Chapter 4
1 Mafarisayo walisikia kwamba Yesu alikuwa anabatiza na
kuwapata wanafunzi wengi kuliko Yohane.
2 Lakini ukweli ni kwamba Yesu hakuwa anabatiza ila
wanafunzi wake.)
3 Basi, Yesu aliposikia hayo, alitoka Yudea akarudi
Galilaya;
4 na katika safari hiyo ilimbidi apitie Samaria.
5 Basi, akafika Sukari, mji mmoja wa Samaria, karibu na
shamba ambalo Yakobo alikuwa amempa mwanawe, Yosefu.
6 Mahali hapo palikuwa na kisima cha Yakobo, naye Yesu,
kutokana na uchovu wa safari, akaketi kando ya kisima. Ilikuwa yapata saa sita
mchana.
7 Basi, mwanamke mmoja Msamaria akafika kuteka maji. Yesu
akamwambia, "Nipatie maji ninywe."
8 (Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini
kununua chakula.)
9 Lakini huyo mwanamke akamwambia, "Wewe ni Myahudi;
mimi ni mwanamke Msamaria! Unawezaje kuniomba maji?" (Wayahudi hawakuwa na
ushirikiano na Wasamaria katika matumizi ya vitu.)
10 Yesu akamjibu, "Kama tu ungalijua zawadi ya Mungu
na ni nani anayekwambia: `Nipatie maji ninywe,` ungalikwisha mwomba, naye
angekupa maji yaliyo hai."
11 Huyo mama akasema, "Mheshimiwa, wewe huna chombo
cha kutekea maji, nacho kisima ni kirefu; utapata wapi maji yaliyo hai?
12 Au, labda wewe wajifanya mkuu kuliko babu yetu Yakobo?
Yeye alitupa sisi kisima hiki; na yeye mwenyewe, watoto wake na mifugo yake
walikunywa maji ya kisima hiki."
13 Yesu akamjibu, "Kila anayekunywa maji haya ataona
kiu tena.
14 Lakini atakayekunywa maji nitakayompa mimi, hataona kiu
milele. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji ya uzima na
kumpatia uzima wa milele."
15 Huyo mwanamke akamwambia, "Mheshimiwa, nipe maji
hayo ili nisione kiu tena; nisije tena mpaka hapa kuteka maji."
16 Yesu akamwambia, "Nenda ukamwite mumeo uje naye
hapa."
17 Huyo mwanamke akamwambia, "Mimi sina mume."
Yesu akamwambia, "Umesema kweli, kwamba huna mume.
18 Maana umekuwa na waume watano, na huyo unayeishi naye
sasa si mume wako. Hapo umesema kweli."
19 Huyo Mwanamke akamwambia, "Mheshimiwa, naona ya
kuwa wewe u nabii.
20 Babu zetu waliabudu juu ya mlima huu, lakini ninyi
mwasema kwamba mahali pa kumwabudu Mungu ni kule Yerusalemu."
21 Yesu akamwambia, "Niamini; wakati unakuja ambapo
hamtamwabudu Baba juu ya mlima huu, wala kule Yerusalemu.
22 Ninyi Wasamaria mnamwabudu yule msiyemjua, lakini sisi
tunamjua huyo tunayemwabudu, kwa maana wokovu unatoka kwa Wayahudi.
23 Lakini wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo
wanaoabudu kweli, watamwabudu Baba kwa nguvu ya Roho; watu wanaomwabudu hivyo ndio
Baba anaotaka.
24 Mungu ni Roho, na watu wataweza tu kumwabudu kweli kwa
nguvu ya Roho wake."
25 Huyo mama akamwambia, "Najua kwamba Masiha, aitwaye
Kristo, anakuja. Atakapokuja atatujulisha kila kitu."
26 Yesu akamwambia, "Mimi ninayesema nawe,
ndiye."
27 Hapo wanafunzi wake wakarudi, wakastaajabu sana kuona
anaongea na mwanamke. Lakini hakuna mtu aliyesema: "Unataka nini?"
au, "Kwa nini unaongea na mwanamke?"
