Chapter 8
1 lakini
Yesu akaenda kwenye mlima wa Mizeituni.
2 Kesho
yake asubuhi na mapema alikwenda tena Hekaluni. Watu wote wakamwendea, naye
akaketi akawa anawafundisha.
3 Basi,
walimu wa Sheria na Mafarisayo wakamletea mwanamke mmoja aliyefumaniwa katika
uzinzi. Wakamsimamisha katikati yao.
4 Kisha
wakamwuliza Yesu, "Mwalimu! Mwanamke huyu alifumaniwa katika uzinzi.
5 Katika
Sheria yetu Mose alituamuru mwanamke kama huyu apigwe mawe. Basi, wewe
wasemaje?"
6 Walisema
hivyo kumjaribu, wapate kisa cha kumshtaki. Lakini Yesu akainama chini,
akaandika ardhini kwa kidole.
7
Walipozidi kumwuliza, Yesu akainuka, akawaambia, "Mtu asiye na dhambi
miongoni mwenu na awe wa kwanza kumpiga jiwe."
8 Kisha
akainama tena, akawa anaandika ardhini.
9
Waliposikia hivyo, wakaanza kutoweka mmojammoja, wakitanguliwa na wazee. Yesu
akabaki peke yake, na yule mwanamke amesimama palepale.
10 Yesu
alipoinuka akamwuliza huyo mwanamke, "Wako wapi wale watu? Je, hakuna hata
mmoja aliyekuhukumu?"
11 Huyo
mwanamke akamjibu, "Mheshimiwa, hakuna hata mmoja!" Naye Yesu
akamwambia, "Wala mimi sikuhukumu. Nenda zako; na tangu sasa usitende
dhambi tena."]*fb* mahali pengine.
12 Yesu
alipozungumza nao tena, aliwaambia, "Mimi ndimi mwanga wa ulimwengu.
Anayenifuata mimi hatembei kamwe gizani, bali atakuwa na mwanga wa uzima."
13 Basi,
Mafarisayo wakamwambia, "Wewe unajishuhudia mwenyewe; kwa hiyo ushahidi
wako si halali."
14 Yesu
akawajibu, "Hata kama ninajishuhudia mwenyewe, ushahidi wangu ni wa kweli
kwa sababu mimi najua nilikotoka na ninakokwenda. Lakini ninyi hamjui
nilikotoka wala ninakokwenda.
15 Ninyi
mnahukumu kwa fikira za kibinadamu, lakini mimi simhukumu mtu.
16 Hata
nikihukumu, hukumu yangu ni ya haki kwa sababu mimi siko peke yangu; Baba
aliyenituma yuko pamoja nami.
17
Imeandikwa katika Sheria yenu ya kwamba ushahidi wa watu wawili ni halali.
18 Mimi
najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma, ananishuhudia pia."
19 Hapo
wakamwuliza, "Baba yako yuko wapi?" Yesu akawajibu "Ninyi
hamnijui mimi wala hamumjui Baba. Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba yangu
pia."
20 Yesu
alisema maneno hayo kwenye chumba cha hazina alipokuwa anafundisha Hekaluni.
Wala hakuna mtu aliyemtia nguvuni, kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado.
21 Yesu
akawaambia tena, "Naenda zangu nanyi mtanitafuta, lakini mtakufa katika
dhambi zenu. Niendako mimi,ninyi hamwezi kufika."
22 Basi,
viongozi wa Wayahudi wakasema, "Je, atajiua? Mbona anasema: `Niendako
ninyi hamwezi kufika?"`
23 Yesu
akawaambia, "Ninyi mmetoka papa hapa chini, mimi nimetoka juu; ninyi ni wa
ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu.
24 Ndiyo
maana niliwaambieni mtakufa katika dhambi zenu. Kama msipoamini kwamba `Mimi
ndimi`, mtakufa katika dhambi zenu."
25 Nao
wakamwuliza, "Wewe ni nani?" Yesu akawajibu, "Nimewaambieni
tangu mwanzo!
26 Ninayo
mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu. Lakini yule aliyenituma ni kweli; nami
nauambia ulimwengu mambo yale tu niliyoyasikia kutoka kwake."
27
Hawakuelewa kwamba Yesu alikuwa akisema nao juu ya Baba.
28 Basi,
Yesu akawaambia, "Mtakapokwisha mwinua Mwana wa Mtu hapo ndipo mtakapojua
kwamba `Mimi ndimi`, na kwamba sifanyi chochote mimi mwenyewe, ila nasema tu
yale Baba aliyonifundisha.
29 Yule
aliyenituma yuko pamoja nami; yeye hakuniacha peke yangu kwani nafanya daima
yale yanayompendeza."
