John
Chapter 1
1 Hapo
Mwanzo, Neno alikuwako; naye alikuwa na Mungu, naye alikuwa Mungu.
2 Tangu
mwanzo Neno alikuwa na Mungu.
3 Kwa njia
yake vitu vyote viliumbwa; hakuna hata kiumbe kimoja kilichoumbwa pasipo yeye.
4 Yeye
alikuwa chanzo cha uhai na uhai huo ulikuwa mwanga wa watu.
5 Na
mwanga huo huangaza gizani, nalo giza halikuweza kuushinda.
6 Mungu
alimtuma mtu mmoja jina lake Yohane,
7 ambaye
alikuja kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Alikuja ili kwa ujumbe wake watu wote
wapate kuamini.
8 Yeye
hakuwa huo mwanga, ila alikuja tu kuwaambia watu juu ya huo mwanga.
9 Huu ndio
mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu wote.
10 Basi,
Neno alikuwako ulimwenguni; na kwa njia yake ulimwengu uliumbwa, lakini
ulimwengu haukumtambua.
11 Alikuja
katika nchi yake mwenyewe, nao walio wake hawakumpokea.
12 Lakini
wale wote waliompokea na kumwamini, hao aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu.
13 Hawa
wamekuwa watoto wa Mungu si kwa uwezo wa kibinadamu, wala kwa nguvu za kimwili,
wala kwa mapenzi ya mtu, bali Mungu mwenyewe ndiye baba yao.
14 Naye
Neno akawa mwanadamu, akakaa kwetu. Nasi tumeuona utukufu wake, utukufu wake
yeye aliye Mwana wa pekee wa Baba; amejaa neema na ukweli.
15 Yohane
aliwaambia watu habari zake, akasema kwa sauti, "Huyu ndiye niliyemtaja
wakati niliposema: `Anakuja mtu mmoja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi,
maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa."`
16
Kutokana na ukamilifu wake sisi tumepokea neema mfululizo.
17 Maana
Mungu alitoa Sheria kwa njia ya Mose, lakini neema na kweli vimekuja kwa njia
ya Kristo.
18 Hakuna
mtu aliyemwona Mungu wakati wowote ule. Mwana wa pekee aliye sawa na Mungu
ambaye ameungana na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za Mungu.
19 Huu
ndio ushahidi Yohane alioutoa wakati viongozi wa Wayahudi kule Yerusalemu
walipowatuma makuhani wa Walawi kwake wamwulize: "Wewe u nani?"
20 Yohane
hakukataa kujibu swali hilo, bali alisema waziwazi, "Mimi siye
Kristo."
21 Hapo
wakamwuliza, "Basi, wewe ni nani? Je, wewe ni Eliya?" Yohane akajibu, "La, mimi siye."
Wakamwuliza, "Je, wewe ni yule nabii?" Yohane akawajibu,
"La!"
22 Nao
wakamwuliza, "Basi, wewe ni nani? Wasema nini juu yako mwenyewe? Tuambie,
ili tuwapelekee jibu wale waliotutuma."
23 Yohane
akawajibu, "Mimi ndiye yule ambaye nabii Isaya alisema habari zake: `Sauti
ya mtu imesikika jangwani: Nyoosheni njia ya Bwana."`
24 Hao watu
walikuwa wametumwa na Mafarisayo.
25 Basi,
wakamwuliza Yohane, "Kama wewe si Kristo, wala Eliya, wala yule nabii,
mbona wabatiza?"
26 Yohane
akawajibu, "Mimi nabatiza kwa maji, lakini yuko mmoja kati yenu, msiyemjua
bado.
27 Huyo anakuja
baada yangu, lakini mimi sistahili hata kumfungua kamba za viatu vyake."
28 Mambo haya
yalifanyika huko Bethania, ng`ambo ya mto Yordani ambako Yohane alikuwa
anabatiza.
29 Kesho yake,
Yohane alimwona Yesu akimjia, akasema, "Huyu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu
aondoaye dhambi ya ulimwengu!
30 Huyu ndiye
niliyesema juu yake: `Baada yangu anakuja mtu mmoja aliye mkuu zaidi kuliko
mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa!`
31 Mimi mwenyewe
sikumfahamu, lakini nimekuja kubatiza kwa maji ili watu wa Israeli wapate
kumjua."
32 Huu ndio
ushahidi Yohane alioutoa: "Nilimwona Roho akishuka kama njiwa kutoka
mbinguni na kutua juu yake.
33 Mimi
sikumjua, lakini yule aliyenituma nikabatize watu kwa maji alikuwa ameniambia:
`Mtu yule utakayemwona Roho akimshukia kutoka mbinguni na kukaa juu yake, huyo
ndiye anayebatiza kwa Roho Mtakatifu.`
34 Mimi nimeona
na ninawaambieni kwamba huyu ndiye Mwana wa Mungu."
35 Kesho yake,
Yohane alikuwa tena mahali hapo pamoja na wanafunzi wake wawili.
36 Alipomwona
Yesu akipita akasema, "Tazameni! Huyu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu."
37 Hao wanafunzi
walimsikia Yohane akisema maneno hayo, wakamfuata Yesu.
38 Basi, Yesu
aligeuka, na alipowaona hao wanafunzi wanamfuata, akawauliza, "Mnatafuta
nini?" Nao wakamjibu, "Rabi (yaani Mwalimu), unakaa wapi?"
39 Yesu
akawaambia, "Njoni, nanyi mtaona." Hao wanafunzi wakamfuata, wakaona
mahali alipokuwa anakaa, wakashinda naye siku hiyo. Ilikuwa yapata saa kumi
jioni.
40 Andrea,
nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa hao wawili waliokuwa wamemsikia Yohane
akisema hivyo, wakamfuata Yesu.
41 Andrea
alimkuta kwanza Simoni, ndugu yake, akamwambia, "Tumemwona Masiha"
(maana yake Kristo).
42 Kisha
akampeleka Simoni kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama Simoni akasema, "Wewe ni
Simoni mwana wa Yohane. Sasa utaitwa Kefa." (maana yake ni Petro, yaani,
"Mwamba.")
43 Kesho yake
Yesu aliamua kwenda Galilaya. Basi, akamkuta Filipo, akamwambia,
"Nifuate."
44 Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji wa akina
Andrea na Petro.
45 Naye Filipo akamkuta Nathanieli, akamwambia,
"Tumemwona yule ambaye Mose aliandika juu yake katika kitabu cha Sheria,
na ambaye manabii waliandika habari zake, yaani Yesu Mwana wa Yosefu, kutoka
Nazareti."
46 Naye Nathanieli akamwuliza Filipo, "Je, kitu chema
chaweza kutoka Nazareti?" Filipo akamwambia, "Njoo uone."
47 Yesu alipomwona Nathanieli akimjia alisema juu yake,
"Tazameni! Huyo ni Mwisraeli halisi: hamna hila ndani yake."
48 Naye Nathanieli akamwuliza, "Umepataje
kunijua?" Yesu akamwambia, "Ulipokuwa chini ya mtini hata kabla
Filipo hajakuita, nilikuona."
49 Hapo Nathanieli akamwambia, "Mwalimu, wewe ni Mwana
wa Mungu. Wewe ni Mfalme wa Israeli!"
50 Yesu akamwambia, "Je, umeamini kwa kuwa nimekwambia
kwamba nilikuona chini ya mtini? Utaona makubwa zaidi kuliko haya."
51 Yesu akaendelea kusema, "Nawaambieni kweli, mtaona
mbingu zinafunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa
Mtu."
|