Chapter 3
1 Kulikuwa na kiongozi mmoja Myahudi, wa kikundi cha
Mafarisayo, jina lake Nikodemo.
2 Siku moja alimwendea Yesu usiku, akamwambia, "Rabi,
tunajua kwamba wewe ni mwalimu uliyetumwa na Mungu, maana hakuna mtu awezaye
kufanya ishara unazozifanya Mungu asipokuwa pamoja naye."
3 Yesu akamwambia, "Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa
upya hataweza kuuona ufalme wa Mungu."
4 Nikodemo akamwuliza, "Mtu mzima awezaje kuzaliwa
tena? Hawezi kuingia tumboni mwa mama yake na kuzaliwa mara ya pili!"
5 Yesu akamjibu, "Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa kwa
maji na Roho, hawezi kamwe kuingia katika ufalme wa Mungu.
6 Mtu huzaliwa kimwili kwa baba na mama, lakini huzaliwa
kiroho kwa Roho.
7 Usistaajabu kwamba nimekwambia kuwa ni lazima kuzaliwa
upya.
8 Upepo huvuma kuelekea upendako; waisikia sauti yake,
lakini hujui unakotoka wala unakokwenda. Ndivyo ilivyo kwa mtu aliyezaliwa kwa
Roho."
9 Nikodemo akamwuliza, "Mambo haya
yanawezekanaje?"
10 Yesu akamjibu, "Je, wewe ni mwalimu katika Israel
na huyajui mambo haya?
11 Kweli nakwambia, sisi twasema tunayoyajua na kushuhudia
tuliyoyaona, lakini ninyi hamkubali ujumbe wetu.
12 Ikiwa nimewaambieni mambo ya kidunia nanyi hamniamini,
mtawezaje kuamini nikiwaambieni mambo ya mbinguni?
13 Hakuna mtu aliyepata kwenda juu mbinguni isipokuwa Mwana
wa Mtu ambaye ameshuka kutoka mbinguni.
14 "Kama vile Mose alivyomwinua juu nyoka wa shaba
kule jangwani, naye Mwana wa Mtu atainuliwa juu vivyo hivyo,
15 ili kila anayemwamini awe na uzima wa milele.
16 Maana Mungu aliupenda ulimwengu hivi hata akamtoa Mwana
wake wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.
17 Maana Mungu hakumtuma Mwanae ulimwenguni ili auhukumu
ulimwengu, bali aukomboe ulimwengu.
18 "Anayemwamini Mwana hahukumiwi; asiyemwamini
amekwisha hukumiwa kwa sababu hakumwamini Mwana wa pekee wa Mungu.
19 Na hukumu yenyewe ndiyo hii: Mwanga umekuja ulimwenguni
lakini watu wakapenda giza kuliko mwanga, kwani matendo yao ni maovu.
20 Kila mtu atendaye maovu anauchukia mwanga, wala haji
kwenye mwanga, maana hapendi matendo yake maovu yamulikwe.
21 Lakini mwenye kuuzingatia ukweli huja kwenye mwanga, ili
matendo yake yaonekane yametendwa kwa kumtii Mungu."
22 Baada ya hayo, Yesu alifika mkoani Yudea pamoja na
wanafunzi wake. Alikaa huko pamoja nao kwa muda, akibatiza watu.
23 Yohane pia alikuwa akibatiza watu huko Ainoni, karibu na
Salemu, maana huko kulikuwa na maji mengi. Watu walimwendea, naye akawabatiza.
24 Wakati huo Yohane alikuwa bado hajafungwa gerezani.)
25 Ubishi ulitokea kati ya baadhi ya wanafunzi wa Yohane na
Myahudi mmoja kuhusu desturi za kutawadha.
26 Basi, wanafunzi hao wakamwendea Yohane na kumwambia,
"Mwalimu, yule mtu aliyekuwa pamoja nawe ng`ambo ya Yordani na ambaye wewe
ulimshuhudia, sasa naye anabatiza, na watu wote wanamwendea."
27 Yohane akawaambia, "Mtu hawezi kuwa na kitu
asipopewa na Mungu.
28 Nanyi wenyewe mwaweza kushuhudia kuwa nilisema: `Mimi
siye Kristo, lakini nimetumwa ili nimtangulie!`
29 Bibiarusi ni wake bwanaarusi, lakini rafiki yake bwana
arusi, anayesimama na kusikiliza, hufurahi sana anapomsikia bwana arusi
akisema. Ndivyo furaha yangu ilivyokamilishwa.
30 Ni lazima yeye azidi kuwa maarufu, na mimi nipungue.
31 "Anayekuja kutoka juu ni mkuu kuliko wote; atokaye
duniani ni wa dunia, na huongea mambo ya kidunia. Lakini anayekuja kutoka
mbinguni ni mkuu kuliko wote.
32 Yeye husema yale aliyoyaona na kuyasikia, lakini hakuna
mtu anayekubali ujumbe wake.
33 Lakini mtu yeyote anayekubali ujumbe wake anathibitisha
kwamba Mungu ni kweli.
34 Yule aliyetumwa na Mungu husema maneno ya Mungu, maana
Mungu humjalia mtu huyo Roho wake bila kipimo.
35 Baba anampenda Mwana na amemkabidhi vitu vyote.
36 Anayemwamini Mwana anao uzima wa milele; asiyemtii Mwana
hatakuwa na uzima wa milele, bali ghadhabu ya Mungu hubaki juu yake."
|