawaambia wanafunzi wake, "Waambieni watu waketi katika makundi ya watu
hamsinihamsini."
15 Wanafunzi wakafanya walivyoambiwa, wakawaketisha wote.
16 Kisha Yesu akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki
wawili, akatazama juu mbinguni, akamshukuru Mungu, akavimega, akawapa wanafunzi
wake wawagawie watu.
17 Wakala wote, wakashiba; wakakusanya makombo ya chakula,
wakajaza vikapu kumi na viwili.
18 Siku moja, Yesu alikuwa anasali peke yake, na wanafunzi
wake walikuwa karibu. Basi, akawauliza, "Eti watu wanasema mimi ni
nani?"
19 Nao wakamjibu, "Wengine wanasema kuwa wewe ni
Yohane mbatizaji, wengine wanasema wewe ni Eliya, hali wengine wanasema kuwa
wewe ni mmoja wa manabii wa kale ambaye amefufuka."
20 Hapo akawauliza, "Na ninyi je, mwasema mimi ni
nani?" Petro akajibu, "Wewe ndiwe Kristo wa Mungu."
21 Halafu Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote habari
hiyo.
22 Akaendelea kusema: "Ni lazima Mwana wa Mtu apate
mateso mengi na kukataliwa na wazee na makuhani wakuu na walimu wa Sheria;
atauawa, lakini siku ya tatu atafufuliwa."
23 Kisha akawaambia watu wote, "Mtu yeyote akitaka
kuwa mfuasi wangu, ni lazima ajikane nafsi yake, auchukue msalaba wake kila
siku, anifuate.
24 Maana, mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe,
atayapoteza; lakini atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayaokoa.
25 Je, kuna faida gani mtu kuupata utajiri wote wa dunia
kwa kujipoteza au kujiangamiza yeye mwenyewe?
26 Mtu akinionea aibu mimi na mafundisho yangu, Mwana wa
Mtu atamwonea aibu mtu huyo wakati atakapokuja katika utukufu wake na wa Baba
na wa malaika watakatifu.
27 Nawaambieni kweli, kuna wengine papa hapa ambao
hawatakufa kabla ya kuuona Ufalme wa Mungu."
28 Yapata siku nane baada ya kusema hayo, Yesu aliwachukua
Petro, Yohane na Yakobo, akaenda nao mlimani kusali.
29 Alipokuwa akisali, sura yake ilibadilika, mavazi yake
yakawa meupe na kung`aa sana.
30 Na watu wawili wakaonekana wakizungumza naye, nao ni
Mose na Eliya,
31 ambao walitokea wakiwa wenye utukufu, wakazungumza naye
juu ya kifo chake ambacho angekikamilisha huko Yerusalemu.
32 Petro na wenzake walikuwa wamelemewa na usingizi mzito,
hata hivyo waliamka, wakauona utukufu wake, wakawaona na wale watu wawili
waliokuwa wamesimama pamoja naye.
33 Basi, watu hao wawili walipokuwa wakiondoka, Petro
alimwambia Yesu, "Bwana, ni vizuri kwamba tupo hapa: basi, tujenge vibanda
vitatu: kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Eliya."--Kwa kweli
hakujua anasema nini.
34 Petro alipokuwa akisema hayo, mara wingu likatokea na
kuwafunika; na wingu hilo lilipowajia, wale wanafunzi waliogopa sana.
35 Sauti ikasikika kutoka katika hilo wingu: "Huyu
ndiye Mwanangu niliyemchagua, msikilizeni."
36 Baada ya hiyo sauti kusikika, Yesu alionekana akiwa peke
yake. Wanafunzi walikaa kimya juu ya tukio hilo, na wakati ule hawakumwambia
mtu yeyote mambo hayo waliyoyaona.
37 Kesho yake walipokuwa wakishuka kutoka kule mlimani,
kundi kubwa la watu lilikutana na Yesu.
38 Hapo, mtu mmoja katika lile kundi akapaaza sauti,
akasema, "Mwalimu! Ninakusihi umwangalie mwanangu - mwanangu wa pekee!
