Chapter 7
1 Baada ya hayo, Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya.
Hakutaka kutembea mkoani Yudea kwa sababu viongozi wa Wayahudi walikuwa
wanataka kumwua.
2 Sikukuu ya Vibanda ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.
3 Basi ndugu zake wakamwambia, "Ondoka hapa uende
Yudea ili wanafunzi wako wazione kazi unazozifanya.
4 Mtu hafanyi mambo kwa siri kama anataka kujulikana kwa
watu. Maadam unafanya mambo haya, basi, jidhihirishe kwa ulimwengu."
5 Hata ndugu zake hawakumwamini!)
6 Basi, Yesu akawaambia, "Wakati wangu ufaao haujafika
bado. Lakini kwenu ninyi kila wakati unafaa.
7 Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi, lakini mimi
wanichukia kwa sababu mimi nauambia wazi kwamba matendo yake ni maovu.
8 Ninyi nendeni kwenye sikukuu hiyo. Mimi siendi kwenye
sikukuu hiyo, maana saa yangu ifaayo haijafika."
9 Alisema hayo kisha akabaki huko Galilaya.
10 Baada ya ndugu zake kwenda kwenye sikukuu, Yesu naye
alikwenda, lakini hakuenda kwa hadhara bali kwa siri.
11 Viongozi wa Wayahudi walikuwa wanamtafuta kwenye sikukuu
hiyo; Wakauliza: "Yuko wapi?"
12 Kulikuwa na minong`ono mingi katika umati wa watu.
Baadhi yao walisema, "Ni mtu mwema." Wengine walisema, "La!
Anawapotosha watu."
13 Hata hivyo hakuna mtu aliyethubutu kusema, habari zake
hadharani kwa kuwaogopa viongozi wa Wayahudi.
14 Sikukuu hiyo ilipofikia katikati, Yesu naye alikwenda
Hekaluni, akaanza kufundisha.
15 Basi, Wayahudi wakashangaa na kusema "Mtu huyu
amepataje elimu naye hakusoma shuleni?"
16 Hapo Yesu akawajibu, "Mafundisho ninayofundisha si
yangu, bali ni yake yeye aliyenituma.
17 Mtu anayependa kufanya yale anayotaka Mungu, atajua kama
mafundisho yangu yametoka kwa Mungu, au mimi najisemea tu mwenyewe.
18 Yeye anayejisemea tu mwenyewe anatafuta sifa yake
mwenyewe; lakini anayetafuta sifa ya yule aliyemtuma, huyo ni mwaminifu, na
ndani yake hamna uovu wowote.
19 Je, Mose hakuwapeni Sheria? Hata hivyo, hakuna hata
mmoja wenu anayeishika Sheria. Kwa nini mnataka kuniua?"
20 Hapo watu wakamjibu, "Una wazimu wewe! Nani anataka
kukuua?"
21 Yesu akawajibu, "Kuna jambo moja nililofanya, nanyi
mnalistaajabia.
22 Mose aliwapeni ile desturi ya kutahiri. (Si kwamba
desturi hiyo ilitoka kwa Mose, bali ilitoka kwa mababu). Sasa ninyi humtahiri
mtu hata siku ya Sabato.
23 Ikiwa basi, mtu hutahiriwa hata siku ya Sabato kusudi
Sheria ya Mose isivunjwe, mbona mnanikasirikia kwa sababu nimemfanya mtu kuwa
mzima kabisa siku ya Sabato?
24 Msihukumu mambo kwa nje tu; toeni hukumu ya haki."
25 Baadhi ya watu wa Yerusalemu walisema, "Je, yule
mtu wanayemtafuta wamuue si huyu?
26 Tazameni sasa! Anawaonya hadharani, wala hakuna mtu
anayemwambia hata neno. Je, yawezekana kuwa viongozi wametambua kweli kwamba
huyu ndiye Kristo?
27 Kristo atakapokuja hakuna mtu atakayejua mahali
alikotoka, lakini sisi tunajua alikotoka mtu huyu!"
