Chapter 10
1 Baada ya hayo, Bwana aliwachagua wengine sabini na
wawili, akawatuma wawiliwawili, wamtangulie katika kila kijiji na mahali ambapo
yeye mwenyewe alitaka kwenda.
2 Akawaambia, "Mavuno ni mengi, lakini wavunaji ni
wachache. Kwa hivyo, mwombeni mwenye shamba atume wavunaji shambani mwake.
3 Sasa nendeni; fahamuni kwamba ninawatuma ninyi kama
kondoo wanaokwenda kati ya mbwa mwitu.
4 Msichukue mfuko wa fedha, mkoba, wala viatu; msimsalimu
mtu yeyote njiani.
5 Mkiingia katika nyumba yoyote, kwanza wasalimuni hivi:
`Amani iwe katika nyumba hii!`
6 Kama akiwako mwenye kupenda amani, amani yenu itakaa
naye, la sivyo, itawarudieni.
7 Kaeni katika nyumba hiyo mkila na kunywa wanavyowapeni,
maana mfanyakazi anastahili mshahara wake. Msiende mara nyumba hii mara nyumba
ile.
8 Kama mkifika mji fulani na watu wakiwakaribisha, kuleni
wanavyowapeni.
9 Ponyeni wagonjwa walioko huko, waambieni watu: `Ufalme wa
Mungu umekaribia kwenu.`
10 Lakini mkiingia katika mji wowote, wasipowakaribisheni,
tokeni; nanyi mpitapo katika barabara zao semeni:
11 `Hata mavumbi ya mji wenu yaliyoshikamana na miguu yetu
tunawakung`utieni. Lakini, jueni kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia.`
12 Hakika nawaambieni, siku ile mji huo utapata adhabu
kubwa zaidi kuliko ile ya watu wa Sodoma.
13 "Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Maana, kama
miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika kule Tiro na Sidoni, watu wake
wangalikwishavaa mavazi ya gunia kitambo, na kukaa katika majivu kuonyesha
kwamba wametubu.
14 Hata hivyo, Siku ya Hukumu ninyi mtapata adhabu kubwa
zaidi kuliko ile ya watu wa Tiro na Sidoni.
15 Na wewe Kafarnaumu, unataka kujikweza mpaka mbinguni?
La; utaporomoshwa mpaka Kuzimu."
16 Halafu akasema, "Anayewasikiliza ninyi,
ananisikiliza mimi; na anayekataa kuwapokea ninyi, anakataa kunipokea mimi.
Yeyote anayekataa kunipokea, anakataa kumpokea yule aliyenituma."
17 Baadaye, wale sabini na wawili walirudi wamejaa furaha,
wakisema, "Bwana, hata pepo wametutii tulipolitaja jina lako."
18 Yeye akawaambia, "Nilimwona Shetani jinsi
alivyokuwa anaporomoka kama umeme kutoka mbinguni.
19 Naam, nimewapeni uwezo wa kukanyaga nyoka na ng`e, na
uwezo juu ya nguvu zote za yule adui; hakuna chochote kitakachowadhuru.
20 Hata hivyo, msifurahi kwa sababu pepo wamewatii, bali
furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni." ic
21 Saa ileile, Yesu akafurahi kwa uwezo wa Roho Mtakatifu,
akasema, "Nakushukuru ee Baba, Bwana wa mbingu na dunia, kwa kuwa
umewaficha wenye hekima na elimu mambo haya, ukawafumbulia wadogo. Naam, Baba,
ndivyo ilivyokupendeza."
22 Kisha akasema, "Baba yangu ameweka yote mikononi
mwangu. Hakuna amjuaye Mwana ni nani ila Baba, wala amjuaye Baba ni nani ila
Mwana, na yeyote yule ambaye Mwana anataka kumfunulia hayo."
23 Halafu akawaelekea wafuasi wake akawaambia, "Heri
wanaoona yale mnayoyaona ninyi!
24 Hakika, manabii na wafalme walitamani kuona yale
mnayoyaona ninyi wasiyaone, na kusikia yale mnayoyasikia wasiyasikie."
25 Baadaye mwalimu mmoja wa Sheria alisimama akamwuliza
akitaka kumtega, "Mwalimu, nifanye nini ili nipate uzima wa milele?"
26 Yesu akamwuliza, "Imeandikwa nini katika Sheria?
Unaelewaje?"
27 Akamjibu, "Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako
wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote. Na,
mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe."
28 Yesu akawaambia, "Vema! Fanya hivyo, nawe
utaishi."
29 Lakini yeye akitaka kujihakikishia kuwa mwema akamwuliza
Yesu, "Na jirani yangu ni nani?"
30 Yesu akamjibu, "Mtu mmoja alikuwa anashuka kutoka
Yerusalemu kwenda Yeriko. Alipokuwa njiani, alivamiwa na majambazi,
wakamnyang`anya mali yake na kumpiga, wakamwacha amelala pale nusu mfu.
31 Kumbe, kuhani mmoja akawa anapita barabara ileile,
akamwona, akapita kando.
32 Hali kadhalika na Mlawi mmoja, alipofika mahali
akamwona, akapita kando.
33 Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa anasafiri, alifika pale
yule mtu alipokuwa, naye alipomwona, alimwonea huruma.
34 Akamwendea, akamtibu majeraha yake kwa kumtia mafuta na
divai; na kuyafunga halafu akampandisha juu ya punda wake akampeleka katika
nyumba moja ya wageni akamuuguza.
35 Kesho yake akatoa fedha dinari mbili akampa yule mwenye
nyumba, akamwambia, `Muuguze mtu huyu; na chochote utakachotumia zaidi,
nitakulipa nitakaporudi."`
36 Kisha Yesu akauliza, "Kati ya hao watatu, ni yupi
aliyeonyesha kuwa jirani yake yule aliyevamiwa na majambazi?"
37 Yule mwalimu wa Sheria akamjibu, "Ni yule
aliyemwonea huruma." Yesu akamwambia, "Nenda ukafanye vivyo
hivyo."
38 Walipokuwa safarini, waliingia katika kijiji kimoja na
mwanamke mmoja, aitwaye Martha, alimkaribisha nyumbani kwake.
39 Martha alikuwa na dada yake aitwaye Maria; huyu aliketi
karibu na Yesu akisikiliza mafundisho yake.
40 Lakini Martha alikuwa anashughulika na mambo mengi.
Basi, akamwendea Yesu, akamwambia, "Bwana, hivi hujali kwamba dada yangu
ameniacha nishughulike peke yangu? Mwambie basi, anisaidie."
41 Lakini Bwana akamjibu, "Martha, Martha, unahangaika
na kusumbuka kwa mambo mengi.
42 Kitu kimoja
tu ni muhimu. Maria amechagua kitu bora zaidi ambacho hakuna mtu
atakayemnyag`anya."
|