Chapter 11
1 Siku moja,
Yesu alikuwa mahali fulani akisali. Alipomaliza kusali, mmoja wa wanafunzi wake
akamwambia, "Bwana, tunakuomba utufundishe kusali kama Yohane mbatizaji
alivyowafundisha wanafunzi wake."
2 Yesu akawaambia, "Mnaposali, semeni: `Baba! Jina
lako litukuzwe; Ufalme wako ufike.
3 Utupe daima chakula chetu cha kila siku.
4 Utusamehe dhambi zetu, maana sisi tunawasamehe wote
waliotukosea; wala usitutie katika majaribu."`
5 Kisha akawaambia, "Tuseme mmoja wenu anaye rafiki,
akaenda kwake usiku wa manane, akamwambia: `Rafiki, tafadhali niazime mikate
mitatu,
6 kwa kuwa rafiki yangu amepitia kwangu akiwa safarini nami
sina cha kumpa.`
7 Naye, akiwa ndani angemjibu: `Usinisumbue! Nimekwisha
funga mlango. Mimi na watoto wangu tumelala; siwezi kuamka nikupe!`
8 Hakika, ingawa hataamka ampe kwa sababu yeye ni rafiki
yake, lakini, kwa sababu ya huyo mtu kuendelea kumwomba, ataamka ampe chochote
anachohitaji.
9 Kwa hiyo, ombeni, nanyi mtapewa, tafuteni, nanyi mtapata,
bisheni nanyi mtafunguliwa.
10 Maana yeyote aombaye hupewa, atafutaye hupata na
abishaye hufunguliwa.
11 Mtoto akimwomba baba yake samaki, je, atampa nyoka
badala ya samaki?
12 Na kama
akimwomba yai, je, atampa ng`e?
13 Ninyi,
ingawa ni waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri. Basi, baba yenu wa
mbinguni atafanya zaidi; atawapa Roho Mtakatifu wale wanaomwomba."
14 Siku
moja Yesu alikuwa anamfukuza pepo aliyemfanya mtu mmoja kuwa bubu. Basi, huyo
pepo alipomtoka, yule mtu akaweza kuongea hata umati wa watu ukashangaa.
15 Lakini
baadhi ya watu hao wakasema, "Anamfukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli,
mkuu wa pepo."
16
Wengine, wakimjaribu, wakamtaka afanye ishara kuonyesha kama alikuwa na idhini
kutoka mbinguni.
17 Lakini
yeye, akiwa anayajua mawazo yao, akawaambia, "Ufalme wowote uliofarakana
wenyewe, hauwezi kudumu; kadhalika, jamaa yeyote inayofarakana huangamia.
18 Kama
Shetani anajipinga mwenyewe, utawala wake utasimamaje? Mnasemaje, basi, kwamba
ninawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli?
19 Kama
ninafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, watoto wenu huwafukuza kwa uwezo wa
nani? Kwa sababu hiyo, wao ndio watakaowahukumu ninyi.
20 Lakini
ikiwa ninawafukuza pepo kwa uwezo wa Mungu, basi jueni kwamba Ufalme wa Mungu
umekwisha fika kwenu.
21
"Mtu mwenye nguvu anapolinda jumba lake kwa silaha, mali yake yote iko
salama.
22 Lakini
akija mwenye nguvu zaidi akamshambulia na kumshinda, huyo huziteka silaha zake
alizotegemea na kugawanya nyara.
23 Yeyote
asiyejiunga nami, ananipinga; na yeyote asiyekusanya pamoja nami, hutawanya.
24
"Pepo mchafu akifukuzwa kwa mtu fulani, huzururazurura jangwani akitafuta
mahali pa kupumzikia. Asipopata, hujisemea: `Nitarudi kwenye makao yangu
nilikotoka.`
25
Anaporudi, huikuta ile nyumba imefagiwa na kupambwa.
26 Basi,
huenda na kuwachukua pepo wengine saba waovu zaidi kuliko yeye; wote huenda na
kumwingia mtu yule. Hivyo, basi hali ya mtu huyo sasa huwa mbaya zaidi kuliko
pale mwanzo."
27
Alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katika lile kundi la watu, akasema kwa
sauti kubwa: "Heri tumbo lililokuzaa, na maziwa yaliyokunyonyesha!"
28 Lakini
Yesu akasema, "Lakini heri zaidi wale wanaolisikia neno la Mungu na
kulishika."
29 Umati
wa watu ulipozidi kuongezeka, Yesu akawaambia, "Kizazi hiki ni kizazi
kiovu. Kinataka ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ya Yona.
