Chapter 21
1 Yesu alitazama
kwa makini, akawaona matajiri walivyokuwa wanatia sadaka zao katika hazina ya
Hekalu,
2 akamwona pia
mama mmoja mjane akitumbukiza humo sarafu mbili ndogo.
3 Basi, akasema,
"Nawaambieni kweli, mama huyu mjane ametia zaidi katika hazina kuliko
wote.
4 Kwa maana,
wengine wote wametoa sadaka zao kutokana na ziada ya mali zao, lakini huyu
mama, ingawa ni maskini, ametoa kila kitu alichohitaji kwa kuishi."
5 Baadhi ya
wanafunzi walikuwa wanazungumza juu ya Hekalu, jinsi lilivyopambwa kwa mawe ya
thamani, pamoja na sadaka zilizotolewa kwa Mungu. Yesu akasema,
6 "Haya
yote mnayoyaona - zitakuja siku ambapo hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu
ya lingine; kila kitu kitaharibiwa."
7 Basi,
wakamwuliza, "Mwalimu, mambo hayo yatatokea lini? Na ni ishara gani
zitakazoonyesha kwamba karibu mambo hayo yatokee?"
8 Yesu
akawajibu, "Jihadharini, msije mkadanganyika. Maana wengi watatokea na
kulitumia jina langu wakisema: `Mimi ndiye`, na, `Wakati ule umekaribia`.
Lakini ninyi msiwafuate!
9 Basi,
mtakaposikia habari za vita na misukosuko, msitishike; maana ni lazima hayo
yatokee kwanza, lakini mwisho wa yote, bado."
10 Halafu
akaendelea kusema: "Taifa moja litapigana na taifa lingine, na ufalme
mmoja utapigana na ufalme mwingine.
11 Kila mahali
kutakuwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi, kutakuwa na njaa na tauni. Kutakuwa na
vituko vya kutisha na ishara kubwa angani.
12 Lakini kabla
ya kutokea hayo yote, watawatieni nguvuni, watawatesa na kuwapelekeni katika
masunagogi na kuwatia gerezani; mtapelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa
ajili ya jina langu.
13 Hii itawapeni
fursa ya kushuhudia Habari Njema.
14 Muwe na
msimamo huu mioyoni mwenu: hakuna kufikiria kabla ya wakati juu ya jinsi
mtakavyojitetea,
15 kwa sababu
mimi mwenyewe nitawapeni ufasaha wa maneno na hekima, hivyo kwamba zenu
hawataweza kustahimili wala kupinga.
16 Wazazi wenu,
ndugu, jamaa na rafiki zenu watawasaliti ninyi; na baadhi yenu mtauawa.
17 Watu wote
watawachukieni kwa sababu ya jina langu.
18 Lakini, hata
unywele mmoja wa vichwa vyenu hautapotea.
19 Kwa uvumilivu
wenu, mtayaokoa maisha yenu.
20
"Mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo mtambue ya
kwamba wakati umefika ambapo mji huo utaharibiwa.
21 Hapo walioko
Yudea wakimbilie milimani; wale walio mjini watoke; na wale walio mashambani
wasirudi mjini.
22 Kwa maana
siku hizo ni siku za adhabu, ili yote yaliyoandikwa yatimie.
23 Ole wao waja
wazito na wanyonyeshao siku hizo! Kwa maana kutakuwa na dhiki kubwa katika
nchi, na hasira ya Mungu itawajia watu hawa.
24 Wengine
watauawa kwa upanga, wengine watachukuliwa mateka katika nchi zote; na mji wa
Yerusalemu utakanyagwa na watu wa mataifa mengine, hadi nyakati zao
zitakapotimia.
25
"Kutakuwa na ishara katika jua na mwezi na nyota. Mataifa duniani yatakuwa
na dhiki kwa sababu ya wasiwasi kutokana na mshindo wa mawimbi ya bahari.
26 Watu
watazirai kwa sababu ya uoga, wakitazamia mambo yatakayoupata ulimwengu; kwa
maana nguvu za mbingu zitatikiswa.
27 Halafu,
watamwona Mwana wa Mtu akija katika wingu, mwenye nguvu na utukufu mwingi.
28 Wakati
mambo hayo yatakapoanza kutukia, simameni na kuinua vichwa vyenu juu, kwa maana
ukombozi wenu umekaribia."
29 Kisha akawaambia mfano: "Angalieni mtini na miti
mingine yote.
30 Mnapoona kwamba imeanza kuchipua majani, mwatambua
kwamba wakati wa kiangazi umekaribia.
31 Vivyo hivyo, mtakapoona mambo hayo yanatendeka,
mtatambua kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia.
32 Nawaambieni hakika, kizazi hiki cha sasa hakitapita
kabla ya hayo yote kutendeka.
33 Mbingu na dunia vitapita, lakini maneno yangu
hayatapita.
34 "Muwe macho, mioyo yenu isije ikalemewa na anasa,
ulevi na shughuli za maisha haya. La sivyo, Siku ile itawajieni ghafla.
35 Kwa maana itawajia kama mtego, wote wanaoishi duniani
pote.
36 Muwe waangalifu basi, na salini daima ili muweze kupata
nguvu ya kupita salama katika mambo haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele
ya Mwana wa Mtu."
37 Wakati wa mchana, siku hizo, Yesu alikuwa akifundisha
watu Hekaluni; lakini usiku alikuwa akienda katika mlima wa Mizeituni na kukaa
huko.
38 Watu wote walikuwa wanakwenda Hekaluni asubuhi na
mapema, wapate kumsikiliza.
|