Chapter 9
1 Yesu
alipokuwa akipita alimwona mtu mmoja, kipofu tangu kuzaliwa.
2 Basi,
wanafunzi wakamwuliza, "Mwalimu! Ni nani aliyetenda dhambi: mtu huyu, ama
wazazi wake, hata akazaliwa kipofu?"
3 Yesu
akajibu, "Jambo hili halikutukia kwa sababu ya dhambi zake yeye, wala
dhambi za wazazi wake; ila alizaliwa kipofu ili nguvu ya Mungu ionekane
ikifanya kazi ndani yake.
4 Kukiwa
bado mchana yatupasa kuendelea kufanya kazi za yule aliyenituma; maana usiku
unakuja ambapo mtu hawezi kufanya kazi.
5 Wakati
ningali ulimwenguni, mimi ni mwanga wa ulimwengu."
6 Baada ya
kusema hayo, akatema mate chini, akafanyiza tope, akampaka yule kipofu machoni,
7
akamwambia, "Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu." (maana ya jina
hili ni "aliyetumwa"). Basi, huyo kipofu akaenda, akanawa, kisha
akarudi akiwa anaona.
8 Basi,
jirani zake na wale waliokuwa wanajua kwamba hapo awali alikuwa maskini
mwombaji, wakasema, "Je, huyu siye yule maskini aliyekuwa akiketi na
kuomba?"
9 Baadhi
yao wakasema, "Ndiye." Wengine wakasema, "La! Ila anafanana
naye." Lakini huyo aliyekuwa kipofu akasema, "Ni mimi!"
10 Basi,
wakamwuliza, "Sasa, macho yako yalipataje kufumbuliwa?"
11 Naye
akawajibu, "Yule mtu aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka machoni na
kuniambia: `Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu.` Basi, mimi nikaenda,
nikanawa, nikapata kuona."
12
Wakamwuliza, "Yeye yuko wapi?" Naye akawajibu, "Mimi
sijui!"
13 Kisha wakampeleka
huyo mtu aliyekuwa kipofu kwa Mafarisayo.
14 Siku
hiyo Yesu alipofanya tope na kumfumbua macho mtu huyo, ilikuwa siku ya Sabato.
15 Basi,
Mafarisayo wakamwuliza mtu huyo, "Umepataje kuona?" Naye akawaambia,
"Alinipaka tope machoni, nami nikanawa na sasa naona."
16 Baadhi
ya Mafarisayo wakasema, "Mtu huyu hakutoka kwa Mungu, maana hashiki sheria
ya Sabato." Lakini wengine wakasema, "Mtu mwenye dhambi awezaje
kufanya ishara za namna hii?" Kukawa na mafarakano kati yao.
17
Wakamwuliza tena huyo mtu aliyekuwa kipofu, "Maadam yeye amekufungua
macho, wasemaje juu yake?" Naye akawaambia, "Yeye ni nabii!"
18
Viongozi wa Wayahudi hawakusadiki kwamba mtu huyo alikuwa kipofu hapo awali na
sasa anaona mpaka walipowaita wazazi wake.
19 Basi,
wakawauliza hao wazazi, "Je, huyu ndiye mtoto wenu ambaye ninyi mwasema
alizaliwa kipofu? Sasa amepataje kuona?"
20 Wazazi
wake wakajibu, "Tunajua kwamba huyu ni mtoto wetu, na kwamba alizaliwa
kipofu.
21 Lakini
amepataje kuona, hatujui; na wala hatumjui yule aliyemfumbua macho. Mwulizeni
yeye mwenyewe; yeye ni mtu mzima, anaweza kujitetea mwenyewe."
22 Wazazi
wake walisema hivyo kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi kwani viongozi
hao walikuwa wamepatana ya kwamba mtu yeyote atakayekiri kwamba Yesu ni Kristo
atafukuzwa nje ya sunagogi.
23 Ndiyo
maana wazazi wake walisema: "Yeye ni mtu mzima, mwulizeni."
24 Basi,
wakamwita tena aliyekuwa kipofu, wakamwambia, "Sema ukweli mbele ya Mungu!
Sisi tunajua kwamba mtu huyu ni mwenye dhambi."
25 Yeye
akajibu, "Kama ni mwenye dhambi mimi sijui. Lakini kitu kimoja najua:
Nilikuwa kipofu, na sasa naona."
26 Basi,
wakamwuliza, "Alikufanyia nini? Alikufumbuaje macho yako?"
27 Huyo
mtu akawajibu, "Nimekwisha waambieni, nanyi hamkusikiliza; kwa nini
mwataka kusikia tena? Je, ninyi pia mnataka kuwa wafuasi wake?"
28 Lakini
wao wakamtukana wakisema, "Wewe ni mfuasi wake; sisi ni wafuasi wa Mose.
29 Sisi
tunajua kwamba Mungu alisema na Mose, lakini mtu huyu hatujui ametoka
wapi!"
30 Naye
akawajibu, "Hili ni jambo la kushangaza! Ninyi hamjui ametoka wapi, lakini
amenifumbua macho yangu!
31 Tunajua
kwamba Mungu hawasikilizi watu wenye dhambi, ila humsikiliza yeyote mwenye
kumcha na kutimiza mapenzi yake.
32 Tangu
mwanzo wa ulimwengu haijasikika kwamba mtu ameyafumbua macho ya mtu aliyezaliwa
kipofu.
33 Kama
mtu huyu hakutoka kwa Mungu, hangeweza kufanya chochote!"
34 Wao
wakamjibu, "Wewe ulizaliwa na kulelewa katika dhambi; unawezaje kutufundisha
sisi?" Basi, wakamfukuzia mbali.
35 Yesu
alisikia kwamba walikuwa wamemfukuzia mbali, naye alipomkuta akamwuliza,
"Je, wewe unamwamini Mwana wa Mtu?"
36 Huyo
mtu akajibu, "Mheshimiwa, niambie yeye ni nani, ili nipate
kumwamini."
37 Yesu
akamwambia, "Umekwisha mwona, naye ndiye anayesema nawe sasa."
38 Basi,
huyo mtu akasema, "Ninaamini Bwana!" Akamsujudia.
39 Yesu
akasema, "Mimi nimekuja ulimwenguni kutoa hukumu, kusudi wasioona wapate
kuona, na wale wanaoona wawe vipofu."
40 Baadhi
ya Mafarisayo waliokuwa pamoja naye walisikia maneno hayo, wakamwuliza,
"Je, sisi pia ni vipofu?"
41 Yesu
akawajibu, "Kama mngekuwa vipofu, hamngekuwa na hatia; lakini sasa ninyi
mwasema: `Sisi tunaona`, na hiyo yaonyesha kwamba mna hatia bado.
|