30 Jinsi
Yona alivyokuwa ishara kwa watu wa Ninewi, ndivyo pia Mwana wa Mtu atakavyokuwa
ishara kwa kizazi hiki.
31 Malkia
wa kusini atatokea wakati kizazi hiki kitakapohukumiwa, naye atashuhudia kwamba
kina hatia. Yeye alisafiri kutoka mbali, akaja kusikiliza maneno ya hekima ya
Solomoni; kumbe hapa pana mkuu zaidi kuliko Solomoni.
32 Watu wa
Ninewi watatokea wakati kizazi hiki kitakapohukumiwa, na watashuhudia kwamba
kizazi hiki kina hatia. Hao watu wa Ninewi walitubu kwa sababu ya mahubiri ya
Yona; na hapa pana mkuu zaidi kuliko Yona!
33
"Hakuna mtu anayewasha taa na kuifunika kwa pishi, bali huiweka juu ya
kinara ili watu wanaoingia ndani wapate kuona mwanga.
34 Jicho
lako ni kama taa ya mwili wako; likiwa zima, mwili wako wote utakuwa katika
mwanga. Jicho lako likiwa bovu, na mwili wako pia utakuwa katika giza.
35 Uwe
mwangalifu basi mwanga ulio ndani yako usije ukawa giza.
36 Basi,
kama mwili wako wote una mwanga, bila kuwa na sehemu yoyote yenye giza, mwili
huo utang`aa kikamilifu kama vile taa inavyokuangazia kwa mwanga wake."
37 Yesu
alipokuwa akiongea, Mfarisayo mmoja alimkaribisha chakula nyumbani kwake, naye
akaenda, akaketi kula chakula.
38 Huyo
Mfarisayo alistaajabu kuona kwamba alikula chakula bila kunawa.
39 Bwana
akamwambia, "Ninyi Mafarisayo huosha kikombe na sahani kwa nje, lakini
ndani mmejaa udhalimu na uovu.
40
Wapumbavu ninyi! Je, aliyetengeneza nje si ndiye aliyetengeneza ndani
pia?
41 Toeni kwa maskini vile vitu vilivyomo ndani, na vingine
vyote vitakuwa halali kwenu.
42 "Lakini ole wenu Mafarisayo, kwa sababu mnatoza
watu zaka hata juu ya majani ya kukolezea chakula, mchicha na majani mengine,
na huku hamjali juu ya haki na upendo kwa Mungu. Mambo haya iliwapasa muwe
mmeyazingatia bila kuyasahau yale mengine.
43 "Ole wenu ninyi Mafarisayo, kwa sababu mnapenda
kuketi mbele mahali pa heshima katika masunagogi, na kusalimiwa kwa heshima
hadharani.
44 Ole wenu, kwa sababu mko kama makaburi yaliyofichika;
watu hutembea juu yake bila kufahamu."
45 Mmoja wa walimu wa Sheria akamwambia, "Mwalimu,
maneno yako yanatukashifu na sisi pia."
46 Yesu akamjibu, "Na ninyi walimu wa Sheria, ole
wenu; maana mnawatwika watu mizigo isiyochukulika, huku ninyi wenyewe hamnyoshi
hata kidole kuwasaidia.
47 Ole wenu, kwa kuwa mnajenga makaburi ya manabii wale
ambao wazee wenu waliwaua.
48 Kwa hiyo mnashuhudia na kukubaliana na matendo ya wazee
wenu; maana wao waliwaua hao manabii, nanyi mnajenga makaburi yao.
49 Kwa hiyo, Hekima ya Mungu ilisema hivi: `Nitawapelekea
manabii na mitume, lakini watawaua baadhi yao, na kuwatesa wengine.`
50 Matokeo yake ni kwamba kizazi hiki kitaadhibiwa kwa
sababu ya damu ya manabii wote iliyomwagika tangu mwanzo wa ulimwengu;
51 tangu kumwagwa damu ya Abeli mpaka kifo cha Zakariya
ambaye walimuua kati ya madhabahu na mahali patakatifu. Naam, hakika kizazi
hiki kitaadhibiwa kwa matendo haya.
52 "Ole wenu ninyi walimu wa Sheria, kwa sababu
mmeuficha ule ufunguo wa mlango wa elimu; ninyi wenyewe hamkuingia na mmewazuia
waliokuwa wanaingia wasiingie."
53 Alipokuwa akitoka pale, wale Mafarisayo na walimu wa
Sheria wakaanza kumshambulia vikali na kumsonga kwa maswali mengi
54 ili wapate kumnasa kwa maneno yake.
|