Chapter 2
1 Siku ya tatu kulikuwa na arusi mjini Kana, mkoani
Galilaya. Mama yake Yesu alikuwapo,
2 naye Yesu alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi
wake.
3 Divai ilipokwisha, mama yake akamwambia, "Hawana divai!"
4 Yesu akamjibu, "Mama, usiniambie la kufanya. Saa
yangu bado."
5 Hapo mama yake akawaambia watumishi, "Lolote
atakalowaambieni, fanyeni."
6 Hapo palikuwa na mitungi sita ya mawe, ambayo kila mmoja
uliweza kuchukua kiasi cha madebe mawili au matatu. Ilikuwa imewekwa hapo
kufuatana na desturi ya Kiyahudi ya kutawadha.
7 Yesu akawaambia, "Ijazeni mitungi hiyo maji."
Nao wakaijaza mpaka juu.
8 Kisha akawaambia, "Sasa choteni mkampelekee mkuu wa
karamu."
9 Mkuu wa karamu alipoonja hayo maji, kumbe yalikuwa
yamegeuka kuwa divai. Yeye hakujua ilikotoka, (lakini wale watumishi waliochota
maji walijua). Mkuu wa karamu akamwita bwana arusi,
10 akamwambia, "Kila mtu huandaa divai nzuri kwanza
hata wakisha tosheka huandaa ile hafifu. Lakini wewe umeiweka divai nzuri mpaka
sasa!"
11 Yesu alifanya ishara hii ya kwanza huko Kana, Galilaya,
akaonyesha utukufu wake; nao wanafunzi wake wakamwamini.
12 Baada ya hayo, Yesu alishuka pamoja na mama yake, ndugu
zake na wanafunzi wake, wakaenda Kafarnaumu ambako walikaa kwa siku chache.
13 Sikukuu ya Wayahudi ya Pasaka ilikuwa imekaribia; hivyo
Yesu akaenda Yerusalemu.
14 Hekaluni aliwakuta watu wakiuza ng`ombe, kondoo na
njiwa, na wavunja fedha walikuwa wamekaa kwenye meza zao.
15 Akatengeneza mjeledi wa kamba, akawafukuza wote nje ya
Hekalu pamoja na kondoo na ng`ombe wao, akazimwaga sarafu za wenye kuvunja
fedha na kupindua meza zao.
16 Akawaambia wale waliokuwa wanauza njiwa, "Ondoeni
vitu hivi hapa. Msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa soko!"
17 Wanafunzi wake wakakumbuka kwamba Maandiko yasema:
"Upendo wangu kwa nyumba yako waniua."
18 Baadhi ya Wayahudi wakamwuliza Yesu, "Utafanya
muujiza gani kuonyesha kwamba unayo haki kufanya mambo haya?"
19 Yesu akawaambia, "Vunjeni Hekalu hili, nami
nitalijenga kwa siku tatu."
20 Hapo Wayahudi wakasema, "Hekalu hili lilijengwa kwa
muda wa miaka arobaini na sita. Je, wewe utalijenga kwa siku tatu?"
21 Lakini Yesu alikuwa anaongea juu ya Hekalu ambalo ni
mwili wake.
22 Basi, alipofufuliwa kutoka wafu, wanafunzi wake
walikumbuka kwamba alikuwa amesema hayo, wakaamini Maandiko Matakatifu na yale
maneno aliyokuwa akisema Yesu.
23 Yesu alipokuwa Yerusalemu kwa sikukuu ya Pasaka, watu
wengi walimwamini walipoona ishara alizozifanya.
24 Lakini Yesu hakuwa na imani nao kwa sababu aliwajua
wote.
25 Hakuhitaji kuambiwa chochote juu ya watu, maana aliyajua
barabara mambo yote yaliyomo mioyoni mwao.
|