Chapter 18
1 Basi,
Yesu aliwasimulia mfano kuonyesha kwamba ni lazima kusali daima bila kukata
tamaa.
2 Alisema:
"Katika mji mmoja kulikuwa na hakimu ambaye hakuwa anamcha Mungu wala
kumjali binadamu.
3 Katika
mji huohuo, kulikuwa pia na mama mmoja mjane, ambaye alimwendea huyo hakimu
mara nyingi akimwomba amtetee apate haki yake kutoka kwa adui yake.
4 Kwa muda
mrefu huyo hakimu hakupenda kumtetea huyo mjane; lakini, mwishowe akajisemea:
`Ingawa mimi simchi Mungu wala simjali binadamu,
5 lakini
kwa vile huyu mjane ananisumbua, nitamtetea; la sivyo ataendelea kufika hapa,
na mwisho atanichosha kabisa!"`
6 Basi,
Bwana akaendelea kusema, "Sikieni jinsi alivyosema huyo hakimu mbaya.
7 Je, ndio
kusema Mungu hatawatetea wale aliowachagua, ambao wanamlilia mchana na usiku?
Je, atakawia kuwasikiliza?
8
Nawaambieni atawatetea upesi. Hata hivyo, je, kutakuwako na imani duniani
wakati Mwana wa Mtu atakapokuja?"
9 Halafu
Yesu aliwaambia pia mfano wa wale ambao walijiona kuwa wema na kuwadharau
wengine.
10
"Watu wawili walipanda kwenda Hekaluni kusali: mmoja Mfarisayo, na
mwingine mtoza ushuru.
11 Huyo
Mfarisayo akasimama, akasali kimoyomoyo: `Ee Mungu, nakushukuru kwa vile mimi
si kama watu wengine: walafi, wadanganyifu au wazinzi. Nakushukuru kwamba mimi
si kama huyu mtoza ushuru.
12 Nafunga
mara mbili kwa juma, natoa zaka sehemu ya kumi ya pato langu.`
13 Lakini
yule mtoza ushuru, akiwa amesimama kwa mbali bila hata kuinua macho yake
mbinguni, ila tu akijipiga kifua kwa huzuni, alisema: `Ee Mungu, unionee huruma
mimi mwenye dhambi.`
14
Nawaambieni, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amesamehewa. Lakini yule
mwingine, sivyo. Kwa maana kila anayejikweza atashushwa, na kila anayejishusha
atakwezwa."
15 Watu
walimletea Yesu watoto wadogo ili awawekee mikono yake. Wanafunzi walipowaona,
wakawazuia kwa maneno makali.
16 Lakini
Yesu akawaita kwake akisema: "Waacheni hao watoto waje kwangu, wala
msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu kama hawa.
17
Nawaambieni kweli, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo,
hataingia katika Ufalme huo."
18
Kiongozi mmoja, Myahudi, alimwuliza Yesu, "Mwalimu mwema, nifanye nini ili
niweze kuupata uzima wa milele?"
19 Yesu
akamwambia, "Mbona waniita mwema? Hakuna aliye mwema ila Mungu peke yake.
20
Unazijua amri: `Usizini; usiue; usiibe; usitoe ushahidi wa uongo; waheshimu
baba yako na mama yako."`
21 Yeye
akasema, "Hayo yote nimeyazingatia tangu ujana wangu."
22 Yesu
aliposikia hayo akamwambia, "Unatakiwa bado kufanya kitu kimoja: uza kila
ulicho nacho, wagawie maskini, na hivyo utakuwa na hazina yako mbinguni; halafu
njoo unifuate."
23 Lakini
huyo mtu aliposikia hayo, alihuzunika sana kwa sababu alikuwa tajiri sana.
24 Yesu
alipoona akihuzunika hivyo, akasema, "Jinsi gani ilivyo vigumu kwa
matajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu!
25 Naam,
ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko tajiri
kuingia katika Ufalme wa Mungu."
26 Wale
watu waliposikia hayo, wakasema, "Nani basi, atakayeokolewa?"
27 Yesu
akajibu, "Yasiyowezekana kwa binadamu, yanawezekana kwa Mungu."
28 Naye
Petro akamwuliza, "Na sisi je? Tumeacha vitu vyote tukakufuata!"
29 Yesu
akawaambia, "Kweli nawaambieni, mtu yeyote aliyeacha nyumba au mke au kaka
au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu,
30
atapokea mengi zaidi wakati huu wa sasa, na kupokea uzima wa milele wakati
ujao."
31 Yesu
aliwachukua kando wale kumi na wawili, akawaambia, "Sikilizeni! Tunakwenda
Yerusalemu na huko kila kitu kilichoandikwa na manabii kuhusu Mwana wa Mtu
kitakamilishwa.
32 Kwa
maana atakabidhiwa kwa watu wa mataifa nao watamtendea vibaya na kumtemea mate.
33
Watampiga mijeledi, watamuua; lakini siku ya tatu atafufuka."
34 Lakini
wao hawakuelewa hata kidogo jambo hilo; walikuwa wamefichwa maana ya maneno
hayo, na hawakutambua yaliyosemwa.
35 Wakati
Yesu alipokaribia Yeriko, kulikuwa na mtu mmoja kipofu ameketi njiani akiomba.
36
Aliposikia umati wa watu ukipita aliuliza, "Kuna nini?"
37 Wakamwambia, "Yesu wa Nazareti anapita."
38 Naye akapaza sauti akisema, "Yesu, Mwana wa Daudi,
nihurumie!"
39 Wale watu waliotangulia wakamkemea wakimwambia anyamaze;
lakini yeye akazidi kupaza sauti: "Mwana wa Daudi, nihurumie;"
40 Yesu alisimama, akaamuru wamlete mbele yake. Yule kipofu
alipofika karibu, Yesu akamwuliza,
41 "Unataka nikufanyie nini?" Naye akamjibu,
"Bwana, naomba nipate kuona tena."
42 Yesu akamwambia, "Ona! Imani yako imekuponya."
43 Na mara yule aliyekuwa kipofu akapata kuona, akamfuata
Yesu akimtukuza Mungu. Watu wote walipoona hayo, wakamsifu Mungu.
|