28 Huyo mama akauacha mtungi wake pale, akaenda mjini na
kuwaambia watu,
29 "Njoni mkamwone mtu aliyeniambia mambo yote
niliyotenda! Je, yawezekana kuwa yeye ndiye Kristo?"
30 Watu wakatoka mjini, wakamwendea Yesu.
31 Wakati huohuo wanafunzi wake walikuwa wanamsihi Yesu:
"Mwalimu, ule chakula."
32 Lakini Yesu akawaambia, "Mimi ninacho chakula
msichokijua ninyi."
33 Wanafunzi wake wakaulizana, "Je, kuna mtu
aliyemletea chakula?"
34 Yesu akawaambia, "Chakula changu ni kufanya
anachotaka yule aliyenituma na kuitimiza kazi yake.
35 Ninyi mwasema: `Bado miezi minne tu, na wakati wa mavuno
utafika!` Lakini mimi nawaambieni, yatazameni mashamba; mazao yako tayari
kuvunwa.
36 Mvunaji anapata mshahara wake, na anakusanya mavuno kwa
ajili ya uzima wa milele; hivyo mpandaji na mvunaji watafurahi pamoja.
37 Kwa sababu hiyo msemo huu ni kweli: `Mmoja hupanda na
mwingine huvuna.`
38 Mimi nimewatuma mkavune mavuno ambayo hamkuyatolea
jasho, wengine walifanya kazi, lakini ninyi mnafaidika kutokana na jasho
lao."
39 Wasamaria wengi wa kijiji kile waliamini kwa sababu ya
maneno aliyosema huyo mama: "Ameniambia mambo yote niliyofanya."
40 Wasamaria walimwendea Yesu wakamwomba akae nao; naye
akakaa hapo siku mbili.
41 Watu wengi zaidi walimwamini kwa sababu ya ujumbe wake.
42 Wakamwambia yule mama, "Sisi hatuamini tu kwa
sababu ya maneno yako; sisi wenyewe tumesikia, na tunajua kwamba huyu ndiye
kweli Mwokozi wa ulimwengu."
43 Baada ya siku mbili Yesu aliondoka hapo, akaenda
Galilaya.
44 Maana Yesu mwenyewe alisema waziwazi kwamba, "Nabii
hapati heshima katika nchi yake."
45 Basi, alipofika Galilaya, Wagalilaya wengi
walimkaribisha. Maana nao pia walikuwa kwenye sikukuu ya Pasaka, wakayaona mambo
yote Yesu aliyotenda huko Yerusalemu wakati wa sikukuu hiyo.
46 Yesu alifika tena huko mjini Kana, mkoani Galilaya,
mahali alipogeuza maji kuwa divai. Kulikuwa na ofisa mmoja aliyekuwa na mtoto
mgonjwa huko Kafarnaumu.
47 Basi, huyo ofisa aliposikia kuwa Yesu alikuwa ametoka
Yudea na kufika Galilaya, alimwendea akamwomba aende kumponya mtoto wake
aliyekuwa mgonjwa mahututi.
48 Yesu akamwambia, "Msipoona ishara na maajabu
hamtaamini!"
49 Huyo ofisa akamwambia, "Mheshimiwa, tafadhali
twende kabla mwanangu hajafa."
50 Yesu akamwambia, "Nenda tu, mwanao yu mzima."
Huyo mtu akaamini maneno ya Yesu, akaenda zake.
51 Alipokuwa bado njiani, watumishi wake walikutana naye,
wakamwambia kwamba mwanawe alikuwa mzima.
52 Naye akawauliza saa mtoto alipopata nafuu; nao
wakamwambia, "Jana saa saba mchana, homa ilimwacha."
53 Huyo baba akakumbuka kwamba ilikuwa ni saa ileile ambapo
Yesu alimwambia: "Mwanao yu mzima." Basi, yeye akaamini pamoja na
jamaa yake yote.
54 Hii ilikuwa ishara ya pili aliyoifanya Yesu alipokuwa
anatoka Yudea kwenda Galilaya.
|