Chapter 12
1 Wakati watu kwa maelfu walipokuwa wamekusanyika hata wakawa
wanakanyagana, Yesu aliwaambia kwanza wanafunzi wake, "Jihadharini na
chachu ya Mafarisayo, yaani unafiki.
2 Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, kila kilichofichika
kitafichuliwa.
3 Kwa hiyo, kila mliyosema gizani, watu watayasikia katika
mwanga, na kila mliyonong`ona faraghani milango imefungwa, yatatangazwa juu ya
nyumba.
4 "Nawaambieni ninyi rafiki zangu: msiwaogope wale
wanaoua mwili, wasiweze kufanya kitu kingine zaidi.
5 Nitawaonyesheni yule ambaye ni lazima kumwogopa:
mwogopeni yule ambaye baada ya kuua ana uwezo wa kumtupa mtu katika moto wa
Jehanamu. Naam, ninawaambieni, mwogopeni huyo.
6 Inajulikana kwamba shomoro watano huuzwa kwa senti kumi,
au sivyo? Lakini mbele ya Mungu hasahauliki hata mmoja.
7 Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote.
Msiogope, basi, ninyi mna thamani zaidi kuliko shomoro wengi!
8 "Nawaambieni kweli, kila mtu anayekiri hadharani
kwamba yeye ni wangu, Mwana wa Mtu naye atakiri mbele ya malaika wa Mungu
kwamba mtu huyo ni wake.
9 Lakini, mtu yeyote anayenikana mbele ya watu, naye
atakanwa mbele ya malaika wa Mungu.
10 "Yeyote anayesema neno la kumpinga Mwana wa Mtu
atasamehewa; lakini anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa.
11 "Watakapowapeleka ninyi mbele ya masunagogi na
mbele ya wakuu na watawala msiwe na wasiwasi juu ya jinsi mtakavyojitetea au
jinsi mtakavyosema.
12 Kwa maana wakati huo Roho Mtakatifu atawafundisheni kile
mnachopaswa kusema."
13 Mtu mmoja katika ule umati wa watu akamwambia,
"Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane urithi aliotuachia baba."
14 Yesu akamjibu, "Rafiki, ni nani aliyeniweka mimi
mwamuzi au msuluhishi kati yenu?"
15 Basi, akawaambia wote, "Jihadharini na kila aina ya
tamaa; maana uzima wa mtu hautegemei wingi wa vitu alivyo navyo."
16 Kisha akawaambia mfano: "Kulikuwa na tajiri mmoja
ambaye shamba lake lilizaa mavuno mengi.
17 Tajiri huyo akafikiri moyoni mwake: `Nitafanyaje nami
sina mahali pa kuhifadhia mavuno yangu?
18 Nitafanya hivi: nitabomoa ghala zangu na kujenga kubwa
zaidi, na humo nitahifadhi mavuno yangu yote na mali yangu.
19 Hapo nitaweza kuiambia roho yangu: sasa unayo akiba ya
matumizi kwa miaka na miaka. Ponda mali, ule, unywe na kufurahi.`
20 Lakini Mungu akamwambia: `Mpumbavu wewe; leo usiku roho
yako itachukuliwa. Na vitu vile vyote ulivyojilundikia vitakuwa vya
nani?"`
21 Yesu akamaliza kwa kusema "Ndivyo ilivyo kwa mtu
anayejilundikia mali kwa ajili yake mwenyewe, lakini si tajiri mbele ya
Mungu."
22 Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Kwa sababu
hiyo nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula mnachohitaji ili kuishi,
wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu.
23 Kwa sababu uzima ni bora kuliko chakula, na mwili ni
bora kuliko mavazi.
24 Chukueni kwa mfano, kunguru: hawapandi, hawavuni wala
hawana ghala yoyote. Hata hivyo, Mungu huwalisha. Ninyi mna thamani zaidi
kuliko ndege!
25 Ni nani kati yenu kwa kuwa na wasiwasi anaweza kuongeza
urefu wa maisha yake?
26 Basi, kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa
nini kuwa na wasiwasi juu ya yale mengine?
27 Angalieni maua jinsi yanavyomea. Hayafanyi kazi wala
hayafumi. Hata hivyo, nawahakikishieni kwamba hata Solomoni mwenyewe na fahari
zake zote hakupata kuvikwa vizuri kama ua mojawapo.
28 Lakini, kama Mungu hulivika vizuri jani la shambani
ambalo leo liko na kesho latupwa motoni, je, hatawafanyia ninyi zaidi? Enyi
watu wenye imani haba!
29 "Basi, msivurugike akili, mkihangaika daima juu ya
mtakachokula au mtakachokunywa.
