Chapter 22
1 Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa chachu, iitwayo Pasaka,
ilikuwa inakaribia.
2 Makuhani wakuu na walimu wa Sheria wakawa wanatafuta njia
ya kumwua Yesu, lakini waliwaogopa watu.
3 Basi, Shetani akamwingia Yuda aitwae Iskarioti, mmoja wa
wale mitume kumi na wawili.
4 Yuda akaenda akajadiliana na makuhani wakuu na walinzi wa
Hekalu kuhusu atakavyomsaliti Yesu kwao.
5 Nao wakafurahi na kupatana naye kumlipa fedha.
6 Yuda akakubali, na akawa anatafuta nafasi nzuri ya
kumkabidhi kwao bila umati wa watu kujua.
7 Basi, siku ya Mikate Isiyotiwa chachu ikafika. Hiyo ndiyo
siku ambayo mwana kondoo wa Pasaka huchinjwa.
8 Hivyo Yesu akawatuma Petro na Yohane, akawaambia,
"Nendeni mkatuandalie karamu ili tupate kula Pasaka."
9 Nao wakamwuliza, "Unataka tuiandae wapi?"
10 Akawaambia, "Sikilizeni! Mtakapokuwa mnakwenda
mjini, mtakutana na mwanamume anayebeba mtungi wa maji. Mfuateni mpaka ndani ya
nyumba atakayoingia.
11 Mwambieni mwenye nyumba: `Mwalimu anakuuliza, kiko wapi
kile chumba ambamo nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?`
12 Naye atawaonyesheni chumba kikubwa ghorofani ambacho
kimepambwa. Andalieni humo."
13 Basi, wakaenda, wakakuta kila kitu sawa kama Yesu
alivyokuwa amewaambia; wakaandaa karamu ya Pasaka.
14 Saa ilipotimia, Yesu akakaa kula chakula pamoja na
mitume wake.
15 Akawaambia, "Nimetamani sana kula Pasaka hii pamoja
nanyi kabla ya kuteswa kwangu.
16 Maana nawaambieni, sitaila tena hadi hapo itakapokamilika
katika Ufalme wa Mungu."
17 Kisha akatwaa kikombe, akashukuru akasema,
"Pokeeni, mgawanye ninyi kwa ninyi.
18 Kwa maana nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu
mpaka Ufalme wa Mungu utakapokuja."
19 Halafu akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa
akisema, "Huu ni mwili wangu, unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa
kunikumbuka."
20 Akafanya vivyo hivyo na kikombe, baada ya chakula,
akisema, "Kikombe hiki ni agano jipya linalothibitishwa kwa damu yangu
inayomwagika kwa ajili yenu.*fd*
21 "Lakini, tazameni! Yule atakayenisaliti yuko nami
hapa mezani.
22 Kweli Mwana wa Mtu anakwenda kuuawa kama ilivyopangwa,
lakini ole wake mtu anayemsaliti."
23 Hapo wakaanza kuulizana wao kwa wao ni nani kati yao
atakayefanya jambo hilo.
24 Kulitokea ubishi kati ya hao mitume kuhusu nani miongoni
mwao anayefikiriwa kuwa mkuu zaidi kuliko wengine.
25 Yesu akawaambia, "Wafalme wa mataifa huwatawala
watu wao kwa mabavu, nao huitwa wafadhili wa watu.
26 Lakini isiwe hivyo kati yenu; bali, yule aliye mkuu kati
yenu ni lazima awe mdogo wa wote, na aliye kiongozi lazima awe kama mtumishi.
27 Kwa maana, ni nani aliye mkuu: yule anayeketi mezani
kula chakula, ama yule anayetumikia? Bila shaka ni yule anayeketi mezani kula
chakula! Hata hivyo, mimi niko hapa kati yenu kama mtumishi.
28 "Ninyi ndio mliobaki nami wakati wote wa majaribu
yangu;
29 na, kama vile Baba yangu alivyonikabidhi Ufalme, vivyo
hivyo nami nitawakabidhi ninyi Ufalme.
30 Mtakula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu, na
mtaketi katika viti vya enzi kuyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.
31 "Simoni, Simoni! Sikiliza! Shetani alitaka
kuwapepeta ninyi kama mtu anavyopepeta ngano.
32 Lakini mimi nimekuombea ili imani yako isipungue. Nawe
utakaponirudia, watie moyo ndugu zako."
33 Naye Petro akamjibu, "Bwana, mimi niko tayari
kwenda pamoja nawe gerezani, na hata kufa."
34 Yesu akamjibu, "Nakwambia wewe Petro, kabla jogoo
hajawika leo utakuwa umenikana mara tatu."
35 Kisha, Yesu akawauliza wanafunzi wake, "Wakati
nilipowatuma bila mfuko wa fedha wala mkoba wala viatu, mlitindikiwa
chochote?" Wakajibu, "La."
36 Naye akawaambia, "Lakini sasa, yule aliye na mfuko
wa fedha auchukue; na aliye na mkoba, hali kadhalika. Na yeyote asiye na upanga, auze koti lake
anunue mmoja.