30 Baada
ya kusema hayo watu wengi walimwamini.
31 Basi,
Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, "Kama mkiyazingatia mafundisho
yangu mtakuwa kweli wanafunzi wangu.
32 Mtaujua
ukweli, nao ukweli utawapeni uhuru."
33 Nao
wakamjibu, "Sisi ni wazawa wa Abrahamu, na hatujapata kamwe kuwa watumwa
wa mtu yeyote yule. Una maana gani unaposema: `mtakuwa huru?"`
34 Yesu
akawajibu, "Kweli nawaambieni, kila mtu anayetenda dhambi ni mtumwa wa
dhambi.
35 Mtumwa
hana makao ya kudumu nyumbani, lakini mwana anayo makao ya kudumu.
36 Kama
mwana akiwapeni uhuru mtakuwa huru kweli.
37 Najua
kwamba ninyi ni wazawa wa Abrahamu. Hata hivyo, mnataka kuniua kwa sababu
hamuyakubali mafundisho yangu.
38 Mimi
nasema yale aliyonionyesha Baba, lakini ninyi mwafanya yale aliyowaambieni baba
yenu."
39 Wao
wakamjibu, "Baba yetu ni Abrahamu!" Yesu akawaambia, "Kama ninyi
mngekuwa watoto wa Abrahamu, mngefanya kama alivyofanya Abrahamu,
40 Mimi
nimewaambieni ukweli niliousikia kwa Mungu; hata hivyo, ninyi mwataka kuniua.
Abrahamu hakufanya hivyo!
41 Ninyi
mnafanya mambo yaleyale aliyofanya babu yenu." Wao wakamwambia, "Sisi
si watoto haramu! Tunaye baba mmoja tu, yaani Mungu."
42 Yesu akawaambia,
"Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda mimi, maana mimi nilitoka kwa
Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila yeye alinituma.
43 Kwa
nini hamwelewi hayo ninayosema? Ni kwa kuwa hamwezi kuusikiliza ujumbe wangu.
44 Ninyi
ni watoto wa baba yenu Ibilisi na mnataka tu kutekeleza tamaa za baba yenu.
Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo; hana msimamo katika ukweli, kwani ukweli
haumo ndani yake. Kila asemapo uongo, husema kutokana na hali yake ya maumbile,
maana yeye ni mwongo na baba wa uongo.
45 Mimi
nasema ukweli, na ndiyo maana ninyi hamniamini.
46 Nani
kati yenu awezaye kuthibitisha kuwa mimi nina dhambi? Ikiwa basi nasema ukweli,
kwa nini hamniamini?
47 Aliye
wa Mungu husikiliza maneno ya Mungu. Lakini ninyi hamsikilizi kwa sababu ninyi
si (watu wa) Mungu."
48
Wayahudi wakamwambia, "Je, hatukusema kweli kwamba wewe ni Msamaria, na
tena una pepo?"
49 Yesu
akajibu, "Mimi sina pepo; mimi namheshimu Baba yangu, lakini ninyi
hamniheshimu.
50 Mimi
sijitafutii utukufu wangu mwenyewe; yuko mmoja mwenye kuutafuta utukufu huo,
naye ni hakimu.
51 Kweli
nawaambieni, anayeuzingatia ujumbe wangu hatakufa milele."
52 Basi,
Wayahudi wakasema, "Sasa tunajua kweli kwamba wewe ni mwendawazimu!
Abrahamu alikufa, na manabii pia walikufa, nawe wasema ati, `Anayeuzingatia
ujumbe wangu hatakufa milele!`
53 Je,
unajifanya mkuu zaidi kuliko baba yetu Abrahamu ambaye alikufa? Hata na manabii
walikufa. Wewe unajifanya kuwa nani?"
54 Yesu
akawajibu, "Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu. Baba yangu
ambaye ninyi mwasema ni Baba yenu, ndiye anayenitukuza.
55 Ninyi
hamjapata kumjua, lakini mimi namjua. Na, nikisema simjui, nitakuwa mwongo kama ninyi. Mimi namjua na
ninashika neno lake.
56
Abrahamu, baba yenu, alishangilia aione siku yangu; naye aliiona,
akafurahi."
57 Basi,
Wayahudi wakamwambia, "Wewe hujatimiza miaka hamsini bado, nawe umemwona
Abrahamu?"
58 Yesu
akawaambia, "Kweli nawaambieni, kabla Abrahamu hajazaliwa, mimi
niko."
59 Hapo
wakaokota mawe ili wamtupie, lakini Yesu akajificha, akatoka Hekaluni.
|