Chapter 24
1 Jumapili, alfajiri na mapema, wale wanawake walikwenda
kaburini wakichukua yale manukato waliyotayarisha.
2 Walikuta lile jiwe limeviringishwa mbali na kaburi.
3 Walipoingia ndani, hawakuona mwili wa Bwana Yesu.
4 Walipokuwa bado wanashangaa juu ya jambo hilo, mara watu
wawili waliovaa mavazi yenye kung`aa sana, wakasimama karibu nao.
5 Hao wanawake wakaingiwa na hofu, wakainama chini. Ndipo
wale watu wakawaambia, "Kwa nini mnamtafuta aliye hai kati ya wafu?
6 Hayuko hapa; amefufuka. Kumbukeni aliyowaambieni
alipokuwa kule Galilaya:
7 `Ni lazima Mwana wa Mtu atolewe kwa watu waovu, nao
watamsulubisha, na siku ya tatu atafufuka."`
8 Hapo wanawake wakayakumbuka maneno yake,
9 wakarudi kutoka kaburini, wakawapa mitume wale kumi na mmoja
na wengine habari za mambo hayo yote.
10 Hao waliotoa habari hizo kwa mitume ni: Maria Magdalene,
Yoana na Maria mama wa Yakobo, pamoja na wanawake wengine walioandamana nao.
11 Mitume waliyachukua maneno hayo kama yasiyo na msingi,
hivyo hawakuamini.
12 Lakini Petro alitoka, akaenda mbio hadi kaburini.
Alipoinama kuchungulia ndani, akaiona tu ile sanda. Akarudi nyumbani huku akiwa
anashangaa juu ya hayo yaliyotokea.
13 Siku hiyohiyo, wawili kati ya wafuasi wake Yesu wakawa
wanakwenda katika kijiji kimoja kiitwacho Emau, umbali wa kilomita kumi na moja
kutoka Yerusalemu.
14 Wakawa wanazungumza juu ya hayo yote yaliyotukia.
15 Walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Yesu mwenyewe
akatokea, akatembea pamoja nao.
16 Walimwona kwa macho, lakini hawakumtambua.
17 Akawauliza, "Mnazungumza nini huku mnatembea?"
Nao wakasimama kimya, nyuso zao wamezikunja kwa huzuni.
18 Mmoja, aitwaye Kleopa, akamjibu, "Je, wewe ni mgeni
peke yako Yerusalemu ambaye hujui yaliyotukia huko siku hizi?"
19 Naye akawajibu, "Mambo gani?" Wao wakamjibu,
"Mambo yaliyompata Yesu wa Nazareti. Yeye alikuwa nabii mwenye uwezo wa
kutenda na kufundisha mbele ya Mungu na mbele ya watu wote.
20 Makuhani na watawala wetu walimtoa ahukumiwe kufa,
wakamsulubisha.
21 Lakini sisi tulitumaini kwamba yeye ndiye angeikomboa
Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu mambo hayo
yalipotendeka.
22 Tena,
wanawake wengine wa kwetu wametushtua. Walikwenda kaburini mapema asubuhi,
23
wasiukute mwili wake. Wakarudi wakasema kwamba walitokewa na malaika
waliowaambia kwamba alikuwa hai.
24 Wengine
wetu walikwenda kaburini wakashuhudia yale waliyosema hao wanawake; ila yeye
hawakumwona."
25 Kisha
Yesu akawaambia, "Mbona mu wapumbavu kiasi hicho na mioyo yenu ni mizito
hivyo kusadiki yote yaliyonenwa na manabii?
26 Je,
haikumpasa Kristo kuteswa, na hivyo aingie katika utukufu wake?"
27
Akawafafanulia mambo yote yaliyomhusu yeye katika Maandiko Matakatifu kuanzia
Mose hadi manabii wote.
28
Walipokikaribia kile kijiji walikokuwa wanakwenda, Yesu akafanya kana kwamba
anaendelea na safari;
29 lakini
wao wakamsihi wakisema, "Kaa pamoja nasi, maana kunakuchwa, na usiku
unakaribia." Basi, akaingia kijijini, akakaa pamoja nao.
30
Alipoketi kula chakula pamoja nao, akachukua mkate, akaubariki, akaumega,
akawapa.
31 Mara
macho yao yakafumbuliwa, wakamtambua; lakini yeye akatoweka kati yao.
32 Basi,
wakaambiana, "Je, mioyo yetu haikuwa inawaka ndani yetu wakati alipokuwa
anatufafanulia Maandiko Matakatifu kule njiani?"
33
Wakaondoka saa ileile, wakarudi Yerusalemu: wakawakuta wale mitume kumi na
mmoja na wale wengine waliokuwa pamoja nao, wamekusanyika
34
wakisema, "Hakika Bwana amefufuka, amemtokea Simoni."
35 Basi,
hao wafuasi wawili wakawajulisha yale yaliyowapata njiani, na jinsi
walivyomtambua katika kumega mkate.
36
Wanafunzi wote wawili walipokuwa wakiwaambia hayo, Yesu mwenyewe akasimama kati
yao, akawaambia "Amani kwenu."
37
Wakashtuka na kushikwa na hofu wakidhani wameona mzimu.
38 Lakini
yeye akawaambia, "Kwa nini mnafadhaika? Mbona mnakuwa na mashaka mioyoni
mwenu?
39
Angalieni mikono na miguu yangu, ya kwamba ni mimi mwenyewe. Nipapaseni
mkanione, maana mzimu hauna mwili na mifupa kama mnionavyo."
40 Baada
ya kusema hayo, akawaonyesha mikono na miguu.
41 Wakiwa
bado katika hali ya kutosadiki kwa sababu ya furaha yao, na wakiwa
wanastaajabu, akawauliza, "Mnacho chakula chochote hapa?"
42 Wakampa
kipande cha samaki wa kuokwa.
43
Akakichukua, akala, wote wakimwona.
44 Halafu
akawaambia, "Hii ndiyo maana ya maneno niliyowaambia nilipokuwa pamoja
nanyi: kwamba ilikuwa lazima kukamilisha yote yaliyoandikwa juu yangu katika
Sheria ya Mose na katika vitabu vya manabii na katika kitabu cha Zaburi."
45 Kisha,
akaziangazia akili zao ili wapate kuelewa Maandiko Matakatifu.
46
Akawaambia, "Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na siku ya tatu
atafufuka kutoka wafu,
47 na
kwamba ni lazima, kwa jina lake, mataifa yote kuanzia na Yerusalemu yahubiriwe
juu ya kutubu na kusamehewa dhambi.
48 Ninyi
ni mashahidi wa mambo hayo.
49 Nami
mwenyewe nitawapelekeeni yule ambaye Baba aliahidi kumtuma, lakini ngojeni huku
mjini mpaka mtakapopewa ile nguvu itokayo juu."
50 Kisha
akawaongoza nje ya mji hadi Bethania, akainua mikono yake juu, akawabariki.
51
Alipokuwa anawabariki, akawaacha; akachukuliwa mbinguni.
52 Wao
wakamwabudu, wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha kubwa:
53 wakakaa
muda wote Hekaluni wakimsifu Mungu.
|