28 Basi, Yesu alipokuwa anafundisha Hekaluni alipaaza sauti
na kusema, "Ati mnanijua; hata nilikotoka mnakujua! Hata hivyo, sikuja kwa
mamlaka yangu mwenyewe; ila yeye aliyenituma mimi ni wa kweli, nanyi hamumjui.
29 Lakini mimi namjua kwa sababu nimetoka kwake, naye ndiye
aliyenituma."
30 Basi, watu wakataka kumtia nguvuni, lakini hakuna mtu
aliyethubutu kumkamata kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado.
31 Wengi katika ule umati wa watu walimwamini, wakasema,
"Je, Kristo akija atafanya ishara kubwa zaidi kuliko alizozifanya
huyu?"
32 Mafarisayo waliwasikia watu wakinong`ona maneno hayo juu
ya Yesu. Basi, wao pamoja na makuhani wakuu wakawatuma walinzi wamtie nguvuni.
33 Yesu akasema, "Bado niko nanyi kwa muda mfupi,
kisha nitamwendea yule aliyenituma.
34 Mtanitafuta lakini hamtaniona, maana pale nitakapokuwa
ninyi hamwezi kufika."
35 Viongozi wa Wayahudi wakasema wao kwa wao, "Mtu
huyu atakwenda wapi ambapo hatutaweza kumpata? Atakwenda kwa Wayahudi
waliotawanyika kati ya Wagiriki, na kuwafundisha Wagiriki?
36 Ana maana gani anaposema: `Mtanitafuta lakini
hamtanipata, na mahali nitakapokuwa ninyi hamwezi kufika?"`
37 Siku ya mwisho ya sikukuu hiyo ilikuwa siku maalum. Yesu
alisimama, akasema kwa sauti kubwa, "Aliye na kiu na aje kwangu anywe.
38 Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: `Anayeniamini mimi,
mito ya maji yenye uzima itatiririka kutoka moyoni mwake!"`
39 Alisema
hayo kumhusu Roho ambaye wale waliomwamini yeye watampokea. Wakati huo Roho
alikuwa hajafika kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa bado.)
40 Baadhi
ya watu katika ule umati walisikia maneno hayo, wakasema, "Kweli mtu huyu
ndiye yule nabii!"
41 Wengine
wakasema, "Huyu ndiye Kristo!" Lakini wengine walisema, "Je,
yawezekana Kristo akatoka Galilaya?
42
Maandiko Matakatifu yasemaje? Yanasema: `Kristo atatoka katika ukoo wa Daudi, na
atazaliwa Bethlehemu, mji wa Daudi!"`
43 Basi,
kukatokea mafarakano juu yake katika ule umati wa watu.
44 Baadhi
ya watu walitaka kumtia nguvuni lakini hakuna aliyejaribu kumkamata.
45 Kisha
wale walinzi wakarudi kwa makuhani wakuu na Mafarisayo; nao wakawauliza,
"Kwa nini hamkumleta?"
46 Walinzi
wakawajibu, "Hakuna mtu aliyepata kamwe kusema kama asemavyo mtu
huyu!"
47
Mafarisayo wakawauliza, "Je, nanyi pia mmedanganyika?
48 Je,
mmekwisha mwona hata mmoja wa viongozi wa watu, au mmoja wa Mafarisayo
aliyemwamini?
49 Lakini
umati huu haujui Sheria ya Mose; umelaaniwa!"
50 Mmoja
wao alikuwa Nikodemo ambaye hapo awali alikuwa amemwendea Yesu. Basi, yeye
akawaambia,
51
"Je, Sheria yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza na kujua anafanya
nini?"
52 Nao
wakamjibu, "Je, wewe pia umetoka Galilaya? Haya, kayachunguze Maandiko
Matakatifu nawe utaona kwamba Galilaya hakutoki kamwe nabii!" [[[
53 Basi,
wote wakaondoka, kila mtu akaenda zake;
|