Chapter 13
1 Wakati huo watu fulani walikuja, wakamweleza Yesu juu ya
watu wa Galilaya ambao Pilato alikuwa amewaua wakati walipokuwa wanachinja
wanyama wao wa tambiko.
2 Naye Yesu akawaambia, "Mnadhani Wagalilaya hao
walikuwa wahalifu zaidi kuliko Wagalilaya wengine, ati kwa sababu wameteseka
hivyo?
3 Nawaambieni hakika sivyo; lakini nanyi, hali kadhalika,
msipotubu, mtaangamia kama wao.
4 Au wale kumi na wanane walioangukiwa na mnara kule
Siloamu wakafa; mnadhani wao walikuwa wakosefu zaidi kuliko wengine wote
walioishi Yerusalemu?
5 Nawaambieni sivyo; lakini nanyi msipotubu, mtaangamia
kama wao."
6 Kisha, Yesu akawaambia mfano huu: "Mtu mmoja alikuwa
na mtini katika shamba lake. Mtu huyu akaenda akitaka kuchuma matunda yake,
lakini akaukuta haujazaa hata tunda moja.
7 Basi, akamwambia mfanyakazi wake: `Angalia! Kwa miaka
mitatu nimekuwa nikija kuchuma matunda ya mtini huu, nami nisiambulie kitu.
Ukate! Kwa nini uitumie ardhi bure?`
8 Lakini naye akamjibu: `Bwana, tuuache tena mwaka huu;
nitauzungushia mtaro na kuutilia mbolea.
9 Kama ukizaa matunda mwaka ujao, vema; la sivyo, basi
utaweza kuukata."`
10 Yesu alikuwa akifundisha katika sunagogi moja siku ya
Sabato.
11 Na hapo palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa mgonjwa kwa
miaka kumi na minane kutokana na pepo aliyekuwa amempagaa. Kwa sababu hiyo,
mwili wake ulikuwa umepindika vibaya hata asiweze kusimama wima.
12 Yesu alipomwona, alimwita, akamwambia, "Mama,
umeponywa ugonjwa wako."
13 Akamwekea mikono, na mara mwili wake ukawa wima tena,
akawa anamtukuza Mungu.
14 Lakini mkuu wa sunagogi alikasirika kwa sababu Yesu
alikuwa amemponya siku ya Sabato. Hivyo akawaambia wale watu walikusanyika
pale, "Mnazo siku sita za kufanya kazi. Basi, fikeni siku hizo mkaponywe
magonjwa yenu; lakini msije siku ya Sabato."
15 Hapo Bwana akamjibu, "Enyi wanafiki! Nani kati yenu
hangemfungua ng`ombe au punda wake kutoka zizini ampeleke kunywa maji, hata
kama siku hiyo ni ya Sabato?
16 Sasa, hapa yupo binti wa Abrahamu ambaye Shetani
alimfanya kilema kwa muda wa miaka kumi na minane. Je, haikuwa vizuri
kumfungulia vifungo vyake siku ya Sabato?"
17 Alipokwisha sema hayo, wapinzani wake waliona aibu
lakini watu wengine wote wakajaa furaha kwa sababu ya mambo yote aliyotenda.
18 Yesu akauliza: "Ufalme wa Mungu unafanana na nini?
Nitaulinganisha na nini?
19 NI kama mbegu ya haradali aliyotwaa mtu mmoja na
kuipanda shambani mwake; ikaota hata ikawa mti. Ndege wa angani wakajenga viota
vyao katika matawi yake."
20 Tena akauliza: "Nitaulinganisha Ufalme wa Mungu na
nini?
21 Ni kama chachu aliyoitwaa mama mmoja na kuichanganya
pamoja na unga debe moja kisha unga wote ukaumuka wote."
22 Yesu alindelea na safari yake kwenda Yerusalemu huku
akipitia mijini na vijijini, akihubiri.
23 Mtu mmoja akamwuliza, "Je, Mwalimu, watu
watakaookoka ni wachache?"
24 Yesu akawaambia, "Jitahidini kuingia kwa kupitia
mlango mwembamba; maana nawaambieni, wengi watajaribu kuingia lakini
hawataweza.
25 "Wakati utakuja ambapo mwenye nyumba atainuka na
kufunga mlango. Ninyi mtasimama nje na kuanza kupiga hodi mkisema: `Bwana,
tufungulie mlango.` Lakini yeye atawajibu: `Sijui mmetoka wapi.`
26 Nanyi mtaanza kumwambia: `Sisi ndio wale tuliokula na
kunywa pamoja nawe; na wewe ulifundisha katika vijiji vyetu.`
27 Lakini yeye atasema: `Sijui ninyi mmetoka wapi; ondokeni
mbele yangu, enyi nyote watenda maovu.`
28 Ndipo mtakuwa na kulia na kusaga meno, wakati
mtakapowaona Abrahamu, Isaka na Yakobo, na manabii wote wapo katika Ufalme wa
Mungu, lakini ninyi wenyewe mmetupwa nje!
29 Watu watakuja kutoka mashariki na magharibi, kutoka
kaskazini na kusini, watakuja na kukaa kwenye karamu katika Ufalme wa Mungu.
30 Naam, wale walio wa mwisho watakuwa wa kwanza; na wale
walio wa kwanza watakuwa wa mwisho."
31 Wakati huohuo, Mafarisayo na watu wengine walimwendea
Yesu wakamwambia, "Ondoka hapa uende mahali pengine, kwa maana Herode anataka
kukuua."
32 Yesu akawajibu, "Nendeni mkamwambie huyo mbweha
hivi: `Leo na kesho ninafukuza pepo na kuponya wagonjwa, na siku ya tatu
nitakamilisha kazi yangu.`
33 Hata hivyo, kwa leo, kesho na kesho kutwa, ni lazima niendelee
na safari yangu, kwa sababu si sawa nabii auawe nje ya Yerusalemu.
34
"Yerusalemu! We Yerusalemu! Unawaua manabii na kuwapiga mawe wale
waliotumwa kwako! Mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako pamoja kama kuku
anavyokusanya vifaranga vyake chini ya mabawa yake, Lakini wewe umekataa.
35 Haya,
utaachiwa mwenyewe nyumba yako. Naam, hakika nawaambieni, hamtaniona mpaka
wakati utakapofika mseme: `Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana."`
|