Chapter 19
1 Yesu aliingia mjini Yeriko, akawa anapita katika njia za
mji huo.
2 Kulikuwa na mtu mmoja mjini, jina lake Zakayo ambaye
alikuwa mkuu wa watoza ushuru tena mtu tajiri.
3 Alitaka kuona Yesu alikuwa nani, lakini kwa sababu ya
umati wa watu, na kwa vile alikuwa mfupi, hakufaulu.
4 Hivyo, alitangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu ili aweze
kumwona Yesu, kwa maana alikuwa apitie hapo.
5 Basi, Yesu alipofika mahali pale, aliangalia juu
akamwambia, "Zakayo, shuka upesi, maana leo ni lazima nishinde nyumbani
mwako."
6 Zakayo akashuka haraka, akamkaribisha kwa furaha.
7 Watu wote walipoona hayo, wakaanza kunung`unika wakisema,
"Amekwenda kukaa kwa mtu mwenye dhambi."
8 Lakini Zakayo akasimama akamwambia Yesu, "Sikiliza
Bwana! Mimi nitawapa maskini nusu ya mali yangu, na kama nimenyang`anya mtu
yeyote kitu, nitamrudishia mara nne."
9 Yesu akamwambia, "Leo wokovu umefika katika nyumba
hii, kwa vile huyu pia ni wa ukoo wa Abrahamu.
10 Kwa maana Mwana wa Mtu amekuja kutafuta na kuokoa
waliopotea." ic
11 Wakati watu walipokuwa bado wanasikiliza hayo, Yesu
akawaambia mfano. (Hapo alikuwa anakaribia Yerusalemu, na watu wale walidhani
kwamba muda si muda, Ufalme wa Mungu ungefika.)
12 Hivyo akawaambia, "Kulikuwa na mtu mmoja wa ukoo wa
kifalme aliyefanya safari kwenda nchi ya mbali ili apokee madaraka ya ufalme,
halafu arudi.
13 Basi, kabla ya kuondoka aliwaita watumishi wake kumi,
akawapa kiasi cha fedha kila mmoja na kumwambia: `Fanyeni nazo biashara mpaka
nitakaporudi.`
14 Lakini wananchi wenzake walimchukia na hivyo wakatuma
wajumbe waende wakaseme: `Hatumtaki huyu atutawale.`
15 "Huyo mtu mashuhuri alirudi nyumbani baada ya
kufanywa mfalme, na mara akaamuru wale watumishi aliowapa zile fedha waitwe ili
aweze kujua kila mmoja amepata faida gani.
16 Mtumishi wa kwanza akatokea, akasema: `Mheshimiwa, faida
iliyopatikana ni mara kumi ya zile fedha ulizonipa.`
17 Naye akamwambia: `Vema; wewe ni mtumishi mwema. Kwa kuwa
umekuwa mwaminifu katika jambo dogo, utakuwa na madaraka juu ya miji kumi!`
18 Mtumishi wa pili akaja, akasema: `Mheshimiwa, faida
iliyopatikana ni mara tano ya zile fedha ulizonipa.`
19 Naye akamwambia pia: `Nawe utakuwa na madaraka juu ya
miji mitano.`
20 "Mtumishi mwingine akaja, akasema: `Chukua fedha
yako; niliificha salama katika kitambaa,
21 kwa maana niliogopa kwa sababu wewe ni mtu mkali. Wewe
ni mtu ambaye huchukua yasiyo yako, na huchuma ambacho hukupanda.`
22 Naye akamwambia: `Nakuhukumu kutokana na msemo wako, ewe
mtumishi mbaya! Ulijua kwamba mimi ni mtu mkali, ambaye huchukua yasiyo yangu
na kuchuma nisichopanda.
23 Kwa nini basi, hukuiweka fedha yangu benki, nami
ningeichukua pamoja na faida baada ya kurudi kwangu?`
24 Hapo akawaambia wale waliokuwa pale: `Mnyang`anyeni hizo
fedha, mkampe yule aliyepata faida mara kumi.`
25 Nao wakamwambia: `Lakini Mheshimiwa, huyo ana faida ya
kiasi hicho mara kumi!`
26 Naye akawajibu: `Kila aliye na kitu atapewa na
kuzidishiwa. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.
27 Na sasa, kuhusu hao maadui wangu ambao hawapendi niwe
mfalme wao, waleteni hapa, mkawaue papa hapa mbele yangu."`
28 Yesu alisema hayo, kisha akatangulia mbele yao kuelekea
Yerusalemu.
29 Alipokaribia kufika Bethfage na Bethania, karibu na
mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili,
30 akawaambia: "Nendeni katika kijiji kilicho mbele
yenu. Mtakapokuwa mnaingia kijijini, mtamkuta mwana punda amefungwa ambaye
hajatumiwa na mtu. Mfungeni, mkamlete hapa.
31 Kama mtu akiwauliza, kwa nini mnamfungua, mwambieni,
`Bwana ana haja naye."`
32 Basi, wakaenda, wakakuta sawa kama alivyowaambia.
33 Walipokuwa wanamfungua yule mwana punda, wenyewe
wakawauliza, "Kwa nini mnamfungua mwana punda huyu?"
34 Nao wakawajibu, "Bwana anamhitaji."
35 Basi, wakampelekea Yesu yule mwana punda. Kisha
wakatandika mavazi yao juu yake wakampandisha Yesu.
36 Yesu akaendelea na safari, na watu wakatandaza mavazi
yao barabarani.
37 Alipofika karibu na Yerusalemu, katika mteremko wa mlima
wa Mizeituni, umati wote na wanafunzi wake, wakaanza kushangilia na kumtukuza
Mungu kwa sauti kubwa, kwa sababu ya mambo makuu waliyoyaona;
38 wakawa wanasema: "Abarikiwe Mfalme ajaye kwa jina
la Bwana. Amani mbinguni, na utukufu juu mbinguni!"
39 Hapo baadhi ya Mafarisayo waliokuwako katika lile kundi
la watu, wakamwambia Yesu, "Mwalimu, wanyamazishe wanafunzi wako!"
40 Yesu akawajibu, "Nawaambieni, kama hawa
wakinyamaza, hakika hayo mawe yatapaza sauti."
41 Alipokaribia zaidi na kuuona ule mji, Yesu aliulilia
42 akisema: "Laiti ungelijua leo hii yale yaletayo
amani! Lakini sasa yamefichika machoni pako.
43 Maana siku zaja ambapo adui zako watakuzungushia maboma,
watakuzingira na kukusonga pande zote.
44 Watakupondaponda wewe pamoja na watoto wako ndani ya
kuta zako; hawatakuachia hata jiwe moja juu jingine, kwa sababu hukuutambua
wakati Mungu alipokujia kukuokoa."
45 Kisha, Yesu aliingia Hekaluni, akaanza kuwafukuzia nje
wafanyabiashara
46 akisema, "Imeandikwa: `Nyumba yangu itakuwa nyumba
ya sala`; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang`anyi."
47 Yesu akawa anafundisha kila siku Hekaluni. Makuhani
wakuu, walimu wa Sheria na viongozi wa watu walitaka kumwangamiza,
48 lakini hawakuwa na la kufanya, maana watu wote walikuwa
wakimsikiliza kwa makini kabisa.
|