39 Pepo huwa anamshambulia, na mara humfanya apige kelele;
humtia kifafa, na povu likamtoka kinywani. Huendelea kumtesa sana, asimwache
upesi.
40 Niliwaomba wanafunzi wako wamfukuze, lakini
hawakuweza."
41 Yesu akasema, "Enyi kizazi kisicho na imani,
kilichopotoka! Nitakaa nanyi na kuwavumilia mpaka lini?" Kisha akamwambia
huyo mtu, "Mlete mtoto wako hapa."
42 Wakati mtoto huyo alipokuwa anamjia Yesu, yule pepo
alimwangusha chini na kumtia kifafa. Lakini Yesu akamkemea yule pepo mchafu
akamponya mtoto na kumkabidhi kwa baba yake.
43 Watu wote wakashangazwa na uwezo mkuu wa Mungu. Wale
watu walipokuwa bado wanashangaa juu ya mambo yote aliyofanya, Yesu aliwaambia
wanafunzi wake,
44 "Tegeni masikio, myasikie mambo haya: Mwana wa Mtu
anakwenda kutiwa mikononi mwa watu."
45 Lakini wao hawakuelewa maana ya usemi huo. Jambo hilo
lilikuwa limefichwa kwao ili wasitambue; nao wakaogopa kumwuliza juu ya msemo
huo.
46 Kukatokea majadiliano kati ya wale wanafunzi kuhusu nani
kati yao aliyekuwa mkuu zaidi.
47 Yesu aliyajua mawazo yaliyokuwa mioyoni mwao; basi
akamchukua mtoto mdogo akamweka karibu naye,
48 akawaambia, "Mtu yeyote anayempokea mtoto huyu
mdogo kwa jina langu, ananipokea mimi; na yeyote anayenipokea mimi, anampokea
yule aliyenituma. Maana yule aliye mdogo kuliko wote kati yenu ndiye aliye
mkubwa kuliko wote."
49 Yohane alidakia na kusema, "Bwana, tumemwona mtu
mmoja akitoa pepo kwa kulitumia jina lako nasi tukajaribu kumkataza kwa kuwa
yeye si mmoja wetu."
50 Lakini Yesu akamwambia, "Msimkataze; kwani
asiyepingana nanyi yuko upande wenu."
51 Wakati ulipokaribia ambapo Yesu angechukuliwa juu
mbinguni, yeye alikata shauri kwenda Yerusalemu.
52 Basi, akawatuma wajumbe wamtangulie, nao wakaenda
wakaingia kijiji kimoja cha Wasamaria ili wamtayarishie mahali.
53 Lakini wenyeji wa hapo hawakutaka kumpokea kwa sababu
alikuwa anaelekea Yerusalemu.
54 Basi, wanafunzi wake, kina Yohane na Yakobo, walipoona
hayo, wakasema, "Bwana, wataka tuamuru moto ushuke kutoka mbinguni
uwateketeze?"
55 Lakini yeye akawageukia, akawakemea.*fa*
56 Wakatoka, wakaenda kijiji kingine. gani mliyo nayo; kwa
maana Mwana wa Mtu hakuja kuyaangamiza maisha ya watu, bali kuyaokoa."
57 Walipokuwa wakisafiri njiani, mtu mmoja akamwambia Yesu,
"Nitakufuata kokote utakakokwenda."
58 Yesu akasema, "Mbweha wana mapango, na ndege wana
viota; lakini Mwana wa Mtu hana mahali pa kupumzikia."
59 Kisha akamwambia mtu mwingine, "Nifuate."
Lakini huyo akasema, "Bwana, niruhusu kwanza niende kumzika baba
yangu."
60 Yesu akamwambia, "Waache wafu wazike wafu wao; bali
wewe nenda ukatangaze Ufalme wa Mungu."
61 Na mtu mwingine akamwambia, "Nitakufuata, lakini
niruhusu kwanza nikawaage wale walio nyumbani kwangu."
62 Yesu akamwambia, "Yeyote anayeshika jembe tayari
kulima na huku anaangalia nyuma, hafai kwa Ufalme wa Mungu."
|