Chapter 2
1 Yesu
alizaliwa mjini Bethlehemu, mkoani Yudea, wakati Herode alipokuwa mfalme. Punde
tu baada ya kuzaliwa kwake, wataalamu wa nyota kutoka mashariki walifika
Yerusalemu,
2
wakauliza, "Yuko wapi mtoto, Mfalme wa Wayahudi, aliyezaliwa? Tumeiona
nyota yake ilipotokea mashariki, tukaja kumwabudu."
3 Mfalme
Herode aliposikia hayo, alifadhaika, yeye pamoja na wakazi wote wa Yerusalemu.
4 Basi
akawaita pamoja makuhani wakuu wote na walimu wa Sheria, akawauliza,
"Kristo atazaliwa wapi?"
5 Nao
wakamjibu, "Mjini Bethlehemu, mkoani Yudea. Ndivyo nabii alivyoandika:
6 `Ewe
Bethlehemu katika nchi ya Yuda, kwa vyovyote wewe si mdogo kabisa kati ya
viongozi wa Yuda; maana kwako atatokea kiongozi atakayewaongoza watu wangu,
Israeli."`
7 Hapo,
Herode aliwaita faraghani hao wataalamu wa nyota, akawauliza wakati hasa ile
nyota ilipowatokea.
8 Kisha
akawatuma Bethlehemu akisema, "Nendeni mkachunguze kwa makini habari za
mtoto huyo. Mkisha mpata nileteeni habari ili nami niende nikamwabudu."
9 Baada ya
kumsikiliza mfalme, hao wataalamu wa nyota wakaenda. Kumbe ile nyota waliyokuwa
wameiona upande wa mashariki iliwatangulia hata ikaenda kusimama juu ya mahali
pale alipokuwa mtoto.
10
Walipoiona hiyo nyota, walifurahi mno.
11 Basi,
wakaingia nyumbani, wakamwona yule mtoto pamoja na Maria mama yake; wakapiga
magoti, wakamsujudia. Kisha wakafungua hazina zao, wakampa zawadi: dhahabu,
ubani na manemane. ic
12 Mungu
aliwaonya katika ndoto wasimrudie Herode; hivyo wakarudi makwao kwa njia
nyingine.
13 Baada
ya wale wageni kuondoka, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto,
akamwambia, "Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, mkimbilie Misri.
Kaeni huko mpaka nitakapokwambia, maana Herode anakusudia kumwua huyu
mtoto."
14 Hivyo,
Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akaondoka usiku, akaenda
Misri.
15 Akakaa
huko mpaka Herode alipokufa. Jambo hilo lilifanyika ili neno alilosema Bwana
kwa njia ya nabii litimie: "Nilimwita Mwanangu kutoka Misri."
16 Herode
alipogundua kwamba wale wataalamu wa nyota walikuwa wamemhadaa, alikasirika
sana. Akaamuru watoto wote wa kiume mjini Bethlehemu na kandokando yake wenye
umri wa miaka miwili na chini yake wauawe. Alifanya hivyo kufuatana na muda
aliopata kujua kutoka kwa wale wataalamu wa nyota.
17 Ndivyo
yalivyotimia maneno yaliyosemwa kwa njia ya nabii Yeremia:
18 "Sauti imesikika mjini Rama, kilio na maombolezo
mengi. Raheli anawalilia watoto wake, wala hataki kutulizwa, maana wote
wamefariki."
19 Baada ya kifo cha Herode, malaika wa Bwana alimtokea
Yosefu katika ndoto kule Misri,
20 akamwambia, "Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama
yake, urudi tena katika nchi ya Israeli, maana wale waliotaka kumwua mtoto huyo
wamekwisha kufa."
21 Basi, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama
yake, akarejea katika nchi ya Israeli.
22 Lakini Yosefu aliposikia kwamba Arkelao mwanawe Herode
alikuwa mfalme wa Yudea mahali pa baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye baada
ya kuonywa katika ndoto, alikwenda katika mkoa wa Galilaya,
23 akahamia katika mji uitwao Nazareti. Ndivyo yalivyotimia
maneno yaliyonenwa kwa njia ya manabii: "Ataitwa Mnazare."
|