37 Maana
nawaambieni, haya maneno ya Maandiko Matakatifu: `Aliwekwa kundi moja na
wahalifu,` ni lazima yatimie. Naam, yale yanayonihusu yanafikia ukamilifu
wake."
38 Nao
wakasema, "Bwana, tazama; hapa kuna panga mbili." Naye akasema,
"Basi!"
39 Yesu
akatoka, na kama ilivyokuwa desturi yake, akaenda katika mlima wa Mizeituni;
wanafunzi wake wakamfuata.
40 Alipofika
huko akawaambia, "Salini, msije mkaingia katika kishawishi."
41 Kisha
akawaacha, akaenda umbali wa mtu kuweza kutupa jiwe, akapiga magoti, akasali:
42
"Baba, kama wapenda, ukiondoe kwangu kikombe hiki; hata hivyo, mapenzi
yako yatimizwe, wala siyo yangu."
43 Hapo,
malaika kutoka mbinguni, akamtokea ili kumtia moyo.
44 Akiwa
katika uchungu mkubwa, alisali kwa bidii zaidi; na jasho likamtoka, kama matone
ya damu, likatiririka mpaka chini.*fe* ic
45 Baada
ya kusali, aliwarudia wanafunzi wake, akawakuta wamelala, kwani walikuwa na
huzuni.
46
Akawaambia, "Mbona mnalala? Amkeni msali, msije mkaingia katika
kishawishi."
47
Alipokuwa bado anaongea, kundi la watu likaja likiongozwa na yule aliyeitwa
Yuda, mmoja wa wale mitume kumi na wawili. Yuda akaenda kumsalimu Yesu kwa
kumbusu.
48 Lakini
Yesu akamwambia, "Yuda! Je, unamsaliti Mwana wa Mtu kwa kumbusu?"
49 Wale
wanafunzi wake walipoona hayo wakasema, "Bwana, tutumie panga zetu?"
50 Na
mmoja wao akampiga upanga mtumishi wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio lake la
kulia.
51 Hapo,
Yesu akasema, "Acha! Hii inatosha." Akaligusa sikio la mtu huyo
akaliponya.
52 Kisha
Yesu akawaambia makuhani wakuu, wakubwa wa walinzi wa Hekalu na wazee waliokuja
kumkamata: "Je, mmekuja na mapanga na marungu kunikamata kana kwamba mimi
ni mnyang`anyi?
53
Nilipokuwa pamoja nanyi kila siku Hekaluni hamkunitia nguvuni. Lakini, huu ndio
wakati wenu hasa, ndio wakati wa utawala wa giza."
54 Basi,
wakamkamata, wakamchukua na kwenda naye nyumbani kwa Kuhani Mkuu. Petro akawa
anamfuata nyuma kwa mbali.
55 Moto
ulikuwa umewashwa katikati ya ua, nao wakawa wameketi pamoja Petro akiwa
miongoni mwao.
56 Mjakazi
mmoja alipomwona Petro ameketi karibu na moto, akamkodolea macho, akasema,
"Mtu huyu alikuwa pia pamoja na Yesu."
57 Lakini
Petro akakana akisema, "Wee! simjui mimi."
58 Baadaye
kidogo, mtu mwingine akamwona Petro, akasema, "Wewe ni mmoja wao."
Lakini Petro akajibu "Bwana we; si mimi!"
59 Kama
saa moja baadaye, mtu mwingine akasisitiza, "Hakika huyu alikuwa pamoja
naye; ametoka Galilaya ati."
60 Lakini
Petro akasema, "Bwana wee; sijui hata unachosema!" Na papo hapo,
akiwa bado anaongea, jogoo akawika.
61 Bwana
akageuka na kumtazama Petro, naye Petro akakumbuka yale aliyokuwa ameambiwa na
Bwana: "Leo kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu."
62 Hapo akatoka nje, akalia sana.
63 Wale watu waliokuwa wanamchunga Yesu, walimpiga na
kumdhihaki.
64 Walimfunga kitambaa usoni, wakawa wanamwuliza, "Ni
nani aliyekupiga? Hebu bashiri tuone!"
65 Wakamtolea maneno mengi ya matusi.
66 Kulipokucha, kikao cha wazee wa watu kilifanyika,
ambacho kilihudhuriwa na makuhani wakuu na walimu wa Sheria. Yesu akaletwa
mbele ya Baraza hilo.
67 Nao wakamwambia, "Twambie! Je, wewe ndiwe
Kristo?" Lakini Yesu akawaambia, "Hata kama nikiwaambieni,
hamtasadiki;
68 na hata kama nikiwaulizeni swali, hamtanijibu.
69 Lakini tangu sasa, Mwana wa Mtu atakuwa ameketi upande
wa kulia wa Mungu Mwenyezi."
70 Hapo wote wakasema, "Ndiyo kusema wewe ni Mwana wa
Mungu?" Naye akasema, "Ninyi mnasema kwamba mimi ndiye."
71 Nao wakasema, "Je, tunahitaji ushahidi mwingine?
Sisi wenyewe tumesikia akisema kwa mdomo wake mwenyewe."sw4323
|