Chapter 23
1 Kisha, wote kwa jumla, wakasimama, wakampeleka Yesu mbele
ya Pilato.
2 Wakaanza kumshtaki wakisema: "Tulimkuta mtu huyu
akiwapotosha watu wetu, akipinga kulipa kodi kwa Kaisari na kujiita ati yeye ni
Kristo, Mfalme."
3 Pilato akamwuliza Yesu, "Wewe ni Mfalme wa
Wayahudi?" Yesu akamjibu, "Wewe umesema."
4 Pilato akawaambia makuhani wakuu na umati wa watu,
"Sioni kosa lolote katika mtu huyu."
5 Lakini wao wakasisitiza wakisema: "Anawachochea watu
kwa mafundisho yake katika nchi yote ya Yudea; alianza Galilaya, na sasa yuko
hapa."
6 Pilato aliposikia hayo, akauliza, "Je, mtu huyu ni
mwenyeji wa Galilaya?"
7 Alipojua kwamba Yesu alikuwa chini ya utawala wa Herode,
akampeleka kwa Herode, ambaye wakati huo alikuwa Yerusalemu.
8 Herode alifurahi sana alipomwona Yesu. Alikuwa amekwisha
sikia habari zake, na hivyo alikuwa anatazamia kwa muda mrefu kumwona kwa macho
yake mwenyewe. Zaidi ya hayo, alikuwa anatumaini kumwona Yesu akitenda mwujiza.
9 Basi, akamwuliza maswali mengi kwa muda mrefu, lakini
Yesu hakumjibu neno.
10 Makuhani wakuu na walimu wa Sheria wakajitokeza mbele,
wakatoa mashtaka yao kwa nguvu sana.
11 Basi, herode pamoja na maaskari wake, wakamwaibisha Yesu
na kumfanyia mzaha; kisha wakamvika vazi la kifalme, wakamrudisha kwa Pilato.
12 Herode na Pilato, ambao hapo awali walikuwa maadui,
tangu siku hiyo wakawa marafiki.
13 Basi, Pilato akaitisha mkutano wa makuhani wakuu,
viongozi na watu,
14 akawaambia, "Mmemleta mtu huyu kwangu mkisema
kwamba alikuwa anawapotosha watu. Sasa sikilizeni! Baada ya kuchunguza jambo
hilo mbele yenu, sikumpata na kosa lolote kuhusu mashtaka yenu juu yake.
15 Wala si mimi tu, bali hata Herode hakuona kosa lolote,
kwa maana amemrudisha kwangu. Ni dhahiri kwamba mtu huyu hakufanya chochote
kinachostahili adhabu ya kifo.
16 Hivyo, nitaamuru apigwe viboko, halafu
nitamwachilia."*ff* mmoja.
17 missing
18 Lakini wote wakapiga kelele pamoja: "Mwondoe huyo,
utufungulie Baraba!"
19 Baraba alikuwa ametiwa ndani kwa kusababisha uasi katika
mji na pia kwa sababu ya kuua.)
20 Pilato alitaka kumwachilia Yesu, hivyo akasema nao tena;
21 lakini wao wakapiga kelele: "Msulubishe,
msulubishe!"
22 Pilato akawaambia mara ya tatu, "Amefanya kosa
gani? Sioni kosa lolote kwake linalomstahili auawe; kwa hiyo nitampiga viboko,
halafu nimwachilie."
23 Lakini wao wakazidi kupiga kelele kwa nguvu sana, kwamba
Yesu ni lazima asulubiwe. Mwishowe, sauti zao zikashinda.
24 Basi, Pilato akaamua kwamba matakwa yao yatimizwe.
25 Akamfungua kutoka gerezani yule waliyemtaka, ambaye
alikuwa ametiwa gerezani kwa sababu ya uasi na kuua; akamtoa Yesu kwao,
wamfanyie walivyotaka.
26 Walipokuwa wakimpeleka, walikutana na mtu mmoja, aitwaye
Simoni wa Kurene, aliyekuwa anatoka shambani. Basi, walimkamata, wakamtwika ule
msalaba auchukue nyuma ya Yesu.
27 Watu, umati kwa umati, walimfuata; miongoni mwao
wakiwemo wanawake waliokuwa wanaomboleza na kumlilia.
28 Yesu akawageukia, akasema, "Enyi kina mama wa
Yerusalemu! Msinililie mimi, ila lieni kwa ajili yenu wenyewe na kwa ajili ya
watoto wenu.