30 Kwa maana hayo yote ndiyo yanayohangaikiwa na watu
wasiomjua Mungu. Baba yenu anajua kwamba mnahitaji vitu hivyo.
31 Shughulikieni kwanza Ufalme wa Mungu, na hayo yote
mtapewa kwa ziada.
32 "Msiogope, enyi kundi dogo! Maana Baba yenu
amependa kuwapeni Ufalme.
33 Uzeni mali yenu mkawape maskini misaada. Jifanyieni
mifuko isiyochakaa, na jiwekeeni hazina mbinguni ambako haitapungua. Huko wezi
hawakaribii, wala nondo hawaharibu.
34 Pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako.
35 "Muwe tayari! Jifungeni mkanda kiunoni, na taa zenu
ziwe zinawaka;
36 muwe kama watumishi wanaomngojea bwana wao arudi kutoka
arusini, ili wamfungulie mara atakapobisha hodi.
37 Heri yao watumishi wale ambao bwana wao atakaporudi
atawakuta wanakesha! Nawaambieni hakika, huyo bwana atajifunga mkanda kiunoni,
atawaketisha mezani na kuwahudumia.
38 Heri yao watumishi hao ikiwa bwana wao atawakuta
wanakesha hata ikiwa atarudi usiku wa manane au alfajiri.
39 Jueni kwamba, kama mwenye nyumba angejua saa ambayo mwizi
atakuja, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe.
40 Nanyi, kadhalika muwe tayari, maana Mwana wa Mtu atakuja
saa msiyoitazamia."
41 Petro akamwambia, "Bwana, mfano huo ni kwa ajili
yetu tu, au ni kwa ajili ya watu wote?"
42 Bwana akajibu, "Ni nani basi, mtumishi aliye
mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya watumishi wake
ili awape chakula wakati ufaao?
43 Heri yake mtumishi huyo ikiwa bwana wake atakaporudi
atamkuta akifanya hivyo.
44 Hakika atampa madaraka juu ya mali yake yote.
45 Lakini, kama mtumishi huyo atafikiri moyoni mwake: na
kusema: `Bwana wangu amekawia sana kurudi` halafu aanze kuwapiga watumishi
wenzake, wa kiume au wa kike, na kula, kunywa na kulewa,
46 bwana wake atarudi siku asiyoitazamia na saa asiyoijua;
atamkatilia mbali na kumweka fungu moja na wasioamini.*fb*
47 Mtumishi ambaye anajua matakwa ya bwana wake lakini
hajiweki tayari kufanya anavyotakiwa, atapigwa sana.
48 Lakini yule afanyaye yanayostahili adhabu bila kujua,
atapigwa kidogo. Aliyepewa vingi atatakiwa vingi; aliyekabidhiwa vingi zaidi
atatakiwa kutoa vingi zaidi.
49 "Nimekuja kuwasha moto duniani, laiti ungekuwa
umewaka tayari!
50 Ninao ubatizo ambao inanipasa niupokee; jinsi gani
ninavyohangaika mpaka ukamilike!
51 Mnadhani nimekuja kuleta amani duniani? Hata kidogo; si
amani bali utengano.
52 Na tangu sasa, jamaa ya watu watano itagawanyika; watatu
dhidi ya wawili, na wawili dhidi ya watatu.
53 Baba atakuwa dhidi ya mwanawe, mwana dhidi ya baba yake;
mama dhidi ya bintiye, binti dhidi ya mama yake; mama mkwe dhidi ya mke wa
mwanawe na huyo dhidi ya mama mkwe wake."
54 Yesu akayaambia tena makundi ya watu, "Mnapoona
mawingu yakitokea upande wa magharibi, mara mwasema: `Mvua itanyesha`, na kweli
hunyesha.
55 Mnapoona upepo wa kusi unavuma, mwasema `Kutakuwa na
hali ya joto` na ndivyo inavyokuwa.
56 Enyi wanafiki! Mnajua kutabiri hali ya hewa kwa
kuangalia dunia na anga; kwa nini basi, hamwezi kujua maana ya nyakati hizi?
57 "Na kwa nini hamwezi kujiamulia wenyewe jambo jema
la kufanya?
58 Maana kama mshtaki wako anakupeleka mahakamani, ingekuwa
afadhali kwako kupatana naye mkiwa bado njiani, ili asije akakupeleka mbele ya
hakimu, naye hakimu akakutoa kwa polisi, nao wakakutia ndani.
59 Hakika hutatoka huko nakwambia, mpaka utakapomaliza
kulipa senti ya mwisho."
|