29 Maana, hakika siku zitakuja ambapo watasema: `Heri yao
wale walio tasa, ambao hawakupata kuzaa wala kunyonyesha watoto!`
30 Wakati huo, ndipo watu wataanza kuiambia milima:
`Tuangukieni!` na vilima, `Tufunikeni!`
31 Kwa maana, kama watu wanautendea mti mbichi namna hiyo,
itakuwaje kwa mti mkavu?"
32 Waliwachukua pia watu wengine wawili, wahalifu, wauawe
pamoja naye.
33 Walipofika mahali paitwapo, "Fuvu la Kichwa,"
ndipo wakamsulubisha Yesu pamoja na wale wahalifu wawili, mmoja upande wake wa
kulia na mwingine upande wake wa kushoto.
34 Yesu akasema, "Baba, uwasamehe kwa maana hawajui
wanalofanya." Kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura.
35 Watu wakawa wamesimama pale wakitazama. Nao viongozi
wakamdhihaki wakisema: "Amewaokoa wengine; sasa na ajiokoe mwenyewe, kama
yeye ndiye Kristo, mteule wa Mungu!"
36 Askari nao walimdhihaki pia; walimwendea wakampa siki
37 wakisema: "Kama kweli wewe ni Mfalme wa Wayahudi,
jiokoe mwenyewe."
38 Vilevile maandishi haya yalikuwa yameandikwa na kuwekwa
juu yake: "Huyu ndiye Mfalme wa Wayahudi."
39 Mmoja wa wale wahalifu waliotundikwa msalabani,
alimtukana akisema: "Je, si kweli kwamba wewe ndiwe Kristo? Basi, jiokoe
mwenyewe, utuokoe na sisi pia."
40 Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake akisema:
"Wewe humwogopi Mungu hata kidogo? Wewe umepata adhabu hiyohiyo.
41 Wewe na mimi tunastahili, maana haya ni malipo ya yale
tuliyotenda. Lakini mtu huyu hakufanya chochote kibaya."
42 Kisha akasema, "Ee Yesu! Unikumbuke wakati
utakapoingia katika ufalme wako."
43 Yesu akamwambia, "Nakwambia kwa hakika, leo utakuwa
pamoja nami peponi."
44 Ilikuwa yapata saa sita mchana; jua likaacha kuangaza,
giza likafunika nchi yote mpaka saa tisa,
45 na pazia lililokuwa limetundikwa Hekaluni likapasuka
vipande viwili.
46 Yesu akalia kwa sauti kubwa: "Baba, naiweka roho
yangu mikononi mwako." Alipokwisha sema hayo, akakata roho. ic
47 Hapo, yule jemadari alipoona yaliyotukia akamsifu Mungu
akisema: "Hakika huyu alikuwa mtu mwema."
48 Watu wale wote waliokuwa wamekusanyika hapo kwa ajili ya
tukio hilo, walipoona hayo yaliyotukia, walirudi makwao wakijipiga vifua kwa
huzuni.
49 Marafiki zake wote pamoja na wale wanawake walioandamana
naye kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali kutazama tukio hilo.
50 Kulikuwa na mtu mmoja jina lake Yosefu, mwenyeji wa
kijiji kimoja cha Wayahudi kiitwacho Armathaya. Alikuwa mtu mwema
anayeheshimika;
51 Alikuwa akitazamia kuja kwa Ufalme wa Mungu. Ingawa
alikuwa mmoja wa Baraza kuu la Wayahudi, hakuwa amekubaliana nao katika kitendo
chao.
52 Basi, yeye alikwenda kwa Pilato, akaomba apewe mwili wa
Yesu.
53 Kisha, akaushusha mwili huo kutoka msalabani,
akauzungushia sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililokuwa limechongwa
kwenye mwamba, ambalo halikuwa limetumika.
54 Siku hiyo ilikuwa Ijumaa, na maandalio ya siku ya Sabato
yalikuwa yanaanza.
55 Wale wanawake walioandamana na Yesu kutoka Galilaya
walimfuata Yosefu, wakaliona lile kaburi na jinsi mwili wake Yesu ulivyowekwa
56 Halafu, walirudi nyumbani, wakatayarisha manukato na
marashi kuyapaka mwili wa Yesu. Siku ya Sabato walipumzika kama ilivyoamriwa na
